Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hifadhi za Pekee za Viumbe Walio Hatarini

Hifadhi za Pekee za Viumbe Walio Hatarini

 Hifadhi za Pekee za Viumbe Walio Hatarini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

MIMEA na wanyama ulimwenguni pote wanakabili hatari ya kutoweka. Wanasayansi fulani wanakadiria kwamba maelfu kati yao hutoweka kila mwaka. Kwa kupendeza, safu za milima huandaa hifadhi salama kwa ajili ya mimea na wanyama waliokuwa wakipatikana katika maeneo mengi. Lakini hata katika hifadhi hizo, uchafuzi na utendaji wa wanadamu umekuwa tisho. Huenda hakuna mahali pengine ambapo hilo linaonekana wazi kuliko katika bara la Ulaya, eneo ambalo lina watu wengi sana duniani.

Katika safu za milima ya Pyrenees iliyo mpakani mwa Ufaransa na Hispania, kuna mbuga kadhaa za taifa ambazo hulinda mimea na wanyama. Katika hifadhi hizo, wageni hupata nafasi ya kuona viumbe wengi wanaokabili hatari ya kutoweka. Acheni tuone kwa ufupi baadhi ya viumbe hao.

Viumbe Wanaokabili Hatari ya Kutoweka

Maua. Baadhi ya maua maridadi zaidi ya mwituni hukua katika maeneo yaliyo mita 1,500 juu ya usawa wa bahari. Maua yanayoitwa kikoroga-maziwa aina ya snow na trumpet (1), yenye petali za rangi nyangavu ya bluu, hutanda maeneo ya juu ambako hakuna miti. Chini zaidi, kati ya miti inayoitwa mifune, maua ya okidi yaliyo hatarini yanayoitwa sapatu ya mama (2) bado yanapatikana. Mamia ya watu wanaopendezwa na mazingira hutembelea eneo hilo kila mwaka kwa hiyo, walinzi wa misitu hulinda mimea hiyo kwa saa 14 kila siku ili kuhakikisha kwamba maua hayo yenye thamani hayaharibiwi au kung’olewa.

Vipepeo. Maeneo ya malisho ya milimani huwa na maua mengi ya mwituni ambako vipepeo wengi maridadi huishi. Kipepeo mkubwa anayeitwa Apollo (3), mwenye mabawa yenye madoa mekundu maangavu hurukaruka kati ya michongoma. Vipepeo wanaoitwa blue na copper (4) wa jamii ya Lycaenidae hutua kwenye maua madogo. Vipepeo wanaoitwa painted-lady na tortoiseshell hurukaruka kwenye maeneo ya juu zaidi.

Wanyama. Wakati mmoja wanyama wengi wakubwa wa Ulaya walikuwa wakiishi katika maeneo mengi ya bara hilo. Lakini watu wamewawinda sana baadhi yao hivi kwamba wanakaribia kutoweka. Mbwa-mwitu, dubu, simba-mangu (5), nyatisinga, chamois, na paa-mbuzi (6) sasa wanapatikana tu katika milima fulani au katika eneo la kaskazini ya mbali. Wanyama hao wakubwa katika hifadhi hizo za safu za milima ya Pyrenees zinawakumbusha watu kuhusu wanyama mwitu wengi ambao wakati mmoja waliishi katika milima hiyo. Wageni fulani hujiuliza ikiwa wanyama waliobaki wataendelea kuwapo.

Tuna kila sababu ya kuwa na hakika kwamba Muumba, Yehova, Yule “ambaye vilele vya milima ni vyake,” anawajali viumbe wake wa milimani. (Zaburi 95:4) Katika zaburi moja, Mungu anasema: “Kila mnyama wa mwituni ni wangu, wanyama walio juu ya milima elfu moja. Najua vizuri kila kiumbe chenye mabawa cha milimani.” (Zaburi 50:10, 11) Tuna kila sababu ya kuamini kwamba Yehova hataruhusu wanyama wa milimani watoweke kwa kuwa anaijali dunia na viumbe wanaoishi humo.

 [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

La Cuniacha