Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ngao za Dunia Zenye Nguvu

Ngao za Dunia Zenye Nguvu

 Ngao za Dunia Zenye Nguvu

ANGA za juu ni eneo hatari lililojaa mnururisho wenye sumu na vimondo. Hata hivyo, ni kana kwamba sayari yetu ya bluu inasonga katikati ya mawe hayo yanayoanguka bila kupata madhara mengi. Kwa nini? Kwa sababu dunia imekingwa na ngao za ajabu, yaani, nguvu za sumaku za dunia na anga-hewa.

Nguvu za sumaku za dunia zinatoka ndani kabisa ya sayari hii na zinaenea kwenye anga za juu ambako zinafanyiza ngao isiyoonekana inayoitwa magnetosphere (picha upande wa kulia). Ngao hiyo inatukinga kutokana na mnururisho mwingi kutoka angani na hatari kutoka kwa jua. Hatari hizo zinatia ndani upepo wenye chembechembe zenye nishati; milipuko kutoka sehemu fulani ndogo ya jua ambayo inatokeza nishati inayolingana na mabilioni ya mabomu ya hidrojeni; na vilevile milipuko kutoka sehemu ya juu ya jua (CME) ambayo hurusha mabilioni ya tani ya mata katika anga za juu. Milipuko kutoka kwa jua hutokeza mimweko yenye rangi zenye kupendeza (picha upande wa kulia chini) zinazoonekana kwenye anga-hewa karibu na ncha za dunia zenye sumaku.

Anga-hewa ya dunia inakinga dunia pia. Sehemu ya juu ya dunia inayoitwa stratosphere, ina aina fulani ya oksijeni ambayo inaitwa ozoni inayofyonza asilimia 99 ya mnururisho wa urujuanimno. Hivyo, ozoni inasaidia kukinga viumbe vingi, kutia ndani wanadamu na uduvi, kutokana na mnururisho hatari. Kwa kupendeza, kiwango cha ozoni kinalingana na mnururisho wa urujuanimno na hivyo kuifanya iwe ngao yenye nguvu na inayofaa kabisa.

 Pia, angahewa hutukinga kutokana na mamilioni ya vimondo vidogo na vikubwa. Vimondo vingi huteketea angani na kutokeza mwangaza unaoitwa nyota-mkia.

Ngao za dunia hazizuii mnururisho ambao ni muhimu kwa uhai kama vile joto na mwangaza. Angahewa hata inasaidia kusambaza joto duniani, na usiku inakuwa kama blanketi inayozuia joto lisitoke haraka.

Kwa kweli, angahewa na nguvu za sumaku za dunia ni maajabu ya ubuni ambayo bado hayajaeleweka kikamili. Tunaweza kusema pia kwamba maji mengi sana yaliyo duniani ni ubuni wa ajabu.