Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chembe Nyekundu za Damu Zenye Kustaajabisha

Chembe Nyekundu za Damu Zenye Kustaajabisha

Chembe Nyekundu za Damu Zenye Kustaajabisha

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

Chembe inayopatikana kwa wingi katika mfumo wako wa damu hufanya damu iwe nyekundu na hivyo inaitwa chembe nyekundu ya damu. Tone moja tu la damu yako lina mamia ya mamilioni ya chembe hizo. Zinapotazamwa kwenye darubini, chembe hizo huwa na umbo la mviringo, ni tambarare, na zimebonyea katikati. Kila chembe ina mamia ya mamilioni ya molekuli za himoglobini. Kwa upande mwingine, kila molekuli ya himoglobini ina umbo maridadi la duara linalofanyizwa na atomu 10,000 hivi za hidrojeni, kaboni, nitrojeni, oksijeni, na salfa, na pia ina atomu nne nzito zaidi za chuma ambazo huwezesha damu kubeba oksijeni. Himoglobini husaidia kusafirisha kaboni-dioksidi kutoka kwenye tishu hadi kwenye mapafu ambako itaondolewa mwilini.

Sehemu nyingine muhimu ya chembe zako nyekundu za damu ni utando wake. Sehemu hiyo ya nje ya ajabu huwezesha chembe zinyumbulike na kuwa nyembamba ili ziweze kujipenyeza kwenye mishipa midogo zaidi ya damu na hivyo kuwezesha sehemu zote za mwili wako kuendelea kutenda.

Chembe nyekundu za damu hutengenezwa katika uboho wa mfupa. Chembe mpya inapoingia katika mfumo wako wa damu, inaweza kuzunguka kutoka katika moyo hadi kwenye mwili wako zaidi ya mara 100,000. Tofauti na chembe nyingine, chembe nyekundu za damu hazina kiini. Hilo hufanya ziwe na nafasi kubwa zaidi ya kubeba oksijeni na kuzifanya ziwe nyepesi zaidi, na hilo husaidia moyo wako kusukuma mabilioni mengi sana ya chembe nyekundu za damu katika sehemu zote za mwili wako. Hata hivyo, kwa kuwa hazina kiini, haziwezi kutengeneza upya sehemu zake za ndani. Kwa hiyo, baada ya siku 120 hivi, chembe zako nyekundu za damu huanza kuharibika na kupoteza uwezo wa kunyumbulika. Chembe kubwa nyeupe za damu zinazoitwa fagositi humeza chembe hizo zilizoharibika na kutokeza atomu za chuma. Atomu hizo za chuma hujishikilia kwenye molekuli za kusafirisha vitu na hupelekwa kwenye uboho wa mifupa ili zitumike kutengeneza chembe mpya nyekundu za damu. Kila sekunde, uboho wa mifupa yako humwaga chembe mpya milioni mbili hadi milioni tatu kwenye mfumo wako wa damu!

Ikiwa chembe nyekundu za damu zingeacha kutenda, ungekufa baada ya dakika chache. Tunapaswa kumshukuru sana Yehova Mungu kwa sehemu hiyo muhimu ya uumbaji, ambayo hutuwezesha kuwa hai na kufurahia maisha. Bila shaka unakubaliana na maneno haya ya mtunga-zaburi aliyesema: “Ee Yehova, umenichunguza kabisa, nawe unanijua. Nitakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa njia ya ajabu yenye kuogopesha. Kazi zako ni za ajabu, kama vile nafsi yangu inavyojua vema.”—Zaburi 139:1, 14.

[Mchoro katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Chembe nyekundu ya damu

Utando

Himoglobini (imeongezwa ukubwa)

Oksijeni