Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Papa Wanaangamizwa

Papa Wanaangamizwa

 Papa Wanaangamizwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

NI WANYAMA wachache sana wanaotisha kuliko papa. Kila mwaka ulimwenguni pote, kuna wastani wa mashambulizi 75 hivi ya papa ambayo hutokea bila papa kuchokozwa na karibu 10 kati ya hayo husababisha kifo. Mashambulizi hayo ambayo hutangazwa kila mahali na maoni mabaya yanayoonyeshwa kwenye sinema humfanya papa aonekane kuwa mla-watu. Bila shaka, mtu anapaswa kuwa mwangalifu anaposhughulika na papa. Hata hivyo, kusema kweli watu wengi zaidi hufa kwa sababu ya kuumwa na nyuki au mamba kuliko wale wanaoshambuliwa na papa.

Kinyume cha hilo, papa anashambuliwa na wanadamu. “Kila mwaka papa milioni 100 wanakamatwa. Hao ni wengi sana hivi kwamba ikiwa tungewaunganisha mmoja baada ya mwingine, wangezunguka dunia mara tano,” akasema mtu mmoja anayefanya utafiti kwa ajili ya shirika la Argus la Wanasayansi Wanaochunguza Bahari katika gazeti Premier. Kuongezea hilo, wao hawazai sana, wanachukua muda mrefu kukomaa, kipindi chao cha kubeba mimba huwa kirefu, na maeneo wanayopenda kuzaliana yanachafuliwa. Matokeo ya mambo yote hayo ni kupungua kwa idadi ya papa. Idadi yao ikipungua sana, itachukua miaka mingi kurudia hali ya zamani.

Papa wengi wanakamatwa ili wakatwe mapezi yao, ambayo yanapendwa sana na watu fulani wa Asia kwa madai ya kwamba yanaweza kutumiwa kwa matibabu na kuamsha hamu ya ngono. * Supu ya mapezi ya papa ni tamu na ghali, bakuli moja linaweza kugharimu dola 150! Jitihada za kutosheleza soko hilo la Asia ndizo zimetokeza zoea katili na lenye kuharibu la kukata mapezi ya papa walio hai na kuwarudisha baharini ili wafe kwa njaa au wazame.

Ni Lazima Hatua Zichukuliwe Ili Kuwaokoa

Je, matatizo yanayokabili papa yanapaswa kutuhangaisha? Huenda tusiwahurumie  papa kadiri ileile tunayowahurumia tembo au nyangumi. Hata hivyo, tunapaswa kutambua fungu lao muhimu la kudumisha usawaziko unaoendeleza uhai katika bahari. Kwa mfano, ulaji wao unasaidia kuhakikisha samaki wengine hawaongezeki kupita kiasi.

Katika nchi fulani hakuna sheria za kudhibiti uvuvi wa papa. Baada ya majadiliano ya miaka kumi, sheria ya kuzuia kukata mapezi ya papa ilipitishwa hivi majuzi nchini Mexico, ambako papa huvuliwa sana. Zaidi ya tani 30,000 huvuliwa kila mwaka nchini humo. Ili kuonyesha zaidi matatizo yanayohusika, biashara ya mapezi ya papa imefanya watu waanze kuvua bila idhini katika hifadhi za bahari sehemu mbalimbali ulimwenguni. Kwa mfano, msimamizi wa Mbuga ya Kitaifa ya Galápagos analalamika: “Kuvuliwa kwa papa bila idhini kwa ajili ya mapezi yao katika Galapagos kumeongezeka sana katika miaka michache iliyopita. Ni biashara yenye faida kubwa na imetokeza wahalifu.”

Hatua muhimu imechukuliwa ili kuokoa papa. Zoea la kukata mapezi ya papa lilipigwa marufuku katika nchi fulani. Hata hivyo, Charlotte Mogensen, ofisa wa kupanga sera kwa ajili ya Hazina ya Wanyamapori Ulimwenguni, anaonya kwamba mengi zaidi yanahitaji kufanywa. Anasema: “Papa wanakabili hatari ulimwenguni pote. Tunasihi mashirika yote ya uvuvi yapige marufuku ukataji wa mapezi ya papa na pia yaweke matakwa ya kukusanya habari kuhusu papa, kupunguza idadi ya papa wanaopaswa kuvuliwa, na kuhakikisha kwamba papa wanaendelea kuzaliana.”

Inafurahisha kwamba Muumba wa wanyamapori hataruhusu uumbaji wake uendelee kuharibiwa kwa muda mrefu. Hiyo inatia ndani mnyama anayetisha lakini muhimu sana, yaani, papa.—Ufunuo 11:18.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Kinyume na inavyofikiriwa, mapezi ya papa yamegunduliwa kuwa na kiasi kikubwa sana cha zebaki kinachoweza kuwafanya wanaume wapoteze nguvu za uzazi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

UKWELI KUHUSU PAPA

Ukubwa: Papa mkubwa zaidi ni papa nyangumi (juu), anayeweza kufikia urefu wa mita 18 na uzito wa tani kadhaa. Lakini ni mnyama asiyedhuru anayekula uduvi na samaki wadogo.

Kipindi cha kubeba mimba: Anaweza kuzaa baada ya kubeba mimba kwa miezi 22.

Idadi ya watoto: Inakadiriwa kwamba papa anaweza kuzaa watoto wawili hadi kumi kwa wakati mmoja. Jamii nyingi za papa huzaa na nyingine hutaga mayai.

Ukuzi: Mara nyingi inachukua miaka 12 hadi 15 kufikia uwezo wa kuzaa.

Muda wa kuishi: Ni vigumu kukadiria muda ambao papa wengi huishi, lakini papa mweupe mkali (chini) anakadiriwa kuwa anaweza kuishi kwa miaka 60.

[Picha zimeandalilwa na]

Seawatch.org

© Kelvin Aitken/age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kati ya zaidi ya aina 300 za papa, 62 wanakabili hatari ya kutoweka

[Picha zimeandalilwa na]

© Mark Strickland/SeaPics.com

[Picha katika ukurasa wa 17]

Gramu 450 hivi za mapezi ya papa zinaweza kuuzwa kwa dola 200 au zaidi. Seti ya taya za papa mweupe inaweza kuwa dola 10,000

[Hisani]

© Ron & Valerie Taylor/SeaPics.com