Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Bustani ya Kitamaduni Yenye Umaridadi wa Pekee

Bustani ya Kitamaduni Yenye Umaridadi wa Pekee

Bustani ya Kitamaduni Yenye Umaridadi wa Pekee

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI GUADELOUPE

WALIISHI mahali maridadi lakini hawangeweza kufurahia uzuri huo. Kuanzia karne ya 17 na kuendelea, hiyo ndiyo iliyokuwa hali ya maelfu ya Waafrika waliotekwa nyara kutoka nchini mwao na kupelekwa Guadeloupe na Martinique. Wangetumikishwa kwenye mashamba ya miwa katika visiwa hivi vya Karibea muda wote wa maisha yao.

Wamiliki wa mashamba katika visiwa hivyo hawakuwaandalia watumwa hao chakula, kwa hiyo iliwabidi wapande vyakula vyao. Hata ingawa tayari walikuwa na kazi nyingi ya kufanya, walifaulu kukuza vyakula walivyopenda. Walikuza mihogo, viazi vikuu, na vyakula vingine ambavyo vilikuwa na lishe na ladha nzuri zaidi kuliko vyakula ambavyo mabwana wao wangewapa. Pia walikuza mitishamba na vilevile viungo vya kupikia.

Mnamo 1848, serikali ya Ufaransa ilipiga marufuku utumwa katika visiwa hivyo, lakini raia waliokuwa wamewekwa huru, waliendelea kukuza vyakula vyao. Leo watu wanaoishi Guadeloupe na Martinique ambao wengi wao ni wazao wa Waafrika hao waliofanya kazi kwa bidii, wanaendelea kulimia yale yanayoitwa mashamba ya Krioli.

Msitu Mdogo wa Mvua

Watumwa walikuwa na aina mbili za bustani. Kwa kawaida, kulikuwa na bustani ya mboga ambayo ilikuwa mbali kidogo na nyumba. “Bustani ya nyumbani,” (au jardin de case, kama inavyojulikana na wenyeji) ilipandwa karibu na nyumba, na hivyo ndivyo bustani za kienyeji za Krioli zilivyo leo. Bustani kama hiyo ina maua, nyasi, miti, na vichaka vingi vilivyoshikana kama vichaka vya msitu wa mvua. Kwa kuwa kuna mimea kila mahali, huenda ukafikiri mimea hiyo maridadi imekua ovyoovyo. Lakini bustani hiyo imepangwa vizuri na kugawanywa katika visehemu. Vijia vyembamba humruhusu mkulima kukaribia mimea yake yote.

Bustani hiyo inaanzia nyuma hadi mbele ya nyumba, nayo huwa mahali maridadi pa kupokea wageni. Wageni wanapofika, familia huwakaribisha hapo katikati ya maua mbalimbali yenye majani na rangi nyangavu inayopendeza.

Mitishamba hukua katika sehemu nyingine za bustani ya Krioli, mara nyingi kwenye sehemu zenye kivuli cha nyumba. Mrehani, mdalasini, jani la loreli, na mitishamba mingine, hutumiwa kama dawa za kienyeji katika visiwa hivyo. Pia mmea unaoitwa lemon grass hukua katika bustani hiyo, na majani yake makavu yanapoteketezwa hutumiwa kufukuza mbu.

Wakazi wengi wa visiwa hivyo huthamini sana ujuzi wao wa mitishamba. Zamani, mtu alipokuwa mgonjwa au kujeruhiwa, daktari alikuwa mbali sana. Kwa hiyo, watu walijitibu kwa kutumia mitishamba ya bustani ya Krioli. Bado mitishamba hiyo inatumiwa, lakini ni hatari kujitibu. Mitishamba inapotumiwa kwa njia isiyofaa inaweza kumfanya mtu awe mgonjwa zaidi badala ya kumtibu. Kwa hiyo, wakazi wa kisasa wa visiwa hivyo hupenda kutibiwa tu na madaktari wenye uzoefu.

Sehemu kuu ya bustani ya Krioli, sehemu iliyo nyuma ya nyumba, hutumiwa kukuza chakula. Bustani hiyo ina viazi vikuu, biringani, mahindi, spleen amaranth, letusi, na mazao mengine, pamoja na viungo ambavyo hutumiwa kutayarisha vyakula hivyo. Huenda migomba ikakua hapo, na unaweza kuona miti kama vile mishelisheli, miparachichi, mipera, au miembe.

Kutembea Kwenye Bustani Hiyo

Unapotembea nje ya bustani ya Krioli, huenda umaridadi wake ukafanya utake kusongea karibu. Unapoingia ndani, utafurahi kutazama maua na majani yaliyojipanga vizuri na kutokeza rangi nyangavu yanapopigwa na jua. Upepo mwanana unapovuma, utahisi harufu zenye kupendeza kuliko marashi. Naam, unavutiwa na bustani hiyo, hata ingawa umeitembelea tu. Wazia shangwe ya mwenye nyumba aliyepanda bustani hiyo na ambaye hutumia muda katika bustani hiyo kila siku!

Je, bustani za Krioli zitaendelea kuwapo? Wakazi fulani wa visiwa hivyo wanalalamika kwamba vijana hawapendezwi kudumisha utamaduni huo unaofaa na wenye kuvutia. Hata hivyo, vijana wengi kutia ndani wazee, wanathamini umaridadi wa bustani hizo na umaana wake wa kitamaduni. Kila bustani ya Krioli inatukumbusha jinsi ambavyo watumwa Waafrika walitokeza kitu maridadi na chenye faida licha ya hali zao zisizofaa.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

“KRIOLI” LINAMAANISHA NINI?

Hapo awali, neno “Krioli” lilirejelea watu kutoka Ulaya waliozaliwa Amerika, lakini sasa neno hilo lina maana nyingi. Wahaiti fulani hutumia neno “Krioli” kufafanua kitu chenye kuvutia sana au cha hali ya juu. Lugha fulani huko Jamaika, Haiti, na sehemu nyingine zinaitwa Krioli. Kwa kweli, krioli ni lugha inayotokana na lugha ya pijini lakini imekuwa lugha ya kienyeji ya watu fulani.

Pia neno “krioli” limetumiwa kufafanua mtindo fulani wa maisha, utamaduni wa wenyeji ambao umesitawi katika visiwa vingi vya Karibea. Nchini Puerto Riko na Jamhuri ya Dominika, neno la Kihispania criollo linalohusiana na hilo lina maana hiyo. Huko Karibea, katika muda wa karne nyingi, wazao wa wenyeji, Waafrika, na Wazungu wamechangamana na kuoana na kuzaa watoto warembo na tamaduni zenye kuvutia. Jina la bustani za Krioli za Guadeloupe na Martinique linatokana na tamaduni hizo.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Picha ndogo (kuanzia juu): “Alpinia,” mpilipili, mnanasi, mkakao, na mikahawa