Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?

Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?

 Je, Mageuzi Ni Jambo Hakika?

“MAGEUZI ni jambo hakika kama tu joto la jua lilivyo hakika,” anadai Profesa Richard Dawkins, mwanasayansi maarufu wa mageuzi. Bila shaka, majaribio na mambo hakika yanayotukia yanathibitisha kwamba jua lina joto. Lakini je, majaribio na mambo hakika yanayotukia yanatoa uthibitisho kama huo usioweza kupingwa kwamba mageuzi yalitukia?

Kabla ya kujibu swali hilo tunahitaji kufafanua jambo moja. Wanasayansi wengi wameona kwamba baada ya muda, wazao wa vitu vilivyo hai hubadilika kidogo. Charles Darwin aliita hatua hiyo “mnyumbuliko unaotokeza mabadiliko.” Mabadiliko hayo yameonekana, yakafanyiwa majaribio, na kutumiwa kwa mafanikio na wazalishaji wa wanyama na mimea. * Mabadiliko hayo yanaweza kuonwa kuwa mambo hakika. Hata hivyo, wanasayansi huita mabadiliko hayo madogo “mageuzi madogo.” Taarifa hiyo inaonyesha dhana ya wanasayansi wengi kwamba mabadiliko hayo madogo yanathibitisha jambo tofauti kabisa, jambo ambalo halijaonekana na yeyote, jambo ambalo wao huliita mageuzi makubwa.

Darwin alidai mengi zaidi kuliko mabadiliko yanayoweza kuonekana. Aliandika hivi katika kitabu chake maarufu The Origin of Species: “Sivioni vitu vyote kuwa viumbe vya pekee, bali naviona kuwa vitu vilivyotokana na vitu vichache vyenye uhai.” Darwin alisema kwamba katika kipindi kirefu cha wakati, vitu hivyo “vichache vilivyo hai” au vitu visivyo tata vyenye uhai, viligeuka polepole, kupitia “mabadiliko madogo sana,” na kutokeza mamilioni ya vitu vyenye uhai duniani. Wanamageuzi wanafundisha kwamba mabadiliko mengi madogo yalitokeza mabadiliko makubwa yaliyohitajika ili kugeuza samaki kuwa amfibia na sokwe kuwa watu. Mabadiliko hayo makubwa yanayodaiwa kuwa yalitukia ndiyo yanayorejelewa kuwa mageuzi makubwa. Wengi hufikiri kwamba dai hilo la pili linapatana na akili. Wao hujiuliza, ‘Ikiwa mabadiliko madogo yanaweza kutukia katika spishi, je, mageuzi hayawezi kutokeza mabadiliko makubwa katika kipindi kirefu cha wakati?’ *

Fundisho kuhusu mageuzi makubwa linategemea dhana tatu kuu:

1. Mabadiliko ya chembe za urithi yanaandaa vitu vinavyohitajika kutokeza jamii mpya. *

2. Uteuzi wa kiasili hutokeza jamii mpya.

3. Mabaki ya kale ya wanyama na mimea huonyesha kwamba mageuzi makubwa yalitukia katika mimea na wanyama.

Je, uthibitisho wa mageuzi makubwa ni wenye nguvu sana hivi kwamba inapaswa kuonwa kwamba yalitukia?

Je, Mabadiliko ya Chembe za Urithi Yanaweza Kutokeza Jamii Mpya?

Habari nyingi kuhusu mimea na wanyama zinategemea maagizo yaliyo katika chembe za urithi, yaani, maagizo yaliyo katika kiini cha kila  chembe. * Watafiti wamegundua kwamba mabadiliko ya chembe za urithi, au mabadiliko yasiyo na mpango ya maagizo katika chembe za urithi yanaweza kutokeza mabadiliko katika vizazi vya wanyama na mimea. Mnamo 1946, Hermann J. Muller, mshindi wa Tuzo la Nobeli na mwanzilishi wa uchunguzi wa mabadiliko ya chembe za urithi, alidai hivi: “Mabadiliko mengi madogo ambayo hayatokei mara nyingi si njia ya msingi ya mwanadamu kuboresha wanyama na mimea tu, bali ndiyo njia hasa ambayo mageuzi yakiongozwa na uteuzi wa kiasili yametukia.”

Kwa kweli, fundisho la mageuzi makubwa linategemea dai la kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayatokezi tu spishi mpya, yaani, aina za mimea na wanyama, bali pia jamii mpya kabisa. Je, kuna njia yoyote ya kuthibitisha dai hilo la kishupavu? Hebu fikiria kile ambacho kimefunuliwa katika miaka 100 hivi ya uchunguzi wa chembe za urithi.

Katika miaka ya 1930, wanasayansi walisisimkia wazo la kwamba ikiwa uteuzi wa kiasili, yaani, kusalimika kwa viumbe bora na kufa kwa visivyo bora, kungeweza kutokeza spishi mpya za mimea kutokana na mabadiliko yanayotukia bila mpango, basi mabadiliko hayo yakiongozwa na mwanadamu yanapaswa kuwa na matokeo makubwa zaidi. Wolf-Ekkehard Lönnig, mwanasayansi katika Taasisi ya Max Planck ya Utafiti wa Kuzalisha Mimea nchini Ujerumani, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Msisimko huo hasa ulienea miongoni wa wanabiolojia, na hasa miongoni mwa wataalamu wa chembe za urithi na wazalishaji wa mimea na wanyama.” Kwa nini kulikuwa na msisimko huo? Lönnig, ambaye amechunguza mabadiliko ya chembe za urithi kwa miaka 28 hivi, anasema: “Watafiti hao walidhani wakati wa kubadili njia za msingi za kuzalisha mimea na wanyama ulikuwa umewadia. Walifikiri kwamba kwa kuchochea mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, wangeweza kutokeza mimea na wanyama wapya walio bora.” *

Wanasayansi nchini Marekani, Asia, na Ulaya walianzisha miradi ya utafiti iliyodhaminiwa kwa pesa nyingi, nao walitumia njia walizotarajia kwamba zingeharakisha hatua za mageuzi. Kumekuwa na matokeo gani baada ya utafiti mkubwa ambao umechukua miaka 40? “Licha ya gharama kubwa,” asema mtafiti Peter von Sengbusch, “majaribio ya kutokeza mabadiliko ya chembe za urithi kupitia njia fulani ya kisayansi, yaliambulia patupu.” Lönnig alisema: “Kufikia miaka ya 1980, matumaini na msisimko uliokuwapo miongoni mwa wanasayansi yaligonga mwamba ulimwenguni pote. Miradi ya uchunguzi wa kuzalisha mimea na wanyama kwa kubadili chembe za urithi ilitupiliwa mbali katika nchi za Magharibi. Karibu mimea na wanyama wote waliotokezwa kwa kubadili chembe za urithi walikuwa na ‘dosari,’ nao walikufa au wakawa dhaifu kuliko wale ambao chembe zao zilibadilika kiasili.” *

Hata hivyo, habari ambayo imekusanywa kwa  miaka 100 ya utafiti wa mabadiliko ya chembe za urithi na hasa miaka 70 ya utafiti wa kuzalisha mimea na wanyama kwa kubadili chembe hizo, imewawezesha wanasayansi kukata kauli mbalimbali kuhusu uwezo wa kutokeza jamii mpya kwa kubadili chembe hizo. Baada ya kuchunguza uthibitisho uliokuwa umetolewa Lönnig alisema: “Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa. Kauli hiyo inapatana na majaribio na matokeo ya utafiti ambao umefanywa katika karne ya 20 na pia inapatana na sheria za uwezekano. Hivyo, sheria ya mabadiliko yanayojirudia-rudia huonyesha kwamba spishi ambazo zinatofautiana na spishi nyingine kwa kutegemea chembe za urithi huwa na mipaka hususa isiyoweza kuvunjwa au kuvukwa wakati mabadiliko ya chembe hizo yanapotokea kiaksidenti.”

Fikiria uzito wa kauli hiyo. Ikiwa wanasayansi stadi hawawezi kutokeza aina mpya za mimea na wanyama kwa kuchochea mabadiliko ya chembe za urithi na kuchagua chembe bora, je, mageuzi yasiyoongozwa na mtu mwenye akili yanaweza kuwa na matokeo bora? Ikiwa utafiti umethibitisha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadilisha spishi za awali na kutokeza mpya, mageuzi makubwa yangewezaje kutokea?

Je, Uteuzi wa Kiasili Unaweza Kutokeza Spishi Mpya?

Darwin aliamini kwamba ule aliourejelea kuwa uteuzi wa kiasili ungechagua viumbe ambavyo vingefaana na mazingira huku viumbe visivyofaana na mazingira vikifa na kutoweka. Wanamageuzi wa kisasa wanafundisha kwamba kadiri spishi zilivyoenea na kutengana, ndivyo uteuzi wa kiasili ulivyochagua viumbe ambavyo mabadiliko ya chembe zao za urithi yalivifanya vipatane zaidi na mazingira mapya. Wanamageuzi wanadai kwamba spishi hizo zilizojitenga hatimaye zilitokeza spishi mpya kabisa.

Kama ilivyosemwa mwanzoni, uchunguzi umethibitisha kwamba mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kamwe kutokeza aina mpya kabisa za mimea na wanyama. Hata hivyo, wanamageuzi wana uthibitisho gani wa kuunga mkono dai lao kwamba uteuzi wa kiasili unachagua chembe bora za urithi zilizobadilishwa ili kutokeza spishi mpya? Kijitabu kilichochapishwa mnamo 1999 na Shirika la Kitaifa la Sayansi (NAS) nchini Marekani kilisema hivi: “Mfano mmoja wenye kusadikisha wa mageuzi ya spishi mpya ulihusisha spishi 13 za shorewanda waliochunguzwa na Darwin katika Visiwa vya Galápagos. Ndege hao sasa wanaitwa shorewanda wa Darwin.”

Katika miaka ya 1970, watafiti kadhaa wakiongozwa na Peter na Rosemary Grant, walianza kuwachunguza shorewanda hao na wakagundua kwamba baada ya mwaka mzima wa ukame, idadi ya shorewanda wenye midomo mirefu waliosalimika ilizidi ile ya wale wenye midomo mifupi. Kwa kuwa ukubwa na umbo la midomo yao ndiyo njia moja kuu ya kutambulisha spishi hizo 13 za shorewanda, huo ulidhaniwa kuwa ugunduzi muhimu. Kijitabu hicho cha NAS kinasema, “Peter na Rosemary Grant wamekadiria kwamba ikiwa visiwa hivyo vitakumbwa na ukame mwaka moja katika kila kipindi cha miaka 10, spishi mpya ya shorewanda itatokezwa baada ya miaka 200 hivi.”

Hata hivyo, kile kijitabu cha NAS hakizungumzii baadhi ya mambo hakika yenye kuaibisha. Katika miaka iliyofuata mwaka huo wa ukame,  shorewanda wenye midomo mifupi walikuwa wengi tena kuliko wale wenye midomo mirefu. Hivyo mnamo 1987, Peter Grant na mhitimu wa chuo kikuu, Lisle Gibbs, waliandika katika jarida la sayansi Nature kwamba walishuhudia “uteuzi ukichukua mkondo ulio kinyume.” Katika 1991, Grant aliandika kwamba “idadi ya ndege, ikiongozwa na uteuzi wa kiasili, ilikuwa ikiongezeka na kupungua,” kila mara hali ya hewa ilipobadilika. Watafiti hao waligundua pia kwamba ndege wa “spishi” kadhaa tofauti walizalisha pamoja na kutokeza ndege waliostahimili kuliko wazazi wao. Peter na Rosemary Grant walikata kauli kwamba ikiwa ndege hao wangeendelea kuzalisha pamoja, baada ya kipindi cha miaka 200 hivi, “spishi” hizo mbili zingeungana na kuwa spishi moja.

Katika 1966, mwanabiolojia wa mageuzi George Christopher Williams aliandika hivi: “Nasikitika kwamba mwanzoni nadharia ya uteuzi wa kiasili ilianzishwa ili kufafanua jinsi mageuzi yalivyotokea. Nadharia hiyo inafaa zaidi kutumiwa kuelezea jinsi ambavyo viumbe hubadilika kulingana na mazingira yao.” Mnamo 1999, mtungaji wa nadharia za mageuzi Jeffrey Schwartz, aliandika kwamba ikiwa kauli ya Williams ni sahihi, uteuzi wa kiasili unaweza kusaidia wanyama na mimea kubadilika kulingana na hali zilizopo, lakini “hautokezi spishi mpya.”

Kwa kweli, shorewanda wa Darwin hawabadiliki na “kuwa ndege wapya.” Bado wao ni shorewanda. Na uhakika wa kwamba wanazalisha pamoja unatilia shaka mbinu za wanasayansi fulani za kuainisha spishi. Isitoshe, hilo limefichua kwamba hata taasisi mashuhuri za sayansi huripoti matokeo ya utafiti mbalimbali huku zikiegemea maoni yao.

Je, Mabaki ya Kale ya Wanyama Yanathibitisha Kwamba Mageuzi Makubwa Yalitokea?

Kijitabu cha NAS kilichonukuliwa mapema kinafanya msomaji afikiri kuwa mabaki ya kale ya wanyama ambayo wanasayansi wamepata yanathibitisha kabisa kwamba mageuzi makubwa yalitokea. Kinasema hivi waziwazi: “Aina nyingi za viumbe zimepatikana kati ya samaki na amfibia, reptilia na mamalia, na pia katika vizazi vya sokwe hivi kwamba imekuwa vigumu kutambua hasa wakati spishi moja inapobadilika na kuwa nyingine.”

Taarifa hiyo ya kishupavu inashangaza sana. Kwa nini? Mnamo 2004, jarida National Geographic lilisema kwamba rekodi ya mabaki ya kale ya wanyama ni kama “sinema ya mageuzi ambayo picha zake za matukio ya miaka 999 katika kila kipindi cha miaka 1,000, huondolewa katika chumba cha kutayarishia sinema.” Je, “picha” za matukio ya mwaka mmoja tu zinaweza kutoa habari ya kutosha kuhusu jinsi mageuzi makubwa yalivyotokea? Mabaki ya kale ya wanyama yanaonyesha nini hasa? Niles Eldredge, ambaye ni mwanamageuzi mshupavu anakubali kwamba uchunguzi wa mabaki ya kale ya wanyama umeonyesha kwamba katika vipindi virefu vya wakati “ni mageuzi madogo sana yaliyotukia katika spishi nyingi.”

Kufikia leo, wanasayansi ulimwenguni pote wamechimbua na kuorodhesha visehemu milioni 200 vikubwa na mabilioni ya visehemu vidogo vya mabaki ya kale ya wanyama. Watafiti wengi wanakubali  kwamba mabaki hayo mengi yanaonyesha jamii zote kuu za wanyama zilitokea wakati mmoja na hazijabadilika sana, na spishi nyingi zilitoweka ghafula kama zilivyotokea. Baada ya kuchunguza uthibitisho unaotegemea mabaki hayo, mwanabiolojia Jonathan Wells aliandika: “Wazo la kwamba wanyama wamechimbuka kutoka katika chanzo kimoja huku wakibadilika ikitegemea mazingira si jambo hakika ambalo limethibitishwa kisayansi. Uchunguzi wa mabaki ya kale na wa mifumo midogo iliyo tata ya vitu hai unaonyesha kwamba hiyo si nadharia iliyothibitishwa kabisa.”

Mageuzi—Ni Jambo Hakika au Ni Hadithi?

Kwa nini wanamageuzi wengi mashuhuri wanasisitiza kuwa mageuzi makubwa ni hadithi? Baada ya kuchambua baadhi ya sababu alizotoa Richard Dawkins, Richard Lewontin, ambaye ni mwanamageuzi mwenye ushawishi mkubwa aliandika kwamba wanasayansi wengi wako tayari kukubali madai ya kisayansi ambayo hayapatani na akili “kwa sababu tayari tumeazimia kushikamana na nadharia fulani, nadharia ya kwamba vitu halisi ndivyo vitu pekee vya hakika na vitu vyote ulimwenguni, kutia ndani vitu hai vilitokea bila ya msaada wa nguvu fulani zinazozidi zile za asili.” Wanasayansi wengi hukataa hata uwezekano wa kuwa kuna Mbuni mwenye akili. Lewontin anasema, “sisi hatuwezi kamwe kukubali uwezekano wa kwamba kuna Mungu.”

Kuhusiana na hilo, jarida Scientific American lilimnukuu mwanasosholojia Rodney Stark aliyesema hivi: “Kwa zaidi ya miaka 200 kumekuwa na wazo la kwamba ikiwa unataka kuonekana kuwa mwanasayansi basi hupaswi kuruhusu dini ikupumbaze akili.” Aliongezea kusema kwamba katika vyuo vikuu vya utafiti, “wanadini hufyata midomo yao,” huku “wale ambao si wanadini wakiwabagua.” Kulingana na Stark, “mtu hupata thawabu kwa kutokuwa mwanadini miongoni mwa watu mashuhuri [yaani, wanasayansi].”

Ikiwa utakubali fundisho la mageuzi makubwa kuwa kweli, utalazimika kuamini kwamba wanasayansi, wanaoamini ya Mungu hayawezi kujulikana na wanaoamini hakuna Mungu, hawataruhusu maoni yao yaathiri kauli zao wanapofanya utafiti. Utalazimika kuamini mabadiliko ya chembe za urithi na uteuzi wa asili ulitokeza vitu vyote tata vyenye uhai, licha ya kwamba utafiti wa karne moja wa kuchunguza mabilioni ya vitu ambavyo chembe zake za urithi zimebadilika, umeonyesha hakuna hata spishi moja ambayo imegeuzwa na kutokeza kitu kipya. Lazima uamini kuwa viumbe vyote viligeuka polepole kutoka kwa kiumbe kimoja, licha ya kwamba mabaki ya kale ya wanyama na mimea inaonyesha aina kuu za mimea na wanyama zilitokea ghafula na hazikubadilika na kuwa aina nyingine, hata baada ya muda mrefu sana kupita. Je, unafikiri imani kama hiyo inategemea mambo hakika? Au, ni hadithi tu?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Wazalishaji wa mbwa wanaweza kuchagua mbwa watakaozalisha ili wazao wa mbwa hao wawe na miguu mifupi au manyoya marefu kuliko wazazi wao. Hata hivyo, mabadiliko katika mbwa wanaozaliwa mara nyingi hutokana na kasoro katika utendaji wa chembe. Kwa mfano, mbwa anayeitwa dachshund ana umbo dogo kwa sababu tishu zake hazisitawi kwa njia ya kawaida, na hilo humfanya awe mfupi mno.

^ fu. 4 Ijapokuwa neno “spishi” limetumiwa mara nyingi katika makala hii, neno hilo halimo katika Biblia, kwani Biblia inatumia neno “aina” ambalo lina maana pana. Kwa kawaida, kile ambacho wanasayansi hurejelea kuwa badiliko katika spishi ni tofauti zilizopo katika “aina” fulani ya viumbe katika Biblia.

^ fu. 6 Ona sanduku “Kuainishwa kwa Viumbe.”

^ fu. 11 Utafiti unaonyesha kwamba sitoplazimu, tando, na maumbo ya chembe hutimiza fungu muhimu katika sura na utendaji wa kiumbe.

^ fu. 13 Maelezo ya Lönnig katika makala hii ni yake binafsi wala si ya Taasisi ya Max Planck ya Utafiti wa Kuzalisha Mimea.

^ fu. 14 Katika majaribio mengi ya kubadili chembe za urithi, idadi ya viumbe wapya ilizidi kupungua huku aina zilezile za mimea na wanyama zikitokezwa. Hilo lilimfanya Lönnig aanzishe “sheria ya mabadiliko yanayojirudia-rudia.” Isitoshe, chini ya asilimia 1 ya mimea iliyotokezwa kwa kubadili chembe za urithi ilitumiwa katika uchunguzi zaidi, na chini ya asilimia 1 ya mimea hiyo ndiyo ilifaa kwa matumizi ya kibiashara. Matokeo ya utafiti uliohusisha wanyama yalikuwa mabaya sana kuliko yale ya mimea hivi kwamba majaribio hayo yakasimamishwa.

 

[Blabu katika ukurasa wa 15]

“Mabadiliko ya chembe za urithi hayawezi kubadili spishi za awali [za wanyama na mimea] na kutokeza spishi mpya kabisa”

[Blabu katika ukurasa wa 16]

Kauli bora tunayoweza kukata ni kwamba shorewanda wa Darwin wanaonyesha kuwa spishi fulani inaweza kubadilikana kulingana na hali ya hewa

[Blabu katika ukurasa wa 17]

Kulingana na mabaki ya kale ya wanyama, jamii zote kuu zilitokea wakati mmoja na hazijabadilika sana

[Chati katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KUAINISHWA KWA VIUMBE

Viumbe vimeainishwa katika vikundi mbalimbali kuanzia spishi, ambacho ndicho kikundi kidogo zaidi, hadi kikundi kikubwa zaidi kinachoitwa himaya. * Kwa mfano, ona jinsi wanadamu na nzi-tunda wanavyoainishwa hapa chini.

WANADAMU NZI-TUNDA

Spishi sapiens melanogaster

Jenasi Homo Drosofila

Jamii Hominidi Drosophilids

Oda Sokwe Diptera

Tabaka Mamalia Wadudu

Faila Kodata Arithropoda

Himaya Wanyama Wanyama

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 49 Taarifa: Mwanzo sura ya 1 inasema mimea na wanyama waliumbwa “kulingana na aina yake.” (Mwanzo 1:12, 21, 24, 25) Hata hivyo, neno “aina” katika Biblia halitumiwi kwa njia hususa na halipaswi kueleweka kuwa na maana sawa na neno “spishi” linalotumiwa katika sayansi.

[Hisani]

Chati hii imetolewa kwenye kitabu Icons of Evolution—Science or Myth? Why Much of What We Teach About Evolution Is Wrong, cha Jonathan Wells.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Nzi-tunda ambaye chembe zake za urithi zilibadilika (juu), bado ni nzi-tunda, ingawa ana kasoro

[Hisani]

© Dr. Jeremy Burgess/Photo Researchers, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Majaribio ya kubadili chembe za urithi za mimea yalionyesha tena na tena kwamba idadi ya mimea mipya ilipungua sana, huku aina ileile ya mimea iliyobadilika ikitokezwa (Mmea ambao chembe zake za urithi zimebadilishwa una maua makubwa zaidi)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

From a Photograph by Mrs. J. M. Cameron/ U.S. National Archives photo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Finch heads: © Dr. Jeremy Burgess/ Photo Researchers, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Dinosaur: © Pat Canova/Index Stock Imagery; fossils: GOH CHAI HIN/AFP/Getty Images