Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Vifaa vya Uharibifu” Vilitabiriwa

“Vifaa vya Uharibifu” Vilitabiriwa

“Vifaa vya Uharibifu” Vilitabiriwa

“Sikuzote mwanadamu aliye na akili iliyopotoka amejaribu kuvitumia vipawa vyake ili kuwatumikisha, kuwaangamiza, au kuwadanganya viumbe wengine.” —Horace Walpole, mwandishi Mwingereza wa karne ya 18.

UWEZO wa kutumia vyombo vya angani umewaletea wanadamu manufaa mengi. Lakini maneno yaliyoonyeshwa juu ya Horace Walpole yamethibitika kuwa ya kweli kama nini! Hata kabla ya wanadamu kupaa angani, watu walikuwa wakifikiria njia nyingi ambazo vyombo vya angani vinaweza kutumiwa kama vifaa vya vita.

Mnamo 1670, zaidi ya miaka 100 kabla ya puto la kwanza kurushwa angani, Mjesuti Mwitaliano Francesco Lana alionyesha uwezekano wa kwamba “Mungu hataruhusu mashine kama hiyo [ndege] iundwe, ili kusiwe na matatizo mengi yanayoweza kusababisha matatizo ya kijamii na ya kisiasa kati ya wanadamu.” Hata hivyo, akitabiri hali itakavyokuwa, aliongeza hivi: “Kwani ni nani [asiyeona] kwamba hakuna jiji lolote litakalokuwa salama kutokana na mashambulizi ya ghafula, yatakayosababishwa na ndege kutua wakati wowote kwenye soko na kuwashusha wavamizi? Jambo hilo lingetendeka katika nyua za nyumba za kibinafsi na kwenye meli baharini . . . Hata bila kushuka, ndege hizo zinaweza kuangusha vyuma ambavyo vitazamisha meli na kuua watu, na meli zinaweza kuteketezwa kwa vifaa vinavyolipuka na kutoa moto na mabomu.”

Maputo yenye hewa yenye joto na gesi ya hidrojeni yalipobuniwa mwishoni mwa karne ya 18, Walpole aliogopa kwamba maputo hayo yangekuwa “vifaa vya uharibifu kwa jamii ya wanadamu.” Kwa kweli, kufikia mwisho wa mwaka 1794, maputo yenye gesi ya hidrojeni yalikuwa yakitumiwa na majenerali Wafaransa kupeleleza vikosi vya maadui na kuongoza vikosi vyao. Pia, maputo yalitumiwa katika Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe nchini Marekani na pia katika vita kati ya Ufaransa na Prussia ya miaka ya 1870. Na katika vita viwili vya ulimwengu vilivyopiganwa katika karne iliyopita, maputo yalitumiwa sana na Wafaransa, Waingereza, Wajerumani, na Wamarekani ili kupeleleza maeneo ya maadui.

Maputo yalitumiwa kama vifaa vya maangamizi katika Vita vya Pili vya Ulimwengu jeshi la Wajapani liliporusha kuelekea Marekani maputo 9,000 yasiyo na mtu na yaliyojazwa mabomu. Zaidi ya maputo 280 yaliyojazwa mabomu yalifika Amerika Kaskazini.

Ndege za Vita Zatazamiwa

Tangu zilipobuniwa, ndege zilionwa kuwa zinaweza kutumiwa kama vifaa vya kivita. Mnamo 1907 Alexander Graham Bell alisema hivi: “Ni watu wachache sana wanaojua Marekani iko karibu kadiri gani kutatua tatizo ambalo litabadili vita kotekote ulimwenguni, yaani, kubuni ndege ya vita inayofaa hali zote.” Mwaka huohuo, gazeti The New York Times lilimnukuu Kapteni wa puto Thomas T. Lovelace akisema hivi: “Katika muda wa miaka miwili hadi mitano kila taifa kubwa litakuwa na ndege za kivita za aina mbalimbali kama tu kulivyo na manowari za aina mbalimbali.”

Miezi mitatu tu baadaye ndugu wawili wa familia ya Wright walipata kandarasi kutoka Jeshi la Marekani ili waunde ndege ya kwanza ya kivita. Makala katika gazeti New York Times la Septemba 13, 1908 (13/9/1908), ilifafanua kwa nini jeshi lilihitaji ndege hiyo: “Bomu litaweza kuangushwa ndani ya bomba la moshi la meli ya kivita, likisababisha uharibifu mkubwa kwenye mitambo ya meli na kisha kulipua matangi ya kutokeza mvuke wa kuendeshea meli.”

Maneno ya Bell yalithibitika kuwa kweli kwani ndege “zilibadili mbinu za kivita ulimwenguni pote.” Kufikia mwaka wa 1915, watengenezaji wa ndege walitengeneza ndege yenye bunduki za kumimina risasi kupitia propela zake. Ndege zenye uwezo wa kuangusha ndege nyingine zilifuatiwa na ndege zenye uwezo wa kuangusha makombora ambazo zilizidi kuwa kubwa na zenye nguvu zaidi kufikia wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Agosti 6, 1945 (6/8/1945) ndege inayoitwa B-29 Superfortress iliangusha bomu la kwanza la atomiki kuwahi kutumiwa katika vita ambalo liliangamiza jiji la Hiroshima huko Japani na kuua karibu watu 100,000.

Miaka miwili tu mapema, mnamo 1943, Orville Wright alisikika akisema faraghani kuwa anasikitika kwamba ndege ilibuniwa. Alisema kwamba katika vita hivyo viwili, ndege ilikuwa imebadilishwa kuwa silaha hatari. Tangu wakati huo kubuniwa kwa makombora yanayoweza kuelekezwa mahali hususa na mabomu mengine ya kisasa yameifanya ndege kuwa kifaa hatari zaidi huku ‘taifa likisimama kupigana na taifa.’—Mathayo 24:7.

[Picha katika ukurasa wa 22, 23]

1. Puto lisilo na watu lililojazwa mabomu

2. Puto la barrage

[Hisani]

Library of Congress, Prints & Photographs Division, FSA/OWI Collection, LC-USE6-D-004722

3. B-29 Superfortress

[Hisani]

USAF photo

4. F/A-18C Hornet

5. F-117A Nighthawk Stealth Fighter

[Hisani]

U.S. Department of Defense