Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Kinaitwa Kisiwa Kikubwa

Kwa Nini Kinaitwa Kisiwa Kikubwa

 Kwa Nini Kinaitwa Kisiwa Kikubwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HAWAII

WATU wanaposikia kuhusu Visiwa vya Hawaii, wao hufikiria nini? Huenda wakafikiria fuo zenye mchanga mweupe, maji safi, minazi, na usiku wenye joto kwenye veranda zisizo na paa kukiwa na mwangaza wa mienge midogo. Mbali na hayo, kuna vyakula vya Hawaii kama vile mananasi, mlo unaotengenezwa kutoka kwa jimbi, salmoni wabichi waliochanganywa na saladi, na nguruwe wa kalua. Ni mahali penye kupendeza sana!

Kuna mambo mengi zaidi ya kupendeza katika kisiwa cha Hawaii. Kwanza, kisiwa hicho kinaitwa Kisiwa Kikubwa kwani visiwa vingine vinavyozunguka vya Hawaii, yaani, Oahu, Maui, na Kauai vinaweza kutoshea ndani yake. Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita 10,432 za mraba na bado kinazidi kuwa kikubwa. Lakini tutazungumzia hilo baadaye.

Eneo na Hali ya Hewa

Kwa kuwa kiko upande wa kusini zaidi, Kisiwa Kikubwa kina hali nzuri ya hewa. Kwa kawaida joto la mchana katika maeneo ya pwani hufikia wastani wa zaidi ya nyuzi 26 Selsiasi katika majira ya kiangazi (Mwezi wa 5 hadi Oktoba) na zaidi ya nyuzi 21 Selsiasi katika majira ya baridi kali (Novemba hadi Aprili) na nyakati za usiku ni kawaida kuwa na kiwango cha joto kati ya nyuzi 15 hadi 18 Selsiasi. Kwa kawaida, wilaya ya Kona, iliyo upande usio na upepo wa kisiwa hicho ina jua zaidi, na eneo la Hilo, lililo upande wenye upepo huwa na mvua nyingi.

Hali ya hewa ya kitropiki na udongo wa volkano wenye rutuba hufanya eneo hilo liwe na matunda na mboga kwa wingi. Kuna matunda mengi matamu kama vile maembe, mapapai, lichi, na matunda mengine, na pia kuna okidi maridadi na maua ya aina ya anthurium. Miti ya makadamia na kahawa hukua kwa wingi. Kahawa ya Kona inajulikana ulimwenguni pote. Kila mwaka, wauzaji wa kahawa kutoka sehemu mbalimbali huenda kwenye Maonyesho ya Kahawa ya Kona ili kuonja na kununua kahawa hiyo.

Kisiwa Kikubwa kina maeneo yenye hali mbalimbali za hewa, kutia ndani msitu wa mvua, jangwa, na nyika. Misitu ya mvua iko upande wa mashariki wenye mvua wa kisiwa hicho. Ndege wengi wa pekee huishi huko, na vilevile kuna mikangaga na aina kadhaa za okidi za msituni. Wilaya ya Kona-Kohala inapata wastani wa sentimita 25 hivi za mvua kila mwaka, na eneo la Hilo linapata zaidi ya sentimita 250 kwa wastani kila mwaka.

 Kilauea—Volkano Hai Yenye Manufaa

Kisiwa hicho kina volkano tano: Mauna Loa, Mauna Kea, Kilauea, Kohala, na Hualalai. Kilauea inamaanisha “Kumwagika Sana.” Mnamo 1979, Mlima Kilauea ulilipuka. Tangu 1983, mlima huo umekuwa ukimwaga lava bila kukoma. Lava hiyo imeangamiza miji mitatu lakini imetokeza ekari nyingi za nchi mpya.

Lava inapofika baharini kwa kelele nyingi, inatokeza mvuke na moshi mwingi na pia mawingu na fuo zenye mchanga mweusi. Watu wanaweza kutazama Mlima Kilauea wakiwa karibu sana bila kuogopa.

Mauna Kea, volkano isiyotenda yenye urefu wa mita 4,205, ndio mlima mrefu zaidi katika kisiwa hicho kwani umeuzidi kidogo Mauna Loa ambao una urefu wa mita 4,169. Hata hivyo, Mauna Kea unapopimwa kutoka kwenye sakafu ya bahari una urefu wa mita 9,000, na hivyo kuufanya kuwa mlima mrefu zaidi ulimwenguni. Kwa upande mwingine, Mauna Loa ndio mlima mkubwa zaidi ulimwenguni kwani unatoshea kwenye eneo lenye kilomita 40,000 hivi za mchemraba.

Mambo Yanayovutia Watalii

Wakati wa majira ya baridi kali, theluji humwagika juu ya Mauna Kea ambapo jina lake la utani Mlima Mweupe lilitoka. Wenyeji huteleza kwenye theluji hiyo, ingawa ni hatari kufanya hivyo kwa sababu ya miamba iliyo kwenye mlima huo. Kwa sasa, darubini 13 zenye nguvu zaidi ulimwenguni, za nchi 11 hivi zimewekwa kwenye kilele katika Hifadhi ya Kisayansi ya Mauna Kea.

Kwenye maeneo ya pwani ya Kisiwa Kikubwa, kuna mambo mengi ambayo mtu anaweza kufanya ili kujifurahisha. Michezo ya majini inaweza kufurahiwa mwaka mzima kwa sababu bahari huwa na joto la kiasi nyakati zote. Kuna fuo zenye mchanga mweupe zinazopendwa sana za hoteli na pia za watu binafsi, ambazo zinaweza kufikiwa tu na watu wanaotembea au kwa magari yenye nguvu.

Mambo mengi ya Kisiwa Kikubwa yanapendeza sana kama vileukubwa, mahali kilipo, hali ya hewa, na vitu vyake vya asili. Utaona kwamba watu huko ni wachangamfu, wenye urafiki, na wenye kujali, nao hufurahia kuonyesha ukarimu wa Hawaii.

[Picha katika ukurasa wa 16]

 

NIHAU

KAUAI

OAHU

HONOLULU

MOLOKAI

MAUI

LANAI

KAHOOLAWE

HAWAII

Hilo

Kohala

Mauna Kea

Hualalai

Mauna Loa

Kilauea

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mlima Mauna Kea ukiwa nyuma

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

U.S. Geological Survey/ Photo by T.J. Takahashi ▸