Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Bahari Isiyo na Kifani—Lakini Imekufa!

Bahari Isiyo na Kifani—Lakini Imekufa!

 Bahari Isiyo na Kifani—Lakini Imekufa!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ISRAELI

BAHARI hiyo ndiyo yenye chumvi nyingi zaidi, ipo chini zaidi ya usawa wa bahari, haina uhai, na watu wengine wanasema ina maji mazuri zaidi kwa afya duniani. Kwa karne nyingi imeitwa Bahari Inayonuka, Bahari ya Ibilisi, na Ziwa la Lami. Biblia inaiita Bahari ya Chumvi na bahari ya Araba. (Mwanzo 14:3; Yoshua 3:16) Wasomi wengi hukubaliana na maoni kwamba magofu ya Sodoma na Gomora yapo chini ya maji yake. Kwa hiyo inajulikana pia kama Bahari ya Sodoma au Bahari ya Loti, ambaye anatajwa katika Biblia kuhusiana na majiji hayo.—2 Petro 2:6, 7.

Baadhi ya majina hayo hayaamshi hamu ya mtu kutembelea mahali hapo. Hata hivyo, kila mwaka maelfu ya watu wanatembelea bahari hiyo ya pekee ambayo leo inajulikana kama Bahari ya Chumvi. Kwa nini ina chumvi nyingi hivyo? Je, ni kweli kwamba bahari hiyo haina uhai wowote, na je, maji yake ni mazuri kwa afya?

Ipo Chini Zaidi ya Usawa wa Bahari na Ina Chumvi Zaidi

Bahari ya Chumvi inapatikana upande wa kaskazini wa Bonde la Ufa, kwenye ufa unaoelekea kusini kuingia Afrika Mashariki. Mto Yordani unasonga upande wa kaskazini hadi ufikie sehemu ya dunia iliyo chini zaidi—mita 418 hivi chini ya usawa wa bahari. Bahari hiyo imezungukwa na vilima vya Yudea upande wa magharibi na milima ya Moabu upande wa mashariki wa Jordan.

Lakini ni nini kinachofanya Bahari ya Chumvi iwe na chumvi nyingi hivyo? Madini mbalimbali hasa magnesi, sodiamu, na kalisi ya kloridi yanaingizwa kwenye Bahari ya Chumvi kutoka kwenye Mto Yordani na mito midogo, vijito, na chemchemi nyingine. Inakadiriwa kwamba Mto Yordani pekee unaingiza tani 850,000 za chumvi kila mwaka. Kwa sababu bahari hiyo iko chini ya usawa wa bahari, njia pekee ya maji kutoka katika bahari hiyo ni kupitia uvukizaji. Katika siku yenye joto, tani milioni saba za maji huvukizwa na hiyo ndiyo sababu maji ya ziwa hilo hayaongezeki. Ingawa maji huvukizwa, chumvi na madini hubaki. Na hilo limesababisha bahari hiyo kuwa yenye chumvi nyingi zaidi duniani, asilimia 30 hivi ya maji hayo yamejaa chumvi na hivyo kuifanya iwe yenye chumvi zaidi ya bahari nyingine.

Tangu zamani, watu wamestaajabia mambo ya pekee ya Bahari ya Chumvi. Mwanafalsafa Mgiriki Aristoto alisikia kwamba Bahari hiyo ilikuwa “chungu na yenye chumvi nyingi sana hivi kwamba hakuna samaki [anayeishi] ndani yake.” Kwa kuwa bahari hiyo ina chumvi nyingi sana, hilo hufanya isiwe rahisi kwa mtu kuzama na hivyo huwasaidia watu ambao hawajui kuogelea waelee. Mwanahistoria Myahudi Flavio Yosefo anaeleza kuhusu Jenerali Mroma Vespasiani ambaye alijaribu kuona ikiwa hilo ni kweli kwa kuwatupa wafungwa wa vita katika bahari hiyo.

 Huenda unajiuliza jinsi maji hayo yaliyokufa yanavyoweza kuwa mazuri kwa afya.

Je, Ni Bahari Yenye Maji Yanayofaa Zaidi?

Wasafiri katika Enzi za Kati walirudi makwao na hadithi kuhusu bahari ambayo haina ndege, samaki, na mimea. Hata ilifikiriwa kwamba mvuke unaonuka wa bahari hiyo ulikuwa hatari. Bila shaka, hilo liliendeleza wazo la kwamba bahari inayonuka imekufa. Ni kweli kwamba kwa sababu ya kiwango kikubwa cha chumvi, viumbe wachache kama vile bakteria, ndio wanaoweza kuishi katika maji yake, na samaki wowote wanaoletwa humo na maji ya mto hufa haraka.

Bahari hiyo haitegemezi uhai, lakini mambo yako tofauti katika eneo linalozunguka bahari hiyo. Licha ya sehemu kubwa ya eneo hilo kuwa kame, kuna chemchemi zenye maporomoko na mimea ya kitropiki. Eneo hilo pia linajulikana kwa sababu lina wanyama-pori wengi. Kuna jamii 24 za wanyama wanaonyonyesha ambao wanaishi karibu na bahari, kutia ndani paka fulani wanaoitwa sand cat, mbwa-mwitu wa Arabia, na mbuzi-mwitu wanaoonekana kwa wingi. Amfibia, reptilia, na samaki wanaishi kwenye maji baridi yanayopatikana kando ya bahari hiyo. Kwa kuwa Bahari ya Chumvi inapatikana karibu na mahali ambapo kwa kawaida ndege hupitia wanapohama, zaidi ya aina 90 za ndege wamepatikana  hapo, kama vile korongo mweusi na mweupe. Tai-mzoga mweupe na yule anayeitwa griffon pia wameonekana huko.

Lakini Bahari ya Chumvi inawezaje kuwa ndiyo yenye maji mazuri zaidi kwa afya? Inasemekana kwamba zamani watu walikunywa maji hayo wakifikiri yanaweza kuponya. Jambo hilo halipendekezwi hata kidogo leo! Wazo linalopatana na akili ni kwamba maji hayo ya chumvi yanaweza kusafisha mwili. Pia faida za kiafya za eneo hilo lote husifiwa sana. Kwa kuwa eneo hilo liko chini ya usawa wa bahari, kuna oksijeni nyingi sana. Inasemekana kwamba bromidi nyingi hewani humfanya mtu atulie, na matope meusi yenye madini mengi na chemchemi za maji moto yenye salfa kwenye fuo za bahari hiyo hutumiwa kutibu magonjwa kadhaa ya ngozi na matatizo fulani yanayohusiana na ugonjwa wa yabisi-kavu. Isitoshe, zeri, mti ambao hapo zamani ulikua katika eneo hilo, umethaminiwa sana kwa sababu unaweza kutumiwa kwenye vipodozi na dawa.

Lami Kutoka Baharini

Jambo linaloshangaza zaidi kuhusu Bahari ya Chumvi ni kwamba bahari hiyo hutokeza lami na mara kwa mara vipande vikubwa vya lami vimeonekana vikielea. Mnamo 1905, jarida The Biblical World liliripoti kwamba kipande kikubwa cha lami chenye uzito wa kilo 2,700 hivi kilisukumwa ufuoni katika mwaka wa 1834. Lami imefafanuliwa kuwa “bidhaa ya petroli ya kwanza kutumiwa na wanadamu.” (Saudi Aramco World, Novemba/Desemba 1984) Zamani watu fulani walifikiri kwamba matetemeko ya nchi yalisababisha vipande vikubwa vya lami vivunjike kutoka sehemu ya chini ya Bahari ya Chumvi na kuelea juu. Lakini sasa inadhaniwa kwamba lami hiyo hupenya kwenye mianya na kufika kwenye sakafu ya bahari ikiwa bado imeshikana na mawe ya chumvi. Kisha mawe hayo ya chumvi yanapoyeyuka, vipande vya lami huelea.

Kwa karne nyingi lami imetumiwa kwa njia mbalimbali kama vile kuzibia matundu kwenye mashua ili maji yasipenye, kwenye ujenzi, na hata kutengeneza dawa za kuzuia kuumwa na wadudu. Inafikiriwa kwamba katikati ya karne ya nne hivi K.W.K., Wamisri walianza kutumia sana lami katika kuhifadhi maiti, ingawa maoni hayo yanapingwa na wataalamu fulani. Wakati huo Wanabataea, jamii ya wahamaji wa zamani walioishi kwenye eneo la Bahari ya Chumvi, ndio waliokuwa wauzaji wakuu wa lami katika eneo hilo. Walileta lami hiyo ufuoni, wakaikata vipandevipande, na kuipeleka Misri.

Kwa kweli, Bahari ya Chumvi ni bahari isiyo na kifani. Hatutilii chumvi tunaposema kwamba bahari hiyo ndiyo yenye chumvi zaidi, ipo chini zaidi ya usawa wa bahari, haina uhai, na huenda ndiyo yenye maji mazuri zaidi kwa afya. Kwa kweli hiyo ndiyo bahari yenye kustaajabisha zaidi duniani!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

KUHIFADHIWA KATIKA MAJI YA CHUMVI

Wanahistoria wanaripoti kwamba Bahari ya Chumvi ilikuwa njia kuu ya biashara. Jambo hilo limethibitishwa na ugunduzi wa hivi karibuni wa nanga mbili za mbao.

Nanga hizo zilipatikana kwenye fuo za Bahari ya Chumvi, karibu na mahali ambako bandari ya zamani ya En-gedi ilikuwa. Nanga moja inafikiriwa kuwa ya miaka 2,500 hivi iliyopita, na hivyo kuifanya kuwa nanga ya zamani zaidi kuwahi kugunduliwa katika eneo la Bahari ya Chumvi. Ya pili inafikiriwa kuwa ya miaka 2,000 hivi iliyopita na inasemekana kuwa ilichongwa kwa kutumia teknolojia bora zaidi ya Roma wakati huo.

Kwa kawaida, nanga za mbao huoza katika maji ya kawaida ya bahari, na nanga za chuma huhifadhiwa. Hata hivyo, kwa kuwa maji ya Bahari ya Chumvi hayana oksijeni na yana chumvi nyingi, mbao na kamba zilizotumiwa kufungia nanga hizo zimebaki katika hali nzuri.

[Picha]

Nanga ya mbao ya kati ya karne ya 7 na ya 5 K.W.K.

[Hisani]

Photograph © Israel Museum, Courtesy of Israel Antiquities Authority

[Picha katika ukurasa wa 26]

Maporomoko ya maji moto

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mbuzi-mwitu dume

[Picha katika ukurasa wa 26]

Watu wanasoma gazeti huku wakielea