Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Gabon—Hifadhi ya Wanyama-Pori

Gabon—Hifadhi ya Wanyama-Pori

Gabon—Hifadhi ya Wanyama-Pori

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI GABON

JE, UNAWEZA kuwazia ufuo wa kitropiki ambako tembo hulisha, viboko huogelea, na nyangumi na pomboo hukusanyika? Kwenye pwani za Afrika, kuna fuo zenye urefu wa kilomita 100 ambako unaweza kufurahia mandhari kama hizo.

Ili watu waendelee kufurahia mandhari kama hizo, ni wazi kwamba pwani hiyo ya pekee inahitaji kuhifadhiwa. Kwa kupendeza, uhitaji wa kuhifadhi mandhari hizo ulizungumziwa Septemba 4, 2002, rais wa Gabon aliposema kwamba asilimia 10 ya Gabon, kutia ndani maeneo fulani ya pwani, yangetengwa kuwa mbuga za taifa.

Mbuga hizo zenye ukubwa wa kilomita 30,000 za mraba, ukubwa unaokaribia kulingana na nchi ya Rwanda, zina mambo mengi yenye kupendeza. “Gabon inaweza kuwa mahali ambapo watu kutoka maeneo yote ya dunia wanakuja kuona maajabu ya asili ya dunia yaliyosalia,” akasema Rais Omar Bongo Ondimba.

Ni nini kinachofanya hifadhi hizo ziwe muhimu sana? Bado asilimia 85 hivi ya Gabon ni msitu, na asilimia 20 hivi ya jamii za mimea katika misitu hiyo hazipatikani sehemu nyingine yoyote ulimwenguni. Isitoshe, misitu ya ikweta ni makao ya sokwe wa aina mbalimbali, tembo, na wanyama wengine wanaokabili hatari ya kutoweka. Mbuga zilizoanzishwa hivi karibuni zitafanya Gabon isaidie sana kutunza unamna-namna wa viumbe wa Afrika.

Loango —Ufuo Usio na Kifani

Huenda Mbuga ya Taifa ya Loango ni kati ya hifadhi za wanyama zenye kupendeza zaidi barani Afrika. Mbuga hiyo ina fuo kubwa zilizo karibu na nyangwa za maji baridi na misitu mikubwa. Lakini jambo ambalo hufanya fuo za Loango ziwe za pekee ni wanyama wanaotembea huko, yaani, viboko, tembo, nyati, chui, na sokwe.

Kwa nini ufuo huo huvutia wanyama wa msituni? Kando ya fuo zenye mchanga mweupe za Loango, kuna maeneo ambayo viboko na nyati hupenda kulisha. Aina fulani ya mitende ambayo hukua kando ya fuo, huzaa matunda mengi ambayo huwavutia tembo kama tu vile peremende inavyowavutia watoto. Lakini jambo linalowavutia sana ni kwamba eneo hilo ni tulivu. Hakuna wanadamu wanaoishi huko.

Kwa kuwa watu hawatembelei eneo hilo mara nyingi, kasa wenye ngozi laini mgongoni hupenda kutaga mayai yao kwenye fuo hizo tulivu. Pia, ndege aina ya mtilili hupenda kujenga viota vyao huko nao huchimba viota hivyo mchangani mita chache kutoka mahali ambapo maji ya bahari hufika. Katika miezi ya kiangazi, nyangumi zaidi 1,000 wenye nundu huja kwenye maji matulivu ya Loango kuzaliana.

Nyangwa mbili kubwa hutenganisha fuo za Loango na misitu ya ikweta, nazo huandaa makao mazuri kwa ajili ya mamba na viboko. Nyangwa hizo zina samaki wengi sana na fuo zake zina misitu ya mikoko. Tai mla-samaki wa Afrika na furukombe wanapenda kutafuta chakula kwenye maji hayo, na jamii kadhaa za mdiria hupenda kutafuta samaki kwenye maji yasiyo na kina. Tembo, ambao hupenda maji, huogelea kwa furaha wakivuka nyangwa hizo ili wakale matunda wanayopenda.

Ndani ya misitu ya ikweta, tumbili hurukaruka kwenye matawi ya juu, nao vipepeo wenye rangi maridadi hurukaruka hapa na pale. Popo wala-matunda hukaa kwenye miti wanayopenda wakati wa mchana, na usiku wanafanya kazi yao muhimu ya kudondosha mbegu msituni. Kwenye kingo za msitu, chozi hula chavua kutoka kwenye miti na vichaka vinavyotoa maua. Haishangazi kwamba mbuga hiyo ya Loango imefafanuliwa kuwa “mahali unapoweza kufurahia mazingira ya ikweta ya Afrika.”

Lopé—Mahali Ambapo Sokwe Bado Wanapatikana kwa Wingi

Mbuga ya Taifa ya Lopé inatia ndani sehemu kubwa za msitu wa mvua ambao haujaharibiwa na wanadamu. Mbuga hiyo ina eneo kubwa la savana na msitu ulio kando ya maji upande wa kaskazini. Watu wanaopenda vitu vya asili ambao wanataka kuona sokwe au nyani wakubwa wa Afrika katika mazingira yao ya asili wanaweza kufurahia eneo hilo. Kuna sokwe kati ya 3,000 na 5,000 katika eneo lililohifadhiwa la kilomita 5,000 za mraba.

Augustin, aliyekuwa ofisa wa mbuga hiyo, anakumbuka jinsi alivyokutana na sokwe mnamo 2002. “Nilipokuwa nikitembea msituni, nilikutana na familia ya sokwe wanne,” anasema. “Sokwe mkubwa wa kiume mwenye miaka 35 hivi, aliye na manyoya meupe mgongoni, alisimama mbele yangu. Uzito wake ulikuwa karibu mara tatu ya uzito wangu. Nilifuata mapendekezo ambayo hutolewa unapokutana na sokwe, yaani, kuketi chini mara moja, kuinamisha kichwa, na kuangalia chini kuonyesha kuwa nimejitiisha. Sokwe huyo alikuja, akaketi kando yangu na kuweka mkono juu ya bega langu. Kisha akachukua mkono wangu, akaukunjua, na kuchunguza kiganja changu. Alipohakikisha kwamba nisingehatarisha familia yake, aliondoka. Siku hiyo ambayo sitawahi kuisahau, niligundua uzuri wa kukutana na wanyama katika mazingira yao ya asili. Ingawa watu huwaua sokwe kwa ajili ya nyama au kwa sababu ya maoni ya uwongo kwamba wao ni hatari, wao ni wanyama watulivu wanaohitaji kulindwa.”

Huko Lopé, nyani wakubwa hukusanyika katika vikundi vikubwa ambavyo nyakati nyingine huwa na nyani zaidi ya elfu moja. Hapo ndipo kuna wanyama wengi zaidi wa jamii ya nyani ulimwenguni, nao hupiga kelele nyingi sana. Mgeni kutoka Kamerun anaeleza kuhusu wakati alikutana na kikundi kimoja kikubwa.

“Mtu aliyekuwa akituongoza alitambua kuwa nyani hao wanakuja kwa sababu ya vifaa fulani ambavyo baadhi yao wamevishwa. Tulisonga mbele ya nyani hao, tukajificha, na kuwangoja. Kwa dakika 20 tulisikiliza muziki wa msitu uliotolewa na ndege na wadudu. Utulivu huo ulikatishwa ghafula nyani hao walipokaribia. Kelele za matawi yakivunjika na sauti zao za juu zilinifanya nifikiri dhoruba kali inakaribia. Lakini nilipoona [nyani waliokuwa wakioongoza], walionekana kama kikosi cha kwanza cha askari-jeshi wanaoongoza uvamizi. Nyani wakubwa wa kiume waliongoza, wakitembea haraka, nao nyani wa kike na vijana waliruka kutoka tawi moja hadi lingine. Ghafula, nyani mmoja wa kiume akasimama na kuangalia huku na huku kama anashuku jambo fulani. Nyani mdogo, aliyekuwa juu ya mti, alikuwa ametuona na kutoa onyo. Kikundi chote kikaongeza mwendo, na kelele zikaongezeka walipotoa sauti za kukasirishwa. Baada ya dakika chache, wote waliondoka. Aliyekuwa akituongoza alikadiria kuwa kikundi hicho kilichotupita kilikuwa na nyani 400 hivi.”

Sokwe wana kelele nyingi kama nyani hao na hawaonekani kwa urahisi kwa kuwa wao husonga haraka sana wakitafuta chakula. Kwa upande mwingine, wageni huona tumbili wenye pua zenye rangi ya kijivu ambao mara kwa mara huonekana kwa wingi kwenye maeneo ya savana yaliyo kando ya msitu. Tumbili mwenye mkia wa rangi nyangavu aliyegunduliwa miaka 20 hivi iliyopita, ndiye anayeonekana mara chache sana huko Lopé.

Ndege wakubwa wenye rangi maridadi—kama vile shorobo na hondohondo—hutoa sauti kubwa. Jamii 400 hivi za ndege zimeonekana katika mbuga hiyo, na hivyo kufanya eneo hilo liwavutie watu wanaopenda kutazama ndege.

Mahali Penye Unamna-namna wa Viumbe

Loango na Lopé ni mbuga mbili tu kati ya mbuga 13 za taifa za Gabon. Katika mbuga nyingine kuna misitu ya mikoko, maua ya pekee, na maeneo ambayo ndege huhamia. “Gabon imetenga maeneo bora ya mazingira katika nchi yote,” anaeleza Lee White wa Shirika la Kuhifadhi Wanyama-pori. “Si ukubwa tu wa maeneo hayo unaovutia, bali pia uzuri wake. Mnamo 2002, mfumo mzuri sana wa mbuga za taifa uliundwa katika muda mfupi, nao unatia ndani unamnanamna wa viumbe na mimea nchini.”

Bila shaka, kama vile Rais Bongo Ondimba anavyosema bado kuna vikwazo vingi. “Tunazungumza kuhusu kazi ya ulimwenguni pote,” anasema, “ambayo itatia ndani kujidhabihu kwa muda mrefu, ili kutuwezesha kutimiza lengo letu la kuhifadhi maajabu ya vitu vya asili kwa ajili ya vizazi vinavyokuja.”

[Ramani katika ukurasa wa 17]

 

AFRIKA

GABON

Mbuga 13 za taifa za Gabon

Mbuga ya Taifa ya Lopé

Mbuga ya Taifa ya Loango

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Nyangumi mwenye nundu na picha ya Loango iliyopigwa kutoka angani

[Hisani]

Whale: Wildlife Conservation Society

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Nyani mkubwa (kushoto) na sokwe (kulia)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Robert J. Ross