Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Usiku Ulipoingia Mchana”

“Usiku Ulipoingia Mchana”

 “Usiku Ulipoingia Mchana”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BENIN

“SALAALA! Mamilioni Washangazwa na Kupatwa kwa Jua.” Hicho kilikuwa kichwa kikuu cha gazeti la Ghana Daily Graphic siku moja baada ya kupatwa kwa jua Machi 29, 2006 (29/3/2006). Wakati wa kupatwa kwa jua kulikoonekana mara ya kwanza upande wa mashariki wa Brazili, kivuli cha mwezi kilifunika Bahari ya Atlantiki kwa mwendo wa kilomita 1,600 kwa saa na kufika kwenye nchi za pwani za Ghana, Togo, na Benin kuanzia saa mbili hivi asubuhi. Watu wa Afrika Magharibi wangetarijia nini?

Jua lilipatwa mara ya mwisho nchini Ghana mnamo 1947. Theodore ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 27, anakumbuka: “Wakati huo watu wengi hawakuwa wamewahi kuona jua likipatwa kwa hiyo hawakuelewa ni nini kinatendeka. Kwa sababu hiyo, watu walifafanua tukio hilo kuwa ‘wakati usiku ulipoingia mchana.’”

Kampeni za Kuwaelimisha Watu

Serikali ilianzisha kampeni za kuwaonya watu kuhusu hatari za kuangalia jua linapopatwa. Mabango yenye kuvutia huko Togo yalionya: “Linda macho yako! Unaweza kupoteza uwezo wa kuona!”

Maofisa wa serikali walitoa mapendekezo mawili. Kwanza, kaa ndani ya jengo na utazame tukio hilo katika televisheni. Pili, ukiwa nje vaa miwani maalumu. Mamilioni ya watu walikodolea macho televisheni na kompyuta ili waone picha hizo zenye kustaajabisha. Hata hivyo, vifaa hivyo havingeweza kuonyesha msisimko uliokuwepo kabla tu na wakati wa tukio hilo. Acheni tuwazie jinsi hali ilivyokuwa.

Watu Wangojea kwa Hamu

Siku hiyo ilionekana kama siku ya kawaida tu huko Afrika Magharibi kwani kulikuwa na jua na hakukuwa na mawingu. Je, kweli jua lingepatwa? Muda ulipozidi kuyoyoma, watu waliokuwa nje wakitazama tukio hilo walivaa miwani yao na kutazama juu. Nao wengine walipiga simu za mkononi wakiwauliza marafiki wao ikiwa wanaona kitu chochote.

Zaidi ya kilomita 350,000 juu, mwezi ambao haukuwa unaonekana, ulikuwa ukisonga kuelekea jua. Ghafula ulionekana kama kitu cheusi kinachong’aa na ukaanza kufunika jua. Kulikuwa na msisimko mkubwa watu walipoanza kuuona.

Kwa saa moja hivi, watu hawakuona mabadiliko yoyote kwenye mazingira yao. Hata hivyo, kadiri mwezi ulivyozidi kufunika jua, kukawa na mabadiliko angani. Anga la  bluu lilianza kutoweka. Kukawa baridi. Taa ambazo huwaka kukiwa na giza, ziliwaka giza lilipoanza kuingia asubuhi. Watu waliingia kwenye majengo. Maduka yalifungwa. Ndege waliacha kuimba, na wanyama walianza kujitayarisha kulala. Giza liliingia polepole. Kisha kukawa giza tititi, na kimya kikatawala.

Giza Lisiloweza Kusahaulika

Nyota zikaanza kutokea. Sehemu za nje tu za jua ndizo zilionekana kuzunguka mwezi mweusi kama pete inayong’aa. Nuru inayoitwa Shanga za Baily * ilimetameta kandokando ya mwezi, na jua lilionekana kama pete yenye almasi lilipokuwa likipita mabonde yaliyo juu ya mwezi. Sehemu ya ndani ya jua ilimetameta kwa rangi ya waridi. Mtazamaji mmoja alisema: “Hiyo ndiyo mandhari yenye kuvutia zaidi ambayo nimewahi kuona, ilikuwa maridadi wee!”

Giza hilo tititi liliendelea kwa dakika tatu hivi. Kisha jua likaanza kujitokeza tena. Watazamaji walishangilia sana. Anga likawa jangavu tena, na nyota zikatokomea. Hali ikarudi jinsi ilivyokuwa.

Mwezi ni “shahidi mwaminifu angani.” Kwa hiyo, kupatwa kwa jua ni jambo linaloweza kujulikana karne nyingi mapema. (Zaburi 89:37) Watu wa Afrika Magharibi walihitaji kungoja miaka 60 kabla ya kuona tukio hilo. Wanatarajia kuona tena kupatwa kwa jua mnamo 2081. Huenda utapata nafasi ya kuona kupatwa kwa jua katika eneo lenu hivi karibuni.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Jina hilo lilitokana na mwastronomia Francis Baily, ambaye aliandika kuhusu shanga hizo wakati wa kupatwa kwa jua mwaka wa 1836.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 29]

Je, Jua Lilipatwa Yesu Alipokufa?

Marko 15:33 inasema: “Ilipofika saa sita kukawa na giza juu ya nchi yote mpaka saa tisa.” Giza hilo la saa tatu, kuanzia saa sita mpaka saa tisa mchana, lilikuwa la kimuujiza. Halikuwa limesababishwa na kupatwa kwa jua. Kwanza, muda mrefu zaidi ambao jua linaweza kupatwa mahali popote duniani ni kwa dakika saba na nusu tu. Pili, Yesu alikufa siku ya 14 ya mwezi wa Nisani. Siku ya kwanza ya Nisani huamuliwa kwa kuonekana kwa mwezi mpya. Wakati huo mwezi huwa katikati ya dunia na jua na hivyo linaweza kupatwa. Kufikia siku ya 14 ya Nisani, tayari mwezi huwa umemaliza nusu ya mzunguko wake. Wakati huo dunia huwa kati ya jua na mwezi, na hivyo badala ya kufunika jua, mwezi unarudisha mwangaza wa jua kikamili. Kwa hiyo kunakuwa na mwezi mpevu, na huo ni wakati unaofaa kuadhimisha Ukumbusho wa kifo cha Yesu.

[Picha]

Nisani 14 huwa karibu au wakati wa mwezi mpevu

[Picha/Ramani katika ukurasa wa 28, 29]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sehemu ambazo zilipatwa na jua

⇧ AFRIKA

BENIN ●

TOGO ●

GHANA ●

[Hisani]

Map: Based on NASA/Visible Earth imagery

[Picha katika ukurasa wa 28]

Kupatwa kwa jua kulikoonekana Machi 29, 2006

[Picha katika ukurasa wa 28]

Miwani maalumu iliwaruhusu watazamaji kuona kupatwa kwa jua