Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fumbo Kubwa la Kisayansi Lafumbuliwa

Fumbo Kubwa la Kisayansi Lafumbuliwa

 Fumbo Kubwa la Kisayansi Lafumbuliwa

WAPIGA-MBIZI walipochunguza meli iliyozama kwenye ufuo wa kisiwa cha Ugiriki kinachoitwa Antikýthēra katika mwaka wa 1901, walipata vitu vyenye thamani. Meli hiyo ilikuwa ya kibiashara ya Waroma wa kale na ilikuwa imebeba vitu vingi kutia ndani, sanamu za marumaru na shaba na pia sarafu za fedha kutoka Pergamamu. Sarafu hizo ziliwawezesha wachunguzi kukadiria kwamba meli hiyo, ambayo huenda ilikuwa ikielekea Roma, ilizama kati ya mwaka wa 85 na 60 K.W.K.

Tangu vitu hivyo vilipogunduliwa, vilihifadhiwa katika Jumba la Makumbusho ya Akiolojia la Kitaifa la Athens, Ugiriki. Hata hivyo, mnamo 2005, wataalamu hawakwenda kwenye jumba hilo la makumbusho kuchunguza sanamu wala sarafu hizo. Walipendezwa hasa na kifaa fulani cha shaba ambacho awali kilikuwa ndani ya kisanduku kidogo cha mbao. Kifaa hicho, kinachojulikana kama Kifaa cha Antikythera (Antikythera Mechanism), kinaonyesha kwamba huenda watu wa kale walikuwa na ujuzi mwingi wa kisayansi kuliko inavyodhaniwa. Kifaa hicho kimesemekana kuwa “kifaa kilichobuniwa kwa njia tata zaidi katika ulimwengu wa kale.”

Hicho ni kifaa cha aina gani? Na kwa nini ni muhimu sana?

Kifaa Kisichojulikana

Kisanduku kilichokuwa na kifaa hicho kilipotolewa kwenye sakafu ya bahari, kilikuwa kimeliwa sana na kutu. Baada ya karibu miaka 2,000, kilifanana na jiwe la rangi ya kijani. Mwanzoni kifaa hicho kisichojulikana kilipuuzwa kwa kuwa watu walisisimuka zaidi kuhusu sanamu zilizokuwa zimepatikana.

Mnamo 1902, mtaalamu Mgiriki wa kuchunguza vitu vya kale alipochunguza kifaa hicho, kilikuwa katika vipande kadhaa. Kilikuwa na magurudumu ya gia yenye ukubwa mbalimbali, na meno ya gia yaliyokatwa kwa usahihi sana katika umbo la pembetatu. Kifaa hicho kilifanana na saa. Lakini kwa kuwa inaaminiwa kwamba ufundi wa kutengeneza saa haukutumika sana hadi miaka 700 hivi iliyopita, ilionekana kuwa hakiwezi kuwa saa.

Makala moja kuhusu kifaa hicho inaeleza kwamba “kwa kawaida wanahistoria hawaamini kwamba [Wagiriki walioishi miaka 2,000 hivi iliyopita] walikuwa na ujuzi wa kutengeneza gia zilizokatwa kwa usahihi sana kisayansi, yaani, gia zilizokatwa kutoka kwa chuma na kupangwa katika njia tata inayoweza kuzungusha mhimili mmoja kwa kutumia mhimili mwingine.” Isitoshe, kifaa hicho kilidhaniwa kuwa aina fulani ya chombo kilichotumiwa kuchunguza latitudo kwa kutegemea mahali jua, mwezi, sayari nyingine, na nyota zilipokuwa.

Pia, wengi walisema kwamba gia hizo zilikuwa tata sana hivi kwamba kifaa hicho hakingeweza kuwa kilibuniwa miaka 2,000 iliyopita. Kwa hiyo, wakaamua kwamba hakikuwa katika meli hiyo ya kale iliyozama. Kwa upande mwingine, msomi mmoja alidokeza kwamba huenda kifaa hicho kilikuwa  Duara ya Archimedes inayojulikana sana. Kifaa hicho kilifafanuliwa na Cicero katika karne ya kwanza K.W.K. kuwa kifaa kinachoonyesha miendo ya jua, mwezi, na sayari tano zinazoweza kuonekana bila kutumia darubini. Hata hivyo, kwa kuwa hakukuwa na uthibitisho mwingine, wazo la kwamba kilikuwa kifaa cha kuchunguza latitudo liliendelezwa.

Kinachunguzwa kwa Uangalifu Zaidi

Mnamo 1958, kifaa hicho kilichunguzwa na Derek de Solla Price, ambaye alikuwa amesomea fizikia kisha akabadili taaluma yake na kuwa profesa wa historia. Aliamini kwamba kifaa hicho kilikuwa na uwezo wa kutambua matukio ya wakati uliopita au wakati ujao, kama vile wakati wa mwezi mpevu utakapoonekana. Aligundua kwamba maandishi yaliyokuwa kwenye uso wa kifaa hicho yaliwakilisha migawanyo katika kalenda, yaani, siku, miezi, na ishara za nyota. Price alidai kwamba wakati mmoja kifaa hicho kilikuwa na vishale vilivyozunguka vikionyesha mahali jua, mwezi, na nyota zilikuwa wakati mbalimbali.

Price alisema kwamba lile gurudumu kubwa kabisa la gia liliwakilisha mzunguko wa jua na kwamba mzunguko mmoja ulikuwa sawa na mwaka mmoja. Ikiwa gia nyingine, iliyounganishwa kwenye ile ya kwanza, iliwakilisha mzunguko wa mwezi, basi wastani wa idadi ya meno katika magurudumu hayo mawili ulionyesha maoni ya Wagiriki wa kale kuhusu mizunguko ya mwezi.

Mnamo 1971, Price alichunguza kifaa hicho kwa kutumia eksirei. Matokeo yalithibitisha nadharia yake. Kifaa hicho kilitumiwa kuhesabu miendo ya nyota. Price alichora picha ya jinsi alivyofikiri kifaa hicho kinafanya kazi na akachapisha matokeo ya uchunguzi wake mnamo 1974. Aliandika hivi: “Hakuna kifaa kama hiki kilichohifadhiwa mahali popote. . . . Kutokana na yote tunayojua kuhusu sayansi na tekinolojia katika Enzi za Wagiriki hatungefikiria kwamba kungekuwa na kifaa kama hicho.” Wakati huo, uchunguzi wa Price haukupata sifa kama ulivyostahili. Hata hivyo, wengine waliendeleza uchunguzi wake.

 Habari Zaidi

Mnamo 2005, kikundi cha wachunguzi waliotajwa mwanzoni mwa makala hii walichunguza kifaa hicho kwa kutumia mashine ya kupiga eksirei ya hali ya juu inayoitwa CAT-scan. Uchunguzi huo ulitoa habari zaidi juu ya jinsi kifaa hicho kinavyofanya kazi. Kadiri mtu alivyozungusha kidude fulani, ndivyo magurudumu 30 hivi ya gia yalivyoendesha vishale vitatu vilivyokuwa mbele na nyuma ya kisanduku hicho. Hilo lilimwezesha mtumiaji wa kifaa hicho kutabiri mizunguko ya jua, mwezi, na nyota, kutia ndani kupatwa kwa jua na mwezi, kwa kulinganisha na kipindi cha miaka minne kati ya michezo ya Olimpiki na michezo mingine ya Kigiriki. Michezo hiyo ilitumiwa kama msingi wa kuhesabu wakati.

Kwa nini habari hiyo ilikuwa muhimu sana? Kuna sababu kadhaa. Elimu ya nyota ilikuwa muhimu kwa sababu watu wa kale walitumia jua na mwezi kama kalenda za kuwajulisha wakulima wakati wa kupanda mbegu. Mabaharia walitumia nyota kuwaonyesha njia. Jamii za Kigiriki zilitegemea sana miendo ya nyota. Na kuna sababu nyingine kwa nini habari hiyo ilikuwa muhimu sana.

“Wababiloni wa kale waliona ni jambo muhimu sana kutabiri wakati wa kupatwa kwa jua, kwa sababu ilidhaniwa kwamba matukio hayo yaliashiria mabaya,” akaandika Martin Allen, wa Mradi wa Kuchunguza Kifaa cha Antikythera. “Kwa kweli, kifaa hicho kimedhaniwa kuwa kilikuwa kifaa cha kisiasa kilichowawezesha watawala kudhibiti raia wao. Pia imesemekana kwamba sababu inayofanya tujue machache sana kuhusu vifaa hivyo, ni kwa sababu vilikuwa siri ya wanajeshi au ya wanasiasa.”

Ingawa tunaweza kujifunza mambo mengine mengi kutokana na kifaa hicho, ubuni wake unathibitisha kwamba elimu ya nyota na ya hesabu ya Wagiriki wa kale, ambayo hasa ilitokana na Wababiloni, ilikuwa ya hali ya juu kuliko tunavyoweza kuwazia. Gazeti Nature linasema hivi: “Kifaa cha kale cha Antikythera hakisahihishi tu maoni yetu kuhusu maendeleo ya kitekinolojia katika muda wa karne zilizopita bali pia kinatutolea habari zaidi za kihistoria.”

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

NI NANI ALIYEKITENGENEZA?

Kulikuwa na vifaa vingine vilivyofanana na Kifaa cha Antikythera. “Huwezi kuona makosa yoyote,” anaandika Martin Allen. “Sehemu zote za kifaa hicho zina kusudi maalumu. Hakuna mashimo ya ziada, au vipande vya chuma vinavyoonyesha kwamba aliyekitengeneza aliboresha kifaa hicho alipokuwa akikitengeneza. Hilo linatufanya tukate kauli kwamba alitengeneza vifaa vingine kadhaa kabla ya kutengeneza kifaa hicho.” Kwa hiyo ni nani aliyekitengeneza? Na vifaa vingine alivyotengeneza vilienda wapi?

Uchunguzi wa karibuni zaidi wa kifaa hicho umeonyesha majina ya miezi kwenye vishale vilivyotabiri kupatwa kwa jua na mwezi. Majina hayo yalitoka Korintho. Hilo liliwafanya wachunguzi kufikia mkataa kwamba kifaa hicho kilitengenezwa na kutumiwa na watu wa utamaduni fulani hususa. Gazeti la kisayansi linaloitwa Nature linasema: “Inaonekana kwamba watu katika vijiji vya Wakorintho vya upande wa kaskazini-magharibi mwa Ugiriki au vya Sirakusa huko Sisili ndio waliotumia kifaa hicho, na ikiwa kilitumiwa huko Sirakusa, basi huenda kilitumiwa wakati wa Archimedes.”

Kwa nini vifaa vingine kama hivyo havijadumu hadi leo? “Shaba ni madini yenye thamani na yanaweza kutumiwa tena,” anaandika Allen. “Kwa hiyo, si rahisi kupata vifaa vya zamani vya shaba. Kwa kweli, vifaa vingi muhimu vya shaba vimepatikana majini, mahali ambapo havingeweza kupatikana na wale ambao wangetaka kutumia tena madini hayo.” “Tuna kifaa hiki peke yake,” akasema mchunguzi mmoja, “kwa kuwa hakingeweza kupatikana na watu ambao wangekiyeyusha na kutumia tena madini yake.”

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sehemu za ndani zilizounganishwa upya za Kifaa cha Antikythera

1. Kishale cha mbele kilionyesha mzunguko wa mwezi, mahali jua na mwezi zilipokuwa. Pia ilionyesha siku na mwezi kulingana na kalenda ya jua na mwendo wa jua (na sayari zinazoonekana) kwa kupatana na ishara za nyota

2. Kishale cha juu cha nyuma kililinganisha muda kati ya miezi, miaka, na muda kati ya michezo ya Kigiriki

3. Kishale cha chini cha nyuma kilitabiri kupatwa kwa jua na mwezi

[Picha]

Sehemu ya mbele

Sehemu ya nyuma

[Hisani]

Both photos: ©2008 Tony Freeth/Antikythera Mechanism Research Project (www.antikythera-mechanism.gr)

[Picha katika ukurasa wa 26]

Huenda bamba la nyuma lilionekana hivi

[Hisani]

©2008 Tony Freeth/Antikythera Mechanism Research Project (www.antikythera-mechanism.gr)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

All photos: ©2005 National Archaeological Museum/Antikythera Mechanism Research Project (www.antikythera-mechanism.gr)