Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Historia Fupi ya Zambarau

Historia Fupi ya Zambarau

Historia Fupi ya Zambarau

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

“Na wewe, Ee mwana wa binadamu, mfanyie Tiro wimbo wa huzuni . . . Mtando wako wa nguo ulikuwa kitani cha rangi mbalimbali kutoka Misri, ili kuwa tanga yako. Uzi wa bluu na sufu iliyotiwa rangi ya zambarau kutoka katika visiwa vya Elisha ndivyo vilivyofunika sitaha yako. . . . Walikuwa wafanya-biashara wako katika mavazi ya fahari.”—Ezekieli 27:2, 7, 24.

TIRO lilikuwa bandari kuu ya Foinike la kale, katika eneo ambalo sasa linaitwa Lebanoni. Jiji hilo lililokuwa likimkaidi Yehova lilikuwa na biashara yenye ufanisi ya vitambaa vya zambarau. Kwa kweli, katika Milki ya Roma, rangi hiyo nyangavu iliitwa zambarau ya Tiro.

Kwa sababu ya bei yake ya juu, rangi ya zambarau ilihusianishwa na wafalme, waheshimiwa, na matajiri. * Kwa kweli, kulingana na sheria za Roma ya kale, mtu wa “kawaida” ambaye angeamua kuvaa nguo iliyotiwa rangi bora ya zambarau angeshtakiwa kwa kosa baya la uhaini.

Zamani na hata sasa, rangi hii hupatikana kwa kiasi kidogo kutoka kwenye konokono wa baharini, konokono mmoja hutoa tone moja. Watiro walitumia konokono wa jamii ya murex, hasa wanaoitwa brandaris na trunculus, ambao hupatikana katika maeneo mbalimbali kando ya Pwani ya Mediterania. Rangi mbalimbali zingeweza kupatikana, ikitegemea mahali hususa ambapo konokono hao walipatikana.

Kufuatia Historia Yake Huko Mexico

Karne nyingi zilizopita wakati washindi Wahispania huko Amerika Kusini walipoonyeshwa vitambaa vilivyotiwa rangi ya zambarau, walivutiwa kuona jinsi ambavyo rangi hiyo haichujuki. Walisema kwamba vitambaa hivyo vilipofuliwa, rangi hiyo ilionekana kuwa bora zaidi. Uthibitisho wa akiolojia unadokeza kwamba wenyeji walivaa mavazi mbalimbali yaliyotiwa rangi ya zambarau.

Wenyeji wa Mexico, hasa watu wa kabila la Mixtec, walitia nguo zao rangi iliyotokana na umajimaji wa konokono aliyeitwa Purpura patula pansa, ambaye ni wa jamii ileile na konokono aliyetumiwa na Watiro. Aina hizo mbili za konokono hutoa umajimaji fulani ambao mwanzoni huonekana kuwa wa rangi hafifu lakini huwa wa zambarau unapopigwa na hewa na nuru. Rangi hiyo hukolea kwenye nguo bila kutiwa kemikali ya pekee inayosaidia rangi isichujuke.

Watu wa kabila la Mixtec waliokota konokono anayeitwa Purpura katika Bahari ya Pasifiki. Ingawa Watiro na Waroma waliua moluska, na hata rundo la makombe matupu la wakati huo limepatikana, watu wa kabila la Mixtec “walikamua” tu konokono hao. Kupuliza moluska kulifanya atoe umajimaji wake wenye thamani, ambao ulitiwa mara moja kwenye nyuzinyuzi, kisha kiumbe huyo akarudishwa baharini. Wenyeji “hawakukamua” konokono hao wakati wa kuzaana. Kwa sababu hiyo, konokono hao wangalipo hadi leo.

Kulingana na tume ya National Commission for the Knowledge and Use of Biodiversity, hadi mwaka wa 1980, watu wa kabila la Mixtec waliotia vitambaa rangi walisafiri kilometa 200 hadi kwenye ghuba ya Huatulco, kuanzia Oktoba hadi Machi, ili kupata rangi ya zambarau. Hata hivyo, desturi hiyo ambayo haingetokeza madhara yoyote kwa mazingira ilivurugwa kuanzia mwaka wa 1981 hadi 1985, wakati shirika fulani la kigeni lilipoanza kutumia bidhaa hiyo. Kwa sababu hiyo, idadi ya konokono wanaoitwa Purpura ilipungua. Hilo lilichochea kuanzishwa kwa mkataba rasmi unaokataza kuuawa kwa konokono huyo na kuruhusu atumiwe kama zamani, na wenyeji peke yao.

Bado konokono wanaoitwa Purpura wanakabiliwa na hatari kutokana na ongezeko la watalii katika ghuba wanakoishi. Hata hivyo, watu wengi wanatumaini kwamba kiumbe huyo mwenye kuvutia atahifadhiwa na kuendelea kutoa rangi yake maridadi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Rangi ya zambarau, ambayo hasa ni mchanganyiko wa bluu na nyekundu, inatia ndani rangi mbalimbali zinazokaribiana na zambarau kama vile rangi ya urujuani na nyekundu. Zamani neno “zambarau” lilitumiwa pia kwa rangi nyekundu iliyokolea.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Konokono anayeitwa “Purpura”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Konokono huyu “hukamuliwa” kisha hurudishwa baharini

[Hisani]

© FULVIO ECCARDI

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Uzi wa zambarau ulio tayari kufumwa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kufuma “posahuanco” (sketi)