Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Alhambra—Kito cha Kiislamu cha Granada

Alhambra—Kito cha Kiislamu cha Granada

Alhambra—Kito cha Kiislamu cha Granada

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

“Ni hekaya na tamaduni ngapi, za kweli na za kubuniwa; ni nyimbo ngapi, za Kiarabu na Kihispania, za mapenzi na vita na mashujaa, zinazohusiana na majengo haya ya mashariki!”—WASHINGTON IRVING, MWANDISHI MMAREKANI WA KARNE YA 19.

ENEO maarufu ambalo lilichochea maneno hayo ni Alhambra, kasri la pekee ambalo hupamba jiji la Hispania linaloitwa Granada. Alhambra limejengwa kusini mwa Ulaya kwa muundo wa majengo ya Arabia au Uajemi. Ngome yake maridadi sana ilijengwa na Waarabu Waislamu, ambao uvutano wao mkubwa huko Hispania ulidumu kwa karne kadhaa. *

Mtawala Mwarabu anayeitwa Zawí ben Zirí alianzisha ufalme huru wa Granada katika karne ya 11. Ulidumu kwa miaka 500 hivi na wakati huo ulinawiri katika sanaa na utamaduni. Ulianza kufifia wakati watawala Wakatoliki Ferdinand na Isabella walipokomesha utawala wa Waislamu huko Hispania mnamo 1492.

Utawala wa Waarabu ulisitawi kabisa baada ya jiji la Córdoba kushindwa na majeshi ya Jumuiya ya Wakristo mnamo 1236. Granada likawa jiji kuu la Hispania ya Waislamu na watawala waliofuata wakajenga kasri kubwa, yaani, Alhambra, ambalo lilikuwa bora zaidi katika Ulaya yote. Mwandishi mmoja mwenye msisimko alilifafanua kuwa “jengo lenye kustaajabisha zaidi ulimwenguni pote.”

Alhambra limejengwa mahali penye kuvutia sana. Vilele vyenye theluji vyenye kimo cha zaidi ya meta 3,400 vya Milima ya Sierra Nevada huonekana nyuma yake. Kasri la Alhambra nalo limesimamishwa juu ya mlima mrefu wenye miti unaoitwa Sabika ambao uko meta 150 juu ya jiji. Kwa maoni ya mshairi wa karne ya 14, Ibn Zamrak, Mlima Sabika hutazama jiji la Granada kama mume anayemtazama mke wake.

Jiji Ndani ya Jiji

Jina Alhambra, linalomaanisha “nyekundu” katika Kiarabu, huenda linarejelea rangi ya matofali ambayo Waarabu walitumia kujenga kuta za nje. Hata hivyo, wengine hupenda zaidi maelezo ya wanahistoria Waarabu ambao wanasema kwamba ujenzi wa Alhambra ulifanywa chini ya “mwangaza wa tochi.” Wanasema kwamba mwangaza huo wa usiku ulifanya kuta ziwe na rangi nyekundu ambalo ndilo jina la jengo hilo.

Alhambra si kasri tu la kawaida. Linaweza kusemwa kuwa jiji ndani ya jiji la Granada. Nyuma ya kuta zake kuna bustani kadhaa, mabanda ya kustarehe, majengo ya kasri, Alcazaba (au, ngome), na hata medina ndogo, au mji. Mtindo wa ujenzi wa Waarabu wa Alhambra na madoido mengine ambayo yameongezwa baadaye yametokeza jengo lenye kuvutia linaloonyesha sanaa ya Waarabu kutia ndani mtindo Kipindi cha Mwamko wa Sanaa huko Ulaya.

Umaridadi wa Alhambra unatokana na mbinu iliyotumiwa na Waarabu na Wagiriki wa kale. Kwanza walichonga maumbo yaliyofanana, yenye ukubwa sawa, na rahisi kwenye mawe laini. Kisha wakapamba majengo yao maridadi. Kama mtaalamu mmoja anavyosema, “sikuzote Waarabu walizingatia kile ambacho wachoraji wa ramani za ujenzi wanachosema kuwa kanuni ya kwanza ya uchoraji ramani, yaani, pamba kitu kilichojengwa wala usijenge kitu kilichopambwa.”

Kuzuru Alhambra

Mtu huingia Alhambra kupitia lango linalofanana na kiatu cha farasi ambalo linaitwa Mlango wa Haki. Jina hilo linamkumbusha mtu mahakama iliyokutana hapo wakati wa utawala wa Waislamu ili kusikiliza haraka malalamishi madogo. Lilikuwa jambo la kawaida kutoa hukumu kwenye lango la jiji kotekote katika Mashariki ya Kati na jambo hilo hata linatajwa katika Biblia. *

Mapambo maridadi, ambayo mara nyingi hupatikana katika kasri za Waarabu kama vile Alhambra, yametengenezwa kwa chokaa. Wasanii walichonga chokaa hiyo katika maumbo ya nyuzi zilizosukwa vizuri na kuyarudia tena na tena. Matao mengine yenye mapambo huonekana kama vitu vilivyoning’inia vilivyojipanga kwa upatano kamili. Jambo jingine kuhusu kasri hilo ni zillij, yaani, vigae vilivyopakwa rangi, kuchomwa na kukatwa kisha vikapangwa katika maumbo mbalimbali. Vigae hivyo vimepangwa kwenye kuta za chini zikiwa na rangi nyangavu, ambazo hupatana vizuri na rangi za chokaa iliyo juu yake.

Ua wa Simba ndio maridadi zaidi kati ya nyua za Alhambra, nao umefafanuliwa kuwa “mfano bora zaidi wa sanaa ya Waarabu huko Hispania.” Kitabu kimoja kuhusu Alhambra kinaeleza: “Kuna jambo fulani kuhusu sanaa halisi ambacho hakiwezi kuigwa wala kubuniwa tena. . . . Hivyo ndivyo sisi huhisi tunaposimama mbele za ua huu ulioko Granada.” Vijia vyake vilivyofunikwa vizuri vyenye matao yaliyotoshana yenye nguzo nyembamba huzunguka chemchemi iliyosimamishwa juu ya simba 12 wa marumaru. Hiyo ndiyo sehemu inayopigwa picha nyingi zaidi nchini Hispania.

Bustani za Kuburudisha Roho

Pia Alhambra ina bustani, chemchemi, na vidimbwi vyenye kupendeza. * Enrique Sordo anasema hivi katika kitabu chake Moorish Spain: “Bustani ya Kiarabu ni mwonjo wa paradiso.” Uvutano wa Uislamu huonekana kila mahali. Mwandishi Mhispania García Gómez alisema: “Paradiso ya Kiislamu imefafanuliwa vizuri katika Kurani kuwa bustani ya fahari . . . inayonyweshwa na vijito vyenye kupendeza.” Katika Alhambra maji hutumiwa sana, jambo ambalo si la kawaida kwa watu waliozoea halihewa ya jangwani. Watu waliobuni bustani hizo walitambua kwamba maji yanapotiririka yanapunguza joto hewani na yanatoa sauti nzuri yenye kutuliza. Vidimbwi vya maji vyenye umbo la mstatili ambavyo humulikwa na anga jangavu la Hispania hufanya sehemu hiyo ionekane kuwa kubwa na safi.

Karibu tu na Alhambra kuna Generalife ambayo ni nyumba kubwa ya Waarabu iliyo na bustani kubwa. Iko mahali palipojificha kwenye Mlima Cerro del Sol ulio kando ya Sabika. Generalife ni mfano mzuri wa jinsi ambavyo Waarabu hutengeneza bustani zao, nayo imetajwa kuwa “mojawapo ya bustani maridadi zaidi ulimwenguni.” * Hapo awali daraja liliunganisha Generalife na Alhambra, na inaonekana kwamba watawala wa Granada walienda huko kupumzika. Ua fulani huongoza kwenye Ngazi ya Maji. Hapo wageni wanaweza kuvutiwa na nuru, rangi, na harufu nyingi mbalimbali.

Sikitiko la Mwarabu

Mfalme wa mwisho wa Granada, Boabdil (Muḥammad XI), aliposalimisha jiji hilo kwa Ferdinand na Isabella, yeye na familia yake walilazimika kwenda uhamishoni. Baada ya kutoka jijini, inasemekana kwamba walisimama katika sehemu fulani ya juu inayoitwa sasa El Suspiro del Moro (Sikitiko la Mwarabu). Walipotazama nyuma ili kuona kwa mara ya mwisho kasri lao tukufu jekundu, inasemekana kwamba mama yake Boabdil alimwambia hivi mwanawe: “Lia kama mwanamke kwa ajili ya kile ulichoshindwa kulinda kama mwanamume!”

Siku hizi, bado wageni zaidi ya milioni tatu ambao huzuru Alhambra kila mwaka hutembelea sehemu hiyo pia. Wakiwa hapo, kama tu Boabdil, wanaweza kuona jiji la Granada lililoenea chini ya kasri lake la Waarabu, linaloonekana kama kito katika taji. Ukitembelea Granada siku moja, huenda wewe pia ukaelewa huzuni aliyokuwa nayo mfalme wake wa mwisho Mwarabu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Mnamo 711 W.K., majeshi ya Waarabu yaliingia Hispania, na kwa miaka saba sehemu kubwa ya peninsula hiyo ikawa chini ya utawala wa Waislamu. Katika muda wa karne mbili, jiji la Córdoba likawa jiji kubwa na huenda lilikuwa ndilo jiji lenye watu wenye elimu na ustaarabu zaidi Ulaya.

^ fu. 13 Kwa mfano, Mungu alimwagiza Musa: ‘Weka waamuzi na maofisa kwa ajili yako ndani ya malango yote . . . , nao watawahukumu watu kwa hukumu ya uadilifu.’—Kumbukumbu la Torati 16:18.

^ fu. 17 Waarabu walianza kutengeneza bustani zao kama Waajemi na Wabizantiamu katika eneo lote la Mediterania kutia ndani Hispania.

^ fu. 18 Neno hili linatokana na neno la Kiarabu “Jennat-al-Arif,” ambalo nyakati nyingine hutafsiriwa kuwa “bustani za juu,” ingawa inaelekea zaidi kuwa neno hilo humaanisha “bustani ya mchora-ramani.”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Alcazaba

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ua la Simba

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Bustani za Generalife

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ngazi ya Maji

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Line art: EclectiCollections

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

All except top photo: Recinto Monumental de la Alhambra y Generalife

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

All photos: Recinto Monumental de la Alhambra y Generalife

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Above photos: Recinto Monumental de la Alhambra y Generalife; bottom photo: J. A. Fernández/San Marcos