Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mwaka wa 2006 ulikuwa mwaka “wa sita wenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa.” Miaka kumi yenye joto zaidi imerekodiwa katika muda wa miaka 12 iliyopita.—SHIRIKA LA UTABIRI WA HALI YA HEWA ULIMWENGUNI.

Katika jitihada zake za kukomesha kichaa cha mbwa, Idara ya Usalama wa Umma ya Beijing imesema kwamba kila familia itaruhusiwa kuwa na “mbwa mmoja” tu. Katika mwaka wa 2004, watu 2,660 hivi walikufa kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa huko China.—XINHUA ONLINE, CHINA.

Watu wanaoshika vitasa vya milango, taa, simu, na vifaa vya kubonyezea televisheni kwa mbali katika vyumba vya hoteli wana “uwezekano wa asilimia 50 wa kuambukizwa virusi vya mafua.”—MACLEAN’S, KANADA.

Kuhesabu Wadudu Katika Amazoni

Kufikia sasa, wataalamu wa wadudu wamegundua jamii 60,000 hivi za wadudu katika msitu wa mvua wa Amazoni. Gazeti Folha Online linasema kwamba bado jamii 180,000 hivi hazijagunduliwa. Kwa sasa kuna wataalamu 20 wa wadudu wanaofanya kazi huko. Takwimu za karibuni zinaonyesha kwamba kwa wastani wataalamu hao huainisha na kufafanua jamii 2.7 za wadudu kila mwaka. Hivyo itachukua vizazi 90 hivi vya wataalamu hao wakifanya kazi kwa miaka 35 kila moja, au jumla ya miaka 3,300 kuainisha wadudu hao wote!

Ukosefu wa Nishati

“Inakadiriwa kwamba watu bilioni 1.6, yaani, karibu robo ya watu ulimwenguni, hawana umeme, na watu bilioni 2.4 hutumia makaa, samadi, au kuni kupikia au kupasha nyumba joto,” linasema gazeti Our Planet linalochapishwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa. “Moshi unaotokezwa na vitu hivyo unasababisha magonjwa yanayowaua wanawake na watoto milioni mbili na nusu hivi kila mwaka.”

Mateso Kwenye Intaneti

Vituo vya Intaneti vya umma huwaruhusu watu kuanzisha urafiki na watu wasiowajua na inasemekana kwamba kufanya hivyo kutawafanya wahisi wanapendwa zaidi. Gazeti Folha Online linasema kwamba waongo, wabaguzi wa rangi, na wadaku hupenda sana vituo hivyo. Watu fulani wanaotumia vituo hivyo hawajitambulishi kikamili. Wengine huwakejeli watu wanene kupita kiasi, wafupi, walio na nywele mbaya, na kadhalika, na hivyo kuwaumiza sana kihisia. Mwanasaikolojia Mbrazili, Ivelise Fortim, anasema kwamba hilo hutukia kwa sababu “wale wanaofanyiwa kejeli huona mambo yanayotukia kwenye mtandao kuwa muhimu kuliko maisha yao ya kawaida.”

Kifaa cha Kale cha Kupigia Hesabu

Wapiga mbizi wanaotafuta sifongo waliokota kifaa kimoja chenye kutu katika meli moja ya Waroma iliyozama kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Antikýthēra mnamo 1901. Kifaa hicho kimetambuliwa kuwa kifaa tata cha karne ya pili K.W. K. kilichotumiwa kupigia hesabu za miendo ya nyota. Wanasayansi waliokichunguza hivi karibuni wakitumia eksirei ya kompyuta ya hali ya juu waligundua kwamba kifaa hicho kilikuwa na magurudumu ya shaba 30 hivi yenye meno ya gia na awali kilikuwa kimewekwa ndani ya sanduku la mbao. Kifaa hicho kingeweza kuonyesha kwa usahihi miendo ya jua na mwezi na kutabiri kupatwa kwa mwezi au jua. Kulingana na gazeti Nature, kifaa hicho ni “tata sana kuliko kifaa chochote kilichoundwa katika muda wa miaka 1,000 iliyofuata.”

[Picha katika ukurasa wa 21 zimeandaliwa na]

AP Photo/Thanassis Stavrakis