Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mafuta Yenye Thamani ya Mediterania

Mafuta Yenye Thamani ya Mediterania

 Mafuta Yenye Thamani ya Mediterania

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

“Nilikuwa na rangi ya kijani, nikabadilika na kuwa mweusi, kisha wakaniponda taratibu, na mwishowe wakanigeuza kuwa dhahabu safi.” —Kitendawili cha zamani cha Hispania.

ZEITUNI inapoiva mtini, rangi yake hugeuka kutoka kijani na kuwa na nyeusi inayong’aa. Lakini ndani ya ganda lake jeusi, mna “dhahabu” iliyo tayari kutolewa. Zinapopondwa, zeituni hutoa umajimaji wenye rangi ya dhahabu ambao umetumiwa kwa maelfu ya miaka huko Mediterania kwa ajili ya chakula. Mafuta hayo ya zeituni ni zao lenye thamani la mizeituni ambayo hukua kwa wingi kwenye milima iliyoko Ureno hadi Siria.

Mafuta ya miti hiyo migumu huwa na ladha nzuri na yanafaa kwa afya. Sikuzote watu wa Mediterania wamezoea kwamba neno “mafuta” humaanisha “mafuta ya zeituni.” Kwa kweli, neno la Kihispania “mafuta,” aceite, linatokana na neno la Kiarabu azzáyt, ambalo linamaanisha “maji ya zeituni.” Na kwa kweli, mafuta hayo ni umajimaji usiochanganywa na chochote wa zeituni zilizopondwa. Ladha, harufu, na ubora wa asili wa zeituni hudumishwa kwa kuwa zinapopondwa  hazihitaji kuongezwa vikolezo au kupitishwa katika utaratibu fulani wa kikemikali.

Mafuta Yasiyo na Kifani

Mwanahistoria Erla Zwingle, anasema kwamba mafuta ya zeituni “yametumiwa kwa miaka mingi kwa ajili ya chakula, nishati, dawa, na mambo ya kidini.” Leo, “bado mafuta ya zeituni hayana kifani yakilinganishwa na mafuta mengine,” anaendelea kusema mwanahistoria huyo. Kwa maelfu ya miaka, njia rahisi ya kutokeza mafuta ya zeituni haijabadilika. Kwanza, wavunaji hupiga matawi ya mizeituni kwa fimbo ili kuangusha zeituni ambazo hukusanywa. Kisha, zeituni kutia ndani mbegu zake zinapondwa katika kinu. Halafu, takataka zinaondolewa. Mwishowe, umajimaji huo hutiwa ndani ya tangi ili mafuta yatenganishwe na maji na kuwa tayari kutumiwa. *

Hata hivyo, tofauti na dhahabu, kama tu divai kuna aina nyingi za mafuta ya zeituni. Ulimwenguni pote, kuna mizeituni bilioni moja. * Wataalamu wameainisha zaidi ya aina 680 ya mizeituni. Licha ya kwamba kuna aina tofauti za miti, mambo kama vile aina ya udongo, hali ya hewa, wakati wa kuvunwa (unaoanzia mwezi wa 11 hadi Februari), na mbinu ya kutokeza mafuta yanaathiri ubora wa ladha, rangi, na harufu. Vikundi vya waonjaji wanaorodhesha ladha ya mafuta kuwa tamu, kali, ladha ya matunda, au nzuri. Waonjaji huhakikisha kwamba ubora wa mafuta unadumishwa.

Hali ya hewa ya Mediterania inafaa kwa ajili ya kukuzwa kwa mizeituni, na hivyo asilimia 95 hivi ya mafuta ya zeituni ulimwenguni hutokezwa kwenye maeneo yanayozunguka Mediterania. Wasafiri watapata mashamba ya mizeituni huko Hispania, Italia, Morocco, Siria, Tunisia, Ugiriki, Ureno, na Uturuki. Kwa kweli, mafuta ya zeituni yametajwa kuwa “dhahabu ya Mediterania.”

Kiungo Chenye Afya Katika Vyakula vya Mediterania

Kwa karne nyingi, vyakula vingi vya Mediterania vinaongezwa ladha kwa mafuta ya zeituni. Mafuta hayo yanaweza kutumiwa kukaanga, kutia marinadi, au kukoleza vyakula. José García Marín ambaye ni mpishi stadi anasema hivi akieleza umuhimu wa mafuta ya zeituni katika upishi wa Kihispania: “Kitu ambacho kimetumiwa katika upishi kwa miaka 4,000 lazima kiwe ni kizuri.” Kisha anaongeza: “Ubora wa mafuta hayo matamu umeboreshwa katika miaka ya karibuni, hasa kwa sababu ya mbinu mufti za kutokeza mafuta.”

Kwa muda mrefu, watafiti wameona kwamba watu wanaokula chakula cha kienyeji cha Mediterania wana afya nzuri. *  Hivi karibuni, wataalamu wa chakula walipanga Kongamano la Manufaa ya Kiafya ya Mafuta ya Zeituni. Walikata kauli kwamba vyakula vya Mediterania, kutia ndani mafuta ya zeituni, huchangia afya bora na maisha marefu. Kula chakula kilicho na mafuta ya zeituni kunaweza kupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo na kansa. “Katika nchi zote ambako watu hula vyakula vya kienyeji vya Mediterania . . . ambavyo hasa hupikwa kwa mafuta ya zeituni kuna watu wachache wenye ugonjwa wa kansa ikilinganishwa na nchi za Ulaya Kaskazini.”

Kunaweza kuwa na sababu nyingi zinazofanya mafuta hayo yafae kwa afya. Sababu moja ni kwamba mafuta ya zeituni yana kiasi kikubwa (kufikia asilimia 80) cha asidi ya oleic ambayo husaidia mfumo wa kuzungusha damu ufanye kazi vizuri. Isitoshe, kwa sababu kemikali na vikolezo havitumiwi inamaanisha kwamba mafuta ya zeituni yana vitamini, mafuta yasiyoganda, na viungo vingine vya asili vya zeituni mbivu.

Mafuta ya zeituni pia hutunza na kulainisha ngozi kwa sababu yana vitu vinavyoweza kuzuia chembe za mwili zisiharibike, kama vile vitamini  E na kemikali fulani zinazotokeza harufu nzuri (polyphenols). Hivyo, yanatumika kwa ukawaida kutengeneza vipodozi, losheni, sabuni za nywele, na sabuni nyingine. Wagiriki na Waroma wa kale walitumia mafuta ya zeituni yaliyokolezwa kwa miti-shamba ili kusafisha na kulainisha ngozi. Baadaye, katika karne ya sita, wasanii Wafaransa walianza kutengeneza sabuni kutokana na mafuta ya zeituni, wakichanganya mafuta hayo na majivu ya mimea ya baharini.

Mafuta ya Zeituni Katika Nyakati za Biblia

Katika nyakati za Biblia mafuta ya zeituni yalitumiwa sana kama chakula, vipodozi, nishati, dawa, na pia kwa makusudi mengine. Biblia inataja mafuta ya zeituni mara zaidi ya 250, ama ikirejelea mafuta yenyewe ama kitu cha kuchanganywa na mafuta yenye manukato.

Maandiko huonyesha wazi jinsi mafuta ya zeituni yalivyokuwa muhimu katika maisha ya familia za Waisraeli. Yalikuwa sehemu muhimu ya chakula chao na kuwa na mafuta mengi ilikuwa ishara ya ufanisi. (Yoeli 2:24) Wanaume na wanawake walijipaka mafuta ya zeituni. Kabla ya kukutana na Boazi, Ruthu ‘alijipaka mafuta.’ (Ruthu 3:3) Baada ya siku saba za kufunga, Mfalme Daudi ‘alisimama kutoka chini, akaoga, akajipaka mafuta, akabadili nguo zake za kujitanda, naye akaja nyumbani kwa Yehova.’—2 Samweli 12:20.

Taa za zamani zilitumia mafuta ya zeituni. (Mathayo 25:1-12) “Mafuta safi ya zeituni zilizopondwa” yalitumiwa katika taa zilizoangaza maskani huko jangwani. (Mambo ya Walawi 24:2) Kufikia wakati wa Mfalme Sulemani, mafuta ya zeituni yalikuwa bidhaa muhimu katika biashara ya kimataifa. (1 Wafalme 5:10, 11) Manabii waliwatia mafuta wafalme. (1 Samweli 10:1) Kwa fadhili, wakaribishaji waliwaonyesha wageni wao ukarimu kwa kupaka vichwa vyao mafuta. (Luka 7:44-46) Msamaria aliyetajwa katika mfano wa Yesu aliyaganga majeraha ya mwanamume aliyeumia kwa mafuta na divai.—Luka 10:33, 34.

Kwa sababu yalitumiwa sana katika matibabu, katika Maandiko mafuta yanalinganishwa na faraja au mashauri yenye kuliwaza. Mwanafunzi Mkristo Yakobo aliandika hivi: “Je, kuna yeyote mgonjwa kati yenu? Na awaite kwake wanaume wazee wa kutaniko, nao wasali juu yake, wakimpaka mafuta katika jina la Yehova. Na sala ya imani itamponya huyo asiyejisikia vizuri, na Yehova atamwinua.”—Yakobo 5:14, 15.

Mizeituni huendelea kutokeza matunda kwa muda mrefu sana. Mzeituni mmoja unaweza kutokeza lita tatu hadi nne za mafuta kila mwaka kwa karne nyingi! Hapana shaka: Umajimaji huu wenye rangi ya dhahabu unaweza kuboresha afya, kulainisha ngozi, na kufanya chakula kipendeze zaidi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Mafuta ya zeituni yanayoitwa extra-virgin na virgin yametolewa moja kwa moja kutoka kwa zeituni na hayajachanganywa na chochote. Mafuta yanayoitwa refined, au common, na olive-pomace yamechanganywa na kemikali ili kupunguza ladha kali.

^ fu. 8 Kila mwaka mizeituni hiyo inatokeza lita bilioni 1.7 hivi za mafuta.

^ fu. 12 Pia matunda na mboga ni sehemu ya chakula hicho.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]

Unachopaswa Kujua Kuhusu Mafuta ya Zeituni

▪ Manufaa yake ya kiafya hudumu kwa miezi 18.

▪ Mwangaza huharibu mafuta hayo, hivyo yanapaswa kuhifadhiwa katika mahali baridi pasipo na mwangaza.

▪ Mafuta ya zeituni hupoteza nguvu zake za kuzuia kuharibika kwa chembe yakitumiwa zaidi ya mara moja kukaanga chakula.

▪ Wataalamu wa chakula wanapendekeza kwamba ili wapate manufaa kamili ya afya kutokana na mafuta ya zeituni, watu wanapaswa kuyatumia katika maisha yao yote.

▪ Manufaa ya kiafya ya mafuta ya zeituni yanaongezeka yanapotumiwa katika vyakula vya kienyeji vya Mediterania, ambavyo vina samaki, mboga, maharagwe, na matunda.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Njia za Zamani za Kutokeza Mafuta ya Zeituni

Wafanyakazi wanapiga-piga matawi ili kuvuna zeituni

Mawe ya kusagia yanaponda zeituni

Mashini hii inatenganisha mafuta na takataka

Mafuta ya zeituni yakitoka kwenye mashini

[Picha zimeandaliwa na

Millstones and machine: Museo del Olivar y el Aceite de Baena

[Picha katika ukurasa wa 18]

Juu: Mashamba ya mizeituni ya karne nyingi

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kulia: Taa ya zamani iliyotumia mafuta ya zeituni

[Hisani]

Lamp: Museo del Olivar y el Aceite de Baena

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kulia kabisa: Mfano wa mabikira kumi na taa zao za mafuta