Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutumia Dawa Vibaya

Kutumia Dawa Vibaya

 Kutumia Dawa Vibaya

“NILIANZA kutumia dawa kwa ajili ya matibabu nilipokuwa na umri wa miaka 14,” akasema mwanamke anayeitwa Lena. * “Nilitamani kuwa na mwili mwembamba unaovutia, kwa hiyo daktari wa familia akanipa dawa za kupunguza uzito. Nilijihisi vizuri wakati tu nilipowavutia vijana. Mwishowe nikaanza kutumia dawa za kulevya na kuishi maisha mapotovu. Kila wakati nilikuwa nikijitahidi kulewa kabisa.”

Mwanamke anayeitwa Myra alikuwa na ugonjwa wa kipanda-uso, kwa hiyo daktari wake akampa dawa za kutuliza maumivu. Baada ya muda, akaanza kumeza dawa nyingi zaidi, si kwa ajili ya kutuliza maumivu tu bali pia ili kutosheleza uraibu wake. Isitoshe, alianza kumeza dawa za washiriki wengine wa familia yake.

Ripoti zinaonyesha kwamba idadi inayoongezeka ya vijana na watu wazima wanatumia vibaya dawa zinazopendekezwa na daktari. Wanazitumia ili kujituliza, kukabiliana na mahangaiko, kuwa macho, kupunguza uzito, au kulewa. Dawa zinazotumiwa vibaya mara nyingi ni zile zinazopatikana nyumbani: dawa za kutuliza maumivu, za kutuliza akili, za kuchochea utendaji wa mwili, na za kumsaidia mtu alale. * Pia, watu hutumia vibaya dawa zinazouzwa bila maagizo ya daktari kama zile za kumsaidia mtu alale, za kuzibua pua, na za mizio.

Tatizo hilo limeenea sana na linazidi kuongezeka. Kwa mfano, katika sehemu fulani za Afrika, Ulaya, na Asia Kusini, watu wanatumia vibaya dawa za kitiba kuliko vile wanavyotumia dawa za kulevya. Nchini Marekani, matumizi mabaya ya dawa za kitiba yanazidi matumizi ya dawa zote za kulevya isipokuwa dawa mbalimbali zinazotokana na bangi. Kulingana na ripoti ya gazeti la hivi karibuni, idadi inayoongezeka ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 17 “wanatumia vibaya dawa zinazopendekezwa na daktari kuliko wanavyotumia kokeini, heroini, na metamfetamini zikiwa pamoja.” Kwa kweli, watu wanatumia sana dawa hizo hivi kwamba wamefanya kuwe na biashara ya dawa bandia za kitiba.

Wewe na watoto wako mnaweza kujilinda jinsi gani msitumie dawa vibaya, iwe ni zile zinazopendekezwa na daktari au za kulevya? Makala zinazofuata zitajibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Majina katika makala hizi yamebadilishwa.

^ fu. 4 Mambo yanayozungumziwa katika makala hizi yanaweza kutumika pia kuhusu dawa za kulevya na kutumia kileo vibaya.

[Sanduku katika ukurasa wa 3]

“Uraibu wa dawa huonekana mtu anaposhindwa kujizuia kuzitumia, anapozitumia kwa sababu zisizo za kitiba, na anapoendelea kuzitumia licha ya kupata madhara au kujua hatari ya kuzitumia,” linasema jarida Physicians’ Desk Reference. Uraibu huonekana mtu anapokosa kujidhibiti na anapopendezwa kupita kiasi na dawa hizo.

Utegemezi wa kimwili huonekana mtu anapoathirika kwa sababu ya kuacha kutumia dawa fulani aliyopendekezewa na daktari. Hilo ni jambo la kawaida na halionyeshi kwamba mtu ni mraibu.

Stahamala ni neno linalotumiwa kuonyesha hali ambayo hutokea mwili unapozoea dawa kabisa hivi kwamba mtu anahitaji kuongezewa kiwango anachotumia ili apunguze maumivu.