Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uhalifu Umetushinda?

Uhalifu Umetushinda?

 Uhalifu Umetushinda?

▪ Mwanafunzi mwenye kichaa aliye na silaha kali anawaua wanafunzi na walimu shuleni kwao.

▪ Msichana mdogo anatekwa nayra na wazazi wake wanahuzunika sana.

▪ Kijana akiri kumuua mtu ili apate msisimko na akiri kwamba aliwaonyesha rafiki zake maiti hiyo, nao hawakumwambia mtu yeyote kwa majuma kadhaa.

▪ Akitumia intaneti, mtu anayevizia watoto ili afanye nao ngono anabadilishana maoni na watu wengine wanaowavizia watoto kuhusu mbinu za kuwashawishi watoto.

HIVYO ni baadhi ya visa vya uhalifu vyenye kushtua ambavyo huripotiwa na vyombo vya habari siku hizi. Je, unahisi ukiwa salama nyumbani kwako, hasa nyakati za usiku? Je, wewe au familia yako mmeathiriwa na uhalifu? Mamilioni ya watu ulimwenguni pote, hata katika nchi ambazo zilionekana kuwa zina usalama, wanakiri kwamba wanaogopa uhalifu na jeuri. Fikiria ripoti zifuatazo kutoka nchi mbalimbali.

JAPANI: Gazeti Asia Times linaripoti: “Wakati mmoja Japani ilikuwa moja kati ya nchi salama zaidi ulimwenguni . . . Hata hivyo, sasa hali hiyo ya usalama iliyofurahiwa zamani imepotea, na badala yake kuna wasiwasi mkubwa kuhusu uhalifu na ugaidi wa ulimwenguni pote.”

AMERIKA YA LATINI: Ripoti moja ya 2006 inasema kwamba watu mashuhuri nchini Brazili wanatabiri kwamba kutakuwa na mapigano ya waasi dhidi ya serikali huko São Paulo. Kwa sababu ya mapigano ya hapa na pale yaliyoendelea kwa majuma kadhaa, rais wa nchi hiyo alituma wanajeshi kwenye mitaa ya jiji hilo. Ripoti moja katika gazeti Tiempos del Mundo kuhusu Amerika ya Kati na Mexico inasema kwamba “kuwepo kwa angalau washiriki 50,000 wa magenge ya vijana kumefanya wenye mamlaka wa eneo hilo wakae chonjo.” Gazeti hilo linaendelea kusema kwamba “katika mwaka wa 2005 peke yake, watu 15,000 hivi waliuawa na magenge ya vijana huko El Salvador, Honduras, na Guatemala.”

KANADA: Mnamo 2006 gazeti USA Today lilisema hivi: “Wataalamu wa masuala ya uhalifu wanasema kwamba magenge yameongezeka.” Gazeti hilo linaendelea kusema, “Polisi . . . waligundua kwamba kuna magenge 73 ya wahalifu huko Toronto.” Kulingana na gazeti hilo, mkuu wa polisi huko Toronto alikiri kwamba hakuna suluhisho la haraka kwa tatizo la magenge yanayozidi kuongezeka mitaani.

AFRIKA KUSINI: Patrick Burton, mtafiti wa masuala ya uhalifu, alisema hivi katika gazeti Financial Mail: “Vijana nchini Afrika Kusini wanaogopa sana uhalifu.” Uhalifu huo unatia ndani “uhalifu wenye jeuri kama vile wizi wa kutumia silaha, kuteka nyara na wizi wa mabenki,” linasema gazeti hilo.

UFARANSA: Kila siku watu wengi mitaani hushikwa na woga “wanapopanda ngazi ambazo zimeharibiwa, wanapoingia kwenye maegesho ya magari ambayo sasa yamekuwa maeneo hatari, na wanapotumia usafiri wa umma ambao ni hatari giza linapoingia.”—Guardian Weekly.

 MAREKANI: Vikundi vya magenge vinachangia ongezeko la uhalifu. Kulingana na ripoti moja katika gazeti The New York Times, katika jimbo moja, uchunguzi wa polisi ulionyesha kwamba karibu vijana 17,000, wa kike na wa kiume, ni washiriki wa moja ya magenge 700 hivi. Hilo ni ongezeko la washiriki 10,000 hivi katika miaka minne tu.

UINGEREZA: Kulingana na ripoti moja ya UNICEF kuhusu jinsi watoto wanavyoathiriwa na uhalifu, gazeti The Times la London lilisema hivi: “Idadi inayozidi kuongezeka ya vijana Waingereza wanauawa kwa kupigwa risasi. . . . Wastani wa umri wa vijana wanaouawa na wale wanaofanya uhalifu huo, unazidi kupungua.” Idadi ya wafungwa nchini Uingereza na Wales imeongezeka sana kufikia karibu 80,000.

KENYA: Mama na binti yake ambao hawakutoka kwenye gari lao haraka walipigwa risasi na majambazi kwenye barabara moja kuu, linasema gazeti moja. Kumekuwa na uhalifu mwingi sana kama vile magari kutekwa nyara, kuporwa barabarani na kuvamiwa nyumbani katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Je, kuna njia ya kukomesha ongezeko hilo la uhalifu? Ni nini kiini hasa cha uhalifu? Je, tuna sababu ya kuwa na tumaini kwamba siku moja watu wataishi kwa amani na usalama wa kweli? Makala zinazofuata zitajibu maswali hayo.