Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Miti Inayokua Majini

Miti Inayokua Majini

Miti Inayokua Majini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

Ni makao ya mamalia, ndege, na reptilia wengi walio katika hatari ya kutoweka. Pia inahifadhi mazingira kwa kuchuja maji. Huko Florida kusini, nchini Marekani, asilimia 75 hivi ya samaki wanaovuliwa na watu ili kujifurahisha na asilimia 90 ya samaki wanaovuliwa kwa ajili ya biashara huitegemea. Pia inazuia maeneo ya pwani yasiharibiwe na dhoruba na mawimbi. Ni nini hiyo? Ni mikoko!

MIKOKO ni aina ya miti au vichaka vinavyopatikana katika zaidi ya nusu ya fuo za bahari za maeneo ya kitropiki ulimwenguni. Kuna jamii mbalimbali za mikoko. Kwa kawaida, miti hiyo hukua katika sehemu za fuo zilizo na mchanganyiko wa maji ya bahari na maji baridi katika maeneo ambako mikondo yenye nguvu hukutana na ile isiyo na nguvu. Ingawa mimea mingi haiwezi kukua katika maji hayo yenye chumvi nyingi, mikoko hukua huko kwa urahisi. Jinsi gani? Kwa kutumia mbinu mbalimbali zenye kustaajabisha na nyakati nyingine zaidi ya mbinu moja wakati uleule.

Imezungukwa na Chumvi

Mikoko fulani huwa na vichujio vinavyozuia chumvi isiingie ndani ya mizizi. Vichujio hivyo huchuja kabisa chumvi hivi kwamba msafiri mwenye kiu anaweza kupata maji yasiyo na chumvi kwa kupasua mizizi ya mikoko hiyo. Jamii nyingine za mikoko huacha chumvi iingie kisha huikusanya na kuitoa kupitia majani yaliyozeeka au sehemu nyingine za miti hiyo ambazo huanguka.

Jamii nyingine huingiza chumvi na kuiondoa mara moja kupitia majani yake. Ukiramba jani la mkoko huo, utapata kwamba lina chumvi nyingi sana. Lakini uwe mwangalifu unaporamba majani ya mikoko fulani! Utomvu wa majani hayo unaweza kukupofusha kwa muda ukiingia ndani ya jicho. Hata hivyo, utomvu huo hutumiwa kuwatibu watu vidonda na wanapoumwa na wadudu.

Jinsi Inavyostahimili Hali

Ili isitawi, mimea mingi huhitaji udongo unaopitisha hewa vizuri. Lakini kwa kawaida mikoko hukua kwenye udongo uliolowa maji. Siri ni mizizi yake inayokua juu ya udongo na hivyo kuingiza hewa moja kwa moja. Mizizi hiyo ni ya aina mbalimbali. Mizizi fulani inaitwa mizizi ya magoti kwa kuwa inakua kutoka katika udongo kisha inajipinda na kurudi udongoni na hivyo kuonekana kama magoti yaliyokunjwa.

Aina nyingine ya mizizi hukua wima kutoka katika udongo na kuwa sambamba na shina la mti. Kuna mizizi mingine ambayo baadaye huutegemeza mkoko inayokua kutoka kwenye sehemu ya chini ya shina. Pia mizizi mingine hukua kutoka sehemu ya chini ya mti ikijipinda-pinda kama nyoka na sehemu yake ya juu ikitokea juu ya udongo. Aina hizo mbalimbali za mizizi zinaiwezesha miti kupumua na pia zinaitegemeza katika udongo mwororo.

Jinsi Inavyozaana

Aina fulani ya mikoko ina matunda makubwa ya mviringo yaliyojaa mbegu. Matunda hayo yanapoiva, hupasuka na kutawanya mbegu zake majini. Baadhi ya mbegu hizo hubebwa na mawimbi, na mwishowe kupata mahali pa kuotea.

Mbegu za mikoko mingine huota zikiwa bado kwenye tunda. Hilo ni jambo lisilo la kawaida hata kidogo kwa mimea. Mikoko hiyo hutokeza miche ambayo hukatika na kuanguka majini. Miche hiyo inaweza kuelea majini kwa miezi kadhaa au hata kwa mwaka mzima ikitafuta mahali panapofaa kuota.

Jinsi miche hiyo inavyoelea hufanya iwe rahisi zaidi kupata mahali panapofaa kuota, yaani, mahali palipo na mchanganyiko wa maji ya chumvi na maji baridi. Miche hiyo huelea ikiwa chali kwenye maji ya chumvi, lakini inapofika kwenye maji yaliyochanganyika, hiyo huelea ikiwa wima na hivyo kufanya iwe rahisi kujipandikiza matopeni.

Makao ya Viumbe Wengi

Mikoko hufanyiza msingi wa mfumo tata wa kutokeza chakula. Majani na sehemu nyingine za miti hiyo huoza na kuwa chakula cha viumbe wenye chembe moja ambao huliwa na wanyama wengine. Viumbe wengi huishi, hula, huzaliana, au kulea watoto wao katika misitu ya mikoko.

Kwa mfano, jamii nyingi za ndege hujenga viota au kutafuta chakula katika misitu ya mikoko, na pia hupumzika huko wakati wa kuhama. Katika misitu ya mikoko huko Belize pekee, kuna jamii zaidi ya 500 za ndege. Samaki wengi huanza maisha yao katika misitu hiyo au hutegemea mfumo wa ekolojia wa mikoko kwa ajili ya chakula. Samaki wa jamii zaidi ya 120 wamevuliwa katika msitu wa mikoko wa Sundarbans, ulio kati ya India na Bangladesh.

Mimea mingi pia hukua katika misitu ya mikoko. Katika pwani ya mashariki ya Australia, jamii 105 za kuvu zimepatikana zikikua kwenye mikoko. Pia, mikangaga, okidi, milimbo, na mimea mingine hukua kwa wingi katika misitu hiyo. Kwa kweli, mikoko ulimwenguni pote ni muhimu sana kwa mimea na wanyama wa aina mbalimbali, kutia ndani kuvu, simbamarara, na hata wanadamu.

Inawafaidi Sana Wanadamu

Mbali na kusaidia kuhifadhi mazingira, mikoko hutokeza vitu vingi moja kwa moja au kwa njia nyingine. Kwa mfano kuni, makaa, tanini, chakula cha mifugo, na dawa. Pia, maeneo yenye mikoko hutokeza chakula kitamu kama vile samaki, krasteshia, moluska, na asali. Wakati mmoja, mabaharia fulani walidhani kwamba chaza hukua kwenye miti kwa sababu wangewakusanya kwa urahisi kutoka kwenye mizizi ya mikoko iliyoonekana baada ya maji kupungua.

Mikoko pia hutokeza mali-ghafi kwa ajili ya viwanda vya karatasi, nguo, ngozi, na katika ujenzi. Pia biashara za uvuvi na utalii hufaidika kutokana na mikoko.

Ingawa mikoko inazidi kuthaminiwa, inakadiriwa kwamba kila mwaka, misitu ya mikoko yenye ukubwa wa zaidi ya kilomita 1,000 za mraba huharibiwa. Mara nyingi inakatwa ili kupata ardhi kwa ajili ya miradi inayoonekana kuwa yenye faida zaidi, kama vile kilimo na ujenzi wa nyumba. Watu wengi huona vinamasi vya mikoko kuwa maeneo yanayofaa kuepukwa kwa sababu yana matope, uvundo, na mbu wengi.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba mikoko ni muhimu na hata huokoa uhai. Mizizi yake ya pekee yenye kufaana na hali, inayopitisha hewa na kuchuja chumvi, imetokeza mifumo tata ya ekolojia iliyo na viumbe wengi. Mikoko ni muhimu kwa uvuvi, wanyama mwitu, na biashara ya bidhaa za mbao. Na pia inazuia mmomonyoko wa udongo kwenye fuo za bahari kwa kupunguza nguvu za vimbunga vikubwa vinavyoweza kuua maelfu ya watu. Kwa kweli, tunapaswa kuithamini mikoko!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Kutafuta Asali Katika Misitu ya Mikoko

Misitu mikubwa zaidi ya mikoko ulimwenguni iko huko Sundarbans, ambayo ni sehemu ya Delta kubwa ya Ganges, iliyo kati ya India na Bangladesh. Baadhi ya watu wanaoishi huko ni Wamowalisi wanaotegemea sana misitu ya mikoko. Wao hufanya mojawapo ya kazi hatari zaidi nchini humo.

Wamowalisi hutafuta asali msituni. Kila mwaka, katika miezi ya Aprili (Mwezi wa 4) na Mei, wao huenda kwenye misitu ya mikoko kutafuta masega ya asali ya nyuki wakubwa. Nyuki hao ni wakubwa sana, na wanaweza kufikia kimo cha zaidi ya sentimita tatu. Ni wakali sana, na hata wamewahi kuua ndovu!

Kwa sababu hiyo, watafutaji wa asali hubeba mienge ya matawi ya mikoko na moshi wake hufukuza nyuki. Watafutaji wenye hekima wa asali huacha sehemu fulani ya mzinga ili nyuki wajenge tena na kutokeza asali mwaka baada ya mwaka.

Si nyuki tu walio tishio kwa watafutaji hao wa asali. Wao hukabili hatari ya kushambuliwa na mamba au nyoka wenye sumu wanaoishi katika misitu ya mikoko. Pia, wezi wanaweza kuwavizia ili kuwanyang’anya asali na nta wanapotoka msituni. Hata hivyo, adui wao mkubwa zaidi ni simbamarara wa Bengal. Kila mwaka, hao simbamarara huua kati ya watafutaji 15 na 20 wa asali.

[Hisani]

Zafer Kizilkaya/Images & Stories

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mikoko na miche yake hukua katika mazingira yanayoweza kuua mimea mingine

[Hisani]

Top right: Zach Holmes Photography/Photographers Direct; lower right: Martin Spragg Photography (www.spraggshots.com)/Photographers Direct