Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Wakati Magonjwa Hayatakuwapo Tena! (Januari 2007) (Mwezi wa 1) Mnaposema kwamba watu wengine “wanapoteza pesa na wakati kwa ajili ya matibabu na dawa ambazo hazitibu au hata zenye madhara,” inaonekana ni kana kwamba mnawaambia watu wasitumie matibabu ya badala kwa kuwa makala hiyo ilikuwa na shaka kuhusu matibabu ya aina hiyo. Je, hilo linamaanisha kwamba Amkeni! linaunga mkono matibabu ya kitaalamu kama njia salama na inayofaa zaidi? Kulingana na Shirika la General Accounting Office la Marekani, kuna uthibitisho wa kutosha kuonyesha kwamba matibabu ya kitaalamu si salama na hayafai.

G. C., Marekani

“Amkeni!” linajibu: Matibabu mengi ambayo yalipendwa sana na kwa kadiri fulani yalionekana salama na yenye kufaa hatimaye yamethibitika kuwa hayafai. Hilo limeonekana kwenye nyanja ya matibabu ya kitaalamu na hata katika matibabu ya badala. Uamuzi wa busara ni kuwa na habari muhimu kuhusu jinsi dawa fulani inavyoweza kufaa na hatari inayoweza kutokea kutokana na matibabu unayotumia, yawe matibabu ya kitaalamu au ya badala, na kuhakikisha kwamba matibabu hayo hayapingani na kanuni za Biblia. Huo ni uamuzi wa kibinafsi. Kama ambavyo tumeeleza mara nyingi, “Amkeni!” halipendekezi matibabu yoyote hususa. Na Wakristo wanajizuia kuingilia au kulaumu maamuzi ya wengine inapohusu matibabu. Kama makala hizo zilivyoonyesha, hakuna matibabu yoyote yawe ya badala au ya kitaalamu, yanayoweza kuwa suluhisho la matatizo ya kiafya ya wanadamu. Ni Ufalme wa Mungu pekee ndio utakaoleta kipindi ambacho hakutakuwa na magonjwa. —Ufunuo 21:3, 4.

‘Nitapanda Juu Kama Vile Paa Anavyofanya’ (Agosti 2006) (Mwezi wa 8) Uvumilivu na unyenyekevu wa Francesco Abbatemarco, ulinifanya nifikiri kwa uzito sana. Hakujitahidi kushinda ulemavu wake ili tu kumtumikia Yehova, bali pia alifanya bidii kushinda hisia zake zisizofaa. Simulizi lake limenisaidia kuona kwamba hata tuwe tunakabili tatizo gani, tunaweza kumtumikia Yehova kwa kadiri ya uwezo wetu. Nilitiwa moyo pia kuona jinsi Neno la Mungu lilivyomsaidia kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yake.

N. G., Kambodia

Francesco alihitaji kushinda vikwazo vingi. Hata hivyo, alipopata kweli, kwa shauku kubwa na bila kulazimishwa alikabiliana navyo vyote. Ndugu huyo ni mfano mzuri wa uimara! Ninatumaini simulizi lake litawatia moyo watu wengi kama lilivyonitia moyo.

M. D., Afrika Kusini

Nimelipenda sana simulizi hilo! Laiti ningeweza kumwambia Francesco Abbatemarco ana kwa ana jinsi ambavyo simulizi hilo limenitia moyo kujitahidi zaidi katika utumishi wangu kwa Yehova.

J. B., Marekani

Asante sana Francesco kwa bidii na uvumilivu wako. Nina hakika kwenye mfumo mpya utapanda juu kama vile paa anavyofanya. Kumbuka una ndugu na dada ambao wanakupenda na kusali kwa ajili yako.

S. G., Urusi