Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Huko Marekani, “kila mwaka, mtu mmoja hivi kati ya wanne hupatwa na angalau ugonjwa fulani wa akili, na karibu mtu mmoja kati ya wawili hupatwa na ugonjwa huo wakati fulani maishani.”—SCIENCE NEWS, MAREKANI.

Mnamo Septemba 2004, Kimbunga Ivan kilitokeza mawimbi 24 hivi yenye kimo cha zaidi ya meta 15 katika Ghuba ya Mexico. Wimbi kubwa zaidi lilikuwa na kimo cha meta 27.7.—GAZETI SCIENCE, MAREKANI.

Kutumia simu za mkononi mtu anapoendesha gari huongeza mara nne uwezekano wa kusababisha aksidenti ambazo watu hulazimika kupelekwa hospitali, iwe dereva anazungumza akiwa ameishika simu hiyo mkononi au kupitia kikuza-sauti.—BMJ, UINGEREZA.

▪ Orodha mpya iliyochapishwa ili kuwasaidia watafsiri wa Biblia inaorodhesha lugha 6,912 ambazo bado zinatumika.—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.

▪ Licha ya kuonywa kwamba kuvuta sigara kunaweza kuwadhuru watoto wao, asilimia 30 ya wanawake nchini Poland huvuta sigara wakiwa wajawazito au wanaponyonyesha.—GAZETI ZDROWIE, POLAND.

Mtazamo Kuhusu Mali

Uchunguzi fulani uliofanywa na Taasisi ya Australia kuhusu mtazamo kuelekea mali umeonyesha kwamba ni milionea 1 tu kati ya 20 huko Australia hujiona kuwa amefanikiwa, linaripoti ABC News Online. Clive Hamilton, mkurugenzi mkuu wa Taasisi hiyo anasema kwamba “kadiri tunavyokuwa matajiri zaidi ndivyo tunavyokosa kuridhika na mapato yetu.” Ni asilimia 13 tu ya watu wenye mapato makubwa huridhika na maisha yao. Hamilton anasema: “Inashangaza kwamba jamii yetu hukimbizana na mafanikio ya kiuchumi kuliko kitu kingine chochote ingawa uthibitisho wote unaonyesha kwamba mambo mengine ndiyo huchangia furaha maishani.”

Takataka Zinazozunguka Angani

“Hebu wazia jinsi ambavyo watu wangekasirika iwapo madereva wangeacha magari yao barabarani baada ya kuishiwa na mafuta,” linasema gazeti New Scientist. Hali hiyo inafanana na setilaiti zilizoharibika ambazo zimeachwa angani. Takataka hizo zinazozunguka angani zinazidisha uwezekano wa kugongana na vyombo vipya vya angani. Inakadiriwa kwamba vyombo vipatavyo 1,120 vyenye upana wa sentimeta 60 viko juu ya ikweta mahali ambapo vyombo vingi vya mawasiliano huwa, lakini ni setilaiti zipatazo 300 tu zinazofanya kazi. Kati ya vyombo hatari ambavyo vimeachwa vikizunguka angani, kuna mitambo 32 ya nyuklia iliyoharibika.

Silaha na Vita

Vita Baridi vilipokoma, biashara ya silaha ilipungua. Hata hivyo, katika miaka michache iliyopita, biashara hiyo imesitawi. Kulingana na ripoti moja ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), mnamo 2004, gharama za kijeshi ulimwenguni pote zilifikia dola trilioni moja. Ikiwa pesa hizo zingegawanywa, kila mwanamume, mwanamke, na mtoto ulimwenguni angepata dola 162. Kulingana na Taasisi hiyo, mnamo mwaka wa 2004, kulikuwa na mapigano 19 ambayo kila moja lilisababisha zaidi ya vifo 1,000. Kati ya mapigano hayo, 16 yalikuwa yakiendelea kwa zaidi ya miaka kumi.

Magari Yanayotumia Aina Mbili za Mafuta

Gari moja jipya kati ya matatu yanayouzwa nchini Brazili hutumia aina mbili za mafuta, linaripoti gazeti Veja. Magari hayo hutumia petroli, alkoholi inayotokana na miwa, au mchanganyiko wa aina hizo mbili za mafuta. Kuanzia 2003 hadi 2004, uuzaji wa mafuta ya alkoholi uliongezeka kwa asilimia 34. Ongezeko hilo halitokani na watu kuhangaikia mazingira. Ni kwamba tu alkoholi ni bei rahisi zaidi kwa madereva wengi. Magari yanayotumia aina mbili za mafuta yanaweza kumfaidi “mwenye gari mafuta yanapopotea au bei inapobadilika-badilika,” anasema Rafael Schechtman, mkurugenzi wa Kituo cha Muundo-Msingi cha Brazili. “Bei ya alkoholi ikipanda, unaweza kutumia petroli, nayo petroli ikipanda, unaweza kutumia alkoholi.”