Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kumhoji Mtaalamu wa Biokemia

Kumhoji Mtaalamu wa Biokemia

Kumhoji Mtaalamu wa Biokemia

MNAMO 1996, Michael J. Behe, ambaye sasa ni profesa wa biokemia katika Chuo Kikuu cha Lehigh, Pennsylvania, Marekani alitoa kitabu chake kiitwacho Darwin’s Black Box—The Biochemical Challenge to Evolution. Toleo la Amkeni! la Mei 8, 1997, lilikuwa na makala ya mfululizo yenye kichwa “Tulikujaje Kuwapo?—Kwa Aksidenti au kwa Ubuni?” ambayo ilirejelea kitabu cha Behe. Katika kipindi cha miaka kumi hivi tangu kitabu Darwin’s Black Box kichapishwe, wanasayansi wanaotetea mageuzi wamejitahidi kupinga hoja za Behe. Wachambuzi wamemlaumu Behe, ambaye ni Mkatoliki, wakidai kwamba ameruhusu imani yake ya kidini iathiri maoni yake ya kisayansi. Wengine wanadai kwamba maoni yake hayapatani na sayansi. Mwandishi wa Amkeni! alimhoji Profesa Behe ili kujua kwa nini maoni yake yamezua ubishi.

MWANDISHI WA AMKENI!: KWA NINI UNAFIKIRI VITU VILIVYO HAI VINATHIBITISHA KWAMBA VILIBUNIWA NA MTU MWENYE AKILI?

PROFESA BEHE: Tunapoona sehemu za mashine zilizopangwa kwa utaratibu ili kufanya kazi fulani tunakata kauli kwamba ilibuniwa. Kwa mfano, fikiria mashine tunazotumia kila siku kama vile mashine ya kukata nyasi, gari, au zile ambazo si tata. Mimi hupenda kutoa mfano wa mtego wa panya. Unakata kauli kwamba mtego wa panya ulibuniwa kwa kuwa una sehemu zilizopangwa kwa utaratibu ili kumnasa panya.

Wanasayansi wamefanya maendeleo hivi kwamba wamegundua jinsi ambavyo sehemu ndogo zaidi za vitu hai hufanya kazi ili kuendeleza uhai wa vitu hivyo. Inashangaza kwamba wanasayansi wamegundua kuna mashine tata zinazofanya kazi katika sehemu hizo za vitu hai. Kwa mfano, katika chembe kuna “malori” madogo yanayosafirisha vitu muhimu katika chembe. Kuna “ishara ndogo za barabarani” zinazoelekeza “malori” hayo kulia au kushoto. Chembe fulani zina “mota” ndogo ambazo huzisukuma kwenye umajimaji. Watu wakiona mashine nyingine yoyote tata inayofanya kazi, watakata kauli kwamba ilibuniwa. Licha ya madai ya nadharia ya Darwin kuhusu mageuzi, hakuna kauli nyingine tunayoweza kukata. Kwa kuwa ni kawaida kukubali kwamba mashine yenye sehemu zilizopangwa kwa utaratibu ilibuniwa, tuna sababu nzuri ya kukata kauli kwamba mifumo ya sehemu hizo ndogo zaidi za vitu hai ilibuniwa na mtu mwenye akili.

MWANDISHI WA AMKENI!: UNAFIKIRI NI KWA NINI WENGI WA WANASAYANSI WENZAKO HAWAKUBALIANI NA MAONI YAKO KWAMBA VITU VILIBUNIWA NA MTU MWENYE AKILI?

PROFESA BEHE: Wanasayansi wengi hawakubaliani na maoni yangu kwamba kuna mbuni mwenye akili kwa kuwa wazo hilo linapita ufafanuzi wa kisayansi, kwani linaonyesha waziwazi kwamba kuna chanzo kikuu kuliko ulimwengu wa asili. Watu wengi hawafurahishwi na kauli hiyo. Hata hivyo, inakubalika kwamba sayansi inapaswa kukubaliana na uthibitisho uliopo bila kuegemea upande wowote. Kwa maoni yangu, kukataa jambo ambalo limethibitishwa kabisa kwa sababu tu ya kuogopa matokeo ya kufanya hivyo si tendo la ujasiri.

MWANDISHI WA AMKENI!: UNA MAONI GANI KUHUSU WACHAMBUZI WANAODAI KWAMBA WATU WASIO NA UJUZI NDIO WANAOAMINI KWAMBA KUNA MBUNI MWENYE AKILI?

PROFESA BEHE: Hatuamini kwamba kuna mbuni kwa sababu hatuna ujuzi. Imani hiyo haitegemei yale tusiyojua; inategemea yale tunayojua. Darwin alipochapisha kitabu chake The Origin of Species miaka 150 iliyopita, uhai ulionekana kuwa kitu rahisi sana. Wanasayansi walifikiri kwamba chembe haikuwa tata sana na hivyo ingeweza kujitokeza kutokana na matope ya bahari. Lakini tangu hapo, wanasayansi wamegundua kwamba chembe ni tata sana kuliko mashine yoyote ya karne hii ya 21. Chembe hizo tata zinazofanya kazi zinathibitisha kwamba kuna mbuni mwenye kusudi.

MWANDISHI WA AMKENI!: JE, SAYANSI IMETOA UTHIBITISHO WOWOTE KWAMBA MAGEUZI, KUPITIA UTEUZI WA KIASILI, YAMETOKEZA MASHINE HIZO TATA ZA SEHEMU NDOGO ZAIDI ZA VITU HAI AMBAZO UNAZUNGUMZIA?

PROFESA BEHE: Ukichunguza vitabu vya sayansi, utagundua kwamba hakuna mwanasayansi ambaye amejaribu sana, iwe kwa kufanya majaribio au kwa kuunda vigezo vya kisayansi, kuthibitisha jinsi mashine hizo ndogo zilivyojitokeza kwa mageuzi. Wameshindwa kufanya hivyo licha ya kwamba katika kipindi cha miaka kumi tangu kitabu changu kilipochapishwa, mashirika mengi ya kisayansi kama vile Shirika la Kitaifa la Sayansi la Marekani na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kisayansi, yamewahimiza washiriki wake wajitahidi wawezavyo kupinga wazo la kwamba vitu hai vinathibitisha kuwa kuna mbuni mwenye akili.

MWANDISHI WA AMKENI!: UNA MAONI GANI KUHUSU WALE WANAOSEMA KWAMBA BAADHI YA VIUNGO AU SEHEMU ZA MIMEA NA WANYAMA ZILIBUNIWA VIBAYA?

PROFESA BEHE: Kutojua kazi ya viungo au sehemu fulani za mimea na wanyama hakumaanishi kwamba havina kazi muhimu. Kwa mfano, ilifikiriwa kwamba viungo fulani ambavyo husemwa kuwa havina kazi, vinathibitisha kuwa mwili wa binadamu na vitu vingine vilibuniwa vibaya. Viungo kama vile kidole cha tumbo na mafindo vilionwa kuwa havina kazi na mara nyingi viliondolewa. Lakini baadaye ikagunduliwa kwamba vina kazi muhimu katika mfumo wa kinga na havikuonwa tena kuwa havina kazi.

Jambo lingine tunalopaswa kukumbuka ni kwamba katika biolojia vitu fulani hutukia kana kwamba kwa aksidenti. Gari langu likibonyea au gurudumu lake likitoboka, hilo halimaanishi kwamba gari hilo au gurudumu lake halikubuniwa. Hali kadhalika, uhakika wa kwamba vitu fulani vilitokea kwa aksidenti katika biolojia haumaanishi kwamba mashine ndogo zilizo tata sana za vitu hai zilijitokeza. Hoja kama hiyo haipatani na akili hata kidogo.

[Blabu katika ukurasa wa 12]

“Kwa maoni yangu, kukataa jambo ambalo limethibitishwa kabisa kwa sababu tu ya kuogopa matokeo ya kufanya hivyo si tendo la ujasiri”