Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kamchatka—Rasi Maridadi Kwenye Pasifiki

Kamchatka—Rasi Maridadi Kwenye Pasifiki

KamchatkaRasi Maridadi Kwenye Pasifiki

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI URUSI

ZAIDI ya miaka 300 iliyopita wavumbuzi Warusi waliokuwa wakielekea mashariki kupitia Asia walifika kwenye rasi yenye milima iliyochomoza kusini kwenye Bahari ya Pasifiki. Rasi hiyo ilitenganisha Bahari ya Okhotsk na Bahari ya Bering. Bado watu wengi hawalijui eneo hilo maridadi ambalo ni kubwa kidogo kuliko Italia.

Wakati wa majira ya baridi kali, sehemu za pwani za Kamchatka huwa na baridi kiasi zikilinganishwa na sehemu zake za bara ambazo hupata theluji inayofikia zaidi ya mita 6 na wakati mwingine hata karibu mita 12! Wakati wa kiangazi, mara nyingi rasi hiyo hufunikwa na ukungu unaotoka baharini na hupigwa na upepo mkali. Mvua nyingi ambayo hunyesha huko Kamchatka hufanya udongo wa volkano utokeze mimea mbalimbali, kutia ndani vichaka vya miforosadi, nyasi zenye urefu kama wa mwanadamu, na maua maridadi ya mwituni, kama vile ua la waridi linalojulikana kama malkia wa mbuga.

Aina fulani ya miti ya mibetula inapatikana katika sehemu kubwa ya rasi hiyo. Mashina na matawi ya miti hiyo yamejikunja na kujipinda kwa sababu ya upepo mkali na theluji nzito. Miti hiyo ambayo hukua polepole na inaweza kustahimili hali ngumu, ina mbao ngumu na mizizi imara. Hilo huiwezesha kukua mahali popote hata inaweza kukua kwa mshazari kwenye majabali! Majani yake huchipuka mwezi wa Juni (Mwezi wa 6), mara nyingi bado kukiwa na theluji, na hugeuka rangi ya manjano mwezi wa Agosti (Mwezi wa 8), na hiyo huwa ni dalili ya kukaribia kwa majira ya baridi kali.

Volkano na Chemchemi za Maji Moto na za Mvuke

Ikiwa kwenye Eneo la Pasifiki Lenye Volkano, Kamchatka ina volkano 30 hivi zilizo hai. Kilele cha volkano inayoitwa Klyuchevskaya kimefafanuliwa kuwa “kilele maridadi sana.” Kina urefu wa mita 4,750 juu ya usawa wa bahari, na hivyo kufanya mlima huo kuwa volkano kubwa zaidi iliyo hai katika mabara ya Ulaya na Asia. Tangu 1697, mwaka ambao wavumbuzi Warusi walifika Kamchatka, milipuko zaidi ya 600 imerekodiwa katika rasi hiyo.

Katika miaka ya 1975/1976 milipuko ya volkano iliyotokea kwenye eneo la Tolbachik ilitokeza “mioto” iliyoruka mita 2,500! Kulikuwa na radi katikati ya mawingu ya majivu. Milipuko hiyo iliyoendelea kwa karibu mwaka moja na nusu bila kukoma ilitokeza milima minne ya volkano. Maziwa na mito ilitokomea, na majivu ya moto yaliteketeza misitu mizima mpaka kwenye mizizi. Maeneo makubwa yaligeuzwa kuwa jangwa.

Jambo linalopendeza ni kwamba milipuko mingi ilitokea mbali na makazi ya watu, na ni watu wachache sana waliokufa. Lakini wageni wanapaswa kujihadhari hasa wanapoenda kwenye Bonde la Kifo, ambalo liko chini ya mlima wa volkano wa Kichpinych. Kunapokuwa hakuna upepo, na hasa wakati theluji inapoyeyuka, gesi zenye sumu za volkano hutanda kwenye bonde hilo na hivyo kuhatarisha maisha ya wanyama. Wakati mmoja, bonde hilo lilikuwa na mizoga ya dubu kumi na wanyama wengi wadogo.

Bonde kubwa linaloitwa Uzon, lina shimo lenye matope yanayotokota na maziwa yenye maji moto yaliyo na miani yenye rangi nyingi. Eneo hilo pia lina Bonde la Chemchemi za Maji Moto na Mvuke lililovumbuliwa mwaka wa 1941. Baadhi ya chemchemi hizo hulipuka kila baada ya dakika mbili au tatu, na nyingine baada ya siku chache. Helikopta huwazungusha wageni kwenye maeneo hayo yanayopendeza yaliyo kilomita 180 hivi kaskazini ya jiji la Petropavlovsk-Kamchatskiy. Hata hivyo, idadi ya watalii hudhibitiwa sana ili kupunguza uharibifu wa mazingira katika eneo hilo. Kwa sababu hiyo, maeneo sita huko Kamchatka yameorodheshwa kati ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni.

Kamchatka ina chemchemi nyingi za maji moto, na nyingi kati ya hizo zina maji yenye kiwango cha joto kati ya 30 na 40 Selsiasi ambayo huwafurahisha watalii na kuwaburudisha wakati wa miezi mirefu ya baridi kali. Joto kutoka kwenye chemchemi hizo hutumiwa pia kuzalisha umeme. Kwa kweli, kituo cha kwanza cha umeme nchini Urusi kinachotegemea joto la chemchemi kilijengwa katika rasi hiyo.

Dubu, Salmoni, na Tai

Bado kuna dubu wa rangi ya kahawia 10,000 hivi huko Kamchatka. Wana uzito wa kilogramu 150 hadi 200 kwa wastani, ingawa wanaweza kuzidi uzito huo mara tatu ikiwa hawatauawa. Katika hekaya za wenyeji wa asili wanaoitwa Itelmen, dubu walikuwa “ndugu” zao, nao waliwaheshimu wanyama hao. Undugu huo ulikwisha bunduki zilipoanza kutumiwa. Sasa wahifadhi wa mazingira wanahofia kwamba wanyama hao watatoweka.

Dubu hao huwaogopa wanadamu na hivyo si rahisi kuwaona. Lakini katika mwezi wa Juni, salmoni wanapoanza kutaga mayai, dubu hujitokeza kwa wingi kula samaki hao, na dubu mmoja anaweza kula salmoni 24 hivi! Kwa nini wao hula sana hivyo? Wakati wa kiangazi, lazima dubu hao wakusanye mafuta mengi sana mwilini ili waweze kustahimili miezi ya majira ya baridi kali kunapokuwa hakuna chakula.Wakati wa majira hayo, wao hulala katika mapango ili kuhifadhi nishati yao.

Mnyama mwingine anayependa kula salmoni ni tai anayeitwa Steller, ndege mwenye kupendeza aliye na mabawa yenye upana wa mita 2.5 kutoka ncha moja hadi nyingine. Sehemu kubwa ya mwili wa ndege huyo ni nyeusi naye ana baka jeupe kwenye mabega na mkia mweupe. Ndege hao ambao wanazidi kupungua, kwa sasa ni karibu 5,000 tu, nao wanapatikana katika eneo hilo tu, na mara kwa mara wanaweza kupatikana katika visiwa vya Aleutia na Pribilof huko Alaska. Ndege hao hutumia kiota kilekile mwaka baada ya mwaka, wakikirekebisha na kukiongezea. Kiota kimoja kilikuwa na kipenyo cha mita tatu, nacho kilikuwa kizito sana hivi kwamba kilivunja mti wa mbetula ambao kiota hicho kilikuwa kimejengwa juu yake!

Wakazi wa Kamchatka

Wengi wa wakazi wa kisasa wa Kamchatka ni Warusi, lakini bado kuna maelfu kadhaa ya wenyeji wa asili, kikundi kikubwa kati yao wakiwa Wakoryak, ambao huishi sehemu za kaskazini za Kamchatka. Wakazi wengine wanatia ndani Wachukchi na Itelmen, na wote wana lugha zao. Wakazi wengi wa Kamchatka huishi Petropavlovsk-Kamchatskiy, kituo cha kuendeshea shughuli za serikali. Maeneo yale mengine ya rasi hiyo hayana watu wengi, na vijiji vingi vilivyoko pwani na kandokando ya mito vinaweza kufikika tu kwa mashua au ndege.

Uchumi wa eneo hilo hutegemea uvuvi wa samaki na kaa. Kaa wakubwa wekundu wa Kamchatka hupendwa sana. Kaa hao wenye upana wa mita 1.7 kutoka ukucha wa mguu moja hadi ule mwingine, huonekana wana rangi zenye kupendeza wakiwa wametandazwa sokoni.

Tangu 1989, Mashahidi wa Yehova wametembelea Kamchatka wakikusudia kufanya uvuvi tofauti. Wakiwa “wavuvi wa watu,” wamekuwa wakiwaletea habari njema ya Ufalme wa Mungu watu wanaoishi katika eneo hilo la mbali la Kamchatka. (Mathayo 4:19; 24:14) Baadhi ya wakazi hao wameitikia na sasa wanawasaidia wengine kumjua na kumwabudu Muumba, Yehova Mungu, badala ya kuabudu uumbaji wake. Matokeo yake ni kwamba wenyeji wengi wanawekwa huru kutokana na hofu ya roho waovu. (Yakobo 4:7) Wanajifunza pia kuhusu wakati ujao ambapo uovu na waovu wote wataondolewa, na dunia nzima “itajawa na kumjua Yehova kama vile maji yanavyoifunika bahari.”—Isaya 11:9.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

BONDE MARIDADI SANA

Bonde la Uzon, lililofanyizwa kutokana na volkano ya kale lina kipenyo cha kilomita kumi. Kitabu kimoja kinasema kwamba ndani ya bonde hilo mna “kila kitu kinachofanya Kamchatka kuwa maarufu.” Bonde hilo lina chemchemi za maji moto na baridi; mashimo yenye matope yanayotokota; vilima vya tope lenye moto; maziwa safi yenye samaki na bata-maji, na mimea mingi.

Kitabu Miracles of Kamchatka Land kinasema kwamba “hakuna mahali popote pengine Duniani” ambapo majira ya kupukutika kwa majani huwa mafupi lakini maridadi sana. Nyanda nyekundu za eneo hilo hutofautiana sana na miti ya mibetula yenye rangi ya dhahabu na manjano. Wakati huohuo ardhi hutoa mvuke mweupe ambao huonekana waziwazi kwenye anga la bluu. Na mapema asubuhi, misitu “huimba” mamilioni ya majani yaliyo na umande yanapoanguka kwa sauti nyororo, kuonyesha kwamba majira ya baridi kali yanakaribia.

[Sanduku katika ukurasa wa 19]

ZIWA HATARI!

Mnamo 1996, volkano iliyofikiriwa kuwa haitendi ililipuka chini ya Ziwa Karymsky, na kutokeza mawimbi yenye urefu wa mita kumi ambayo yaliangusha miti katika misitu inayozunguka ziwa hilo. Katika muda wa dakika chache tu, ziwa hilo likawa na asidi nyingi sana hivi kwamba hakuna kiumbe ambacho kingeendelea kuwa hai humo. Hata hivyo, hakuna wanyama waliopatikana wakiwa wamekufa karibu na ziwa hilo licha ya kwamba majivu ya volkano hiyo na mawimbi yalienea kotekote katika ufuo, anaeleza mtafiti Andrew Logan. “Kabla ya mlipuko huo,” anasema, “kulikuwa na mamilioni ya samaki (hasa salmoni na trauti) katika Ziwa Karymsky. Baada ya mlipuko huo hakukuwa na kiumbe yeyote katika ziwa hilo.” Hata hivyo, huenda samaki kadhaa waliokoka. Wanasayansi wanakisia kwamba huenda jambo fulani, kama vile kubadilika kwa maji, liliwaonya samaki na kuwafanya wakimbilie Mto Karymsky ulio karibu.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

URUSI

KAMCHATKA