Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

 Kuutazama Ulimwengu

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, idadi ya misiba ya asili ulimwenguni imeongezeka mara nne. Watu zaidi ya milioni 250 huathiriwa kila mwaka.—EL UNIVERSAL, MEXICO.

“Kwa miaka mingi, pepo za msimu, ambazo ndizo pepo zenye nguvu kwenye Pasifiki, zimekusanya rundo kubwa la takataka zinazoelea.” Kwa sasa, eneo linalofunikwa na rundo hilo linatoshana na nchi ya Australia.—LA DÉPÊCHE DE TAHITI, TAHITI.

Kilo 200 za mahindi zinahitajika ili kutokeza lita 50 za mafuta kwa ajili ya gari ndogo. Chakula hicho “kinatosha kulisha mtu mmoja kwa mwaka mzima!”—GAZETA WYBORCZA, POLAND.

Biblia Zinazochapishiwa Nchini China

“China imekuwa mojawapo ya nchi zinazochapisha Biblia nyingi zaidi ulimwenguni,” anasema Ye Xiaowen, kiongozi wa Usimamizi wa Kitaifa wa Masuala ya Kidini. Kampuni ya Kichina ya uchapishaji iliyo Nanjing, mji mkuu wa Jimbo la Jiangsu, ilifikia kilele cha uchapishaji wa Biblia nchini humo ilipochapisha nakala ya milioni 50 ya Biblia nzima. Kulingana na gazeti People’s Daily Online, “katika miaka ya karibuni, [kampuni] hiyo imekuwa ikichapisha nakala milioni 3 hivi za Biblia kila mwaka.” Inaripotiwa kwamba idadi ya watu wanaodai kuwa Wakristo nchini China inaongezeka.

Sanamu Zaibiwa

“Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, kumekuwa na wizi katika zaidi ya makanisa 1,000 nchini Urusi,” linaripoti gazeti Russky Newsweek. Wizara ya Masuala ya Ndani ya Urusi imepata ripoti kwamba sanamu 40,000 hivi zimeibiwa. Sasa, kutokana na makubaliano kati ya Wizara hiyo na Kanisa Othodoksi la Urusi, sanamu zote za kanisa zitatiwa alama ya kuzitambulisha ambayo itaonekana tu kwa kutumia mwangaza wa urujuanimno. Hilo litawasaidia wapelelezi kutambua wamiliki halali wa sanamu zitakazopatikana. Gazeti Russky Newsweek linasema kwamba Baraza la Makasisi la Moscow linaunga mkono uamuzi huo “kwa kuwa alama hizo za ‘kidunia’ hazitaathiri uwezo wa kufanya miujiza wa sanamu hizo.”

Pesa za Afrika Zaishia Vitani

“Kati ya 1990 na 2005, nchi 23 za Afrika zilihusika katika vita ambavyo viligharimu jumla ya dola bilioni 300 hivi za Marekani,” linasema gazeti International Herald Tribune. “Pesa ambazo Afrika inatumia zinaweza kutumiwa kugharimia matibabu ya UKIMWI, ama kugharimia elimu, maji, kuzuia na kutibu kifua kikuu na malaria,” anasema Ellen Johnson-Sirleaf, Rais wa Liberia. “Maelfu ya hospitali, shule, na barabara zingeweza kujengwa.” Gazeti hilo linamalizia kwa kusema kwamba kama hakungekuwa na vita Afrika “bara hilo lingekuwa na maendeleo badala ya kuwa bara maskini zaidi ulimwenguni.”

Kulala Kidogo Mchana Kunaweza Kukusaidia

Uchunguzi uliofanyiwa wanaume na wanawake Wagiriki zaidi ya 23,000 ulionyesha kwamba kulala kidogo mchana angalau mara tatu kwa juma kunaweza kupunguza kwa asilimia 37 hatari ya kufa kutokana na mshtuko wa moyo. “Kuna uthibitisho wa kutosha unaoonyesha kwamba mfadhaiko mkali na ule wa muda mrefu unaweza kusababisha ugonjwa wa moyo,” anaeleza Dimitrios Trichopoulos, ambaye ni mtafiti na mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza katika Shule ya Afya ya Umma ya Harvard, huko Marekani. Anasema kwamba “kulala kidogo mchana kunaweza kupunguza mfadhaiko na vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo.”