Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Damu Iliyopimwa Ukimwi Ni Salama?

Je, Damu Iliyopimwa Ukimwi Ni Salama?

 Je, Damu Iliyopimwa Ukimwi Ni Salama?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NIGERIA

▪ SWALI hilo lilizuka nchini Nigeria ilipojulikana kwamba msichana mchanga aliambukizwa UKIMWI kupitia damu aliyotiwa mishipani katika hospitali maarufu nchini humo.

Kulingana na msimamizi katika hospitali hiyo, mara tu baada ya kuzaliwa, iligunduliwa kwamba Eniola alikuwa na homa ya nyongo ya manjano. Ilipendekezwa atiwe damu mishipani, na baba yake akatolewa damu ili itumiwe. Lakini kwa kuwa damu ya baba haikupatana na damu ya binti yake, walitumia damu kutoka katika hifadhi ya hospitali hiyo. Baada ya muda mfupi, iligunduliwa kwamba mtoto huyo ana virusi vya UKIMWI, ingawa wazazi wake hawakuwa navyo. Kulingana na hospitali hiyo, “damu aliyotiwa mtoto huyo ilikuwa imepimwa na kupatikana haina virusi vya UKIMWI.”

Hivyo basi, mtoto huyo aliambukizwaje? Serikali ya Nigeria ilifanya uchunguzi na kukata kauli kwamba huenda mtoto huyo aliambukizwa kupitia damu aliyotiwa mishipani. Gazeti Nigerian Tribune lilimnukuu mtaalamu wa virusi aliyesema: “Damu hiyo ilipotolewa, mhusika hakuwa na kinga-mwili za kuonyesha kwamba ana UKIMWI.”

Hicho ni kisa kimoja tu, hata hivyo kinakazia kwamba kutiwa damu mishipani si salama. Vikifafanua kile kipindi ambapo mtu hana kinga-mwili za kutosha kuonyesha ana UKIMWI, Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vinasema: “Inaweza kuchukua muda kabla mfumo wa kinga haujatokeza kinga-mwili za kutosha kuonekana mtu anapopimwa, na muda huo unaweza kutofautiana kati ya watu mbalimbali. Watu wengi hutokeza kinga-mwili zinazoweza kuonekana kati ya majuma 2 hadi 8 (kipindi cha wastani ni siku 25). Hata hivyo, watu fulani wanaweza kuchukua muda mrefu sana kutokeza kinga-mwili zinazoweza kuonekana. . . . Katika visa vichache sana, hilo linaweza kuchukua hata miezi 6.”

Hivyo, hata ingawa damu imepimwa na kupatikana haina virusi vya UKIMWI, huo si uthibitisho wa kwamba ni salama. Shirika la UKIMWI la San Francisco linaonya hivi: “Ingawa huenda virusi vya UKIMWI visigunduliwe mtu anapopimwa wakati wa kipindi cha kutokeza kinga-mwili, virusi hivyo vinaweza kupitishwa wakati huo. Kwa kweli, mara nyingi watu wanaweza kuwaambukiza wengine virusi hivyo kwa urahisi zaidi wakati huo (yaani, muda mfupi baada ya kuambukizwa UKIMWI).”

Kwa miaka mingi, Mashahidi wa Yehova wamefuata mwelekezo wa Biblia wa “kuendelea kujiepusha na . . . damu.” (Matendo 15:29) Ulinzi ambao wamepata kutokana na mwelekezo huo unakazia hekima ya kutii maagizo ya Mungu. Ili kujifunza mengi kuhusu matibabu yanayoweza kutumiwa badala ya kutiwa damu mishipani, tafadhali ona broshua Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako? *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.