Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Urafiki Huchangia Hali Bora ya Moyo

Gazeti Diario Médico la Hispania linasema hivi: “Kuwa na marafiki na uhusiano mzuri pamoja na familia hupunguza hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo au kiharusi.” Kwa muda mrefu, madaktari wamefikiri kwamba kiasi cha kolesteroli katika damu, shinikizo la damu, na unene ndio mambo ambayo huathiri moyo zaidi. Lakini uchunguzi wa hivi karibuni ambao ulihusisha wanawake 500 hivi waliokuwa na maumivu ya kifua, ulionyesha kwamba idadi ya watu wa familia na marafiki ambao mgonjwa ana uhusiano wa karibu pamoja nao inapaswa kuzingatiwa pia. Uchunguzi huo mpya ulifunua kwamba “hatari ya kufa mapema kwa wanawake walio na uhusiano mbaya na wengine ilikuwa mara mbili zaidi ikilinganishwa na wale ambao wana uhusiano mzuri na wengine.” Carl J. Pepine, mmoja kati ya wale walioanzisha uchunguzi huo, anaongeza kwamba ‘mtu akiwa na rafiki mmoja au wawili wa karibu, hatari ya kupatwa na kiharusi au mshtuko wa moyo inapungua.’

Sifongo wa Ajabu

Hivi karibuni, watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Stuttgart, Ujerumani, walivumbua sifongo mweupe mwenye umbo la duara aliye na uwezo wa ajabu, lasema gazeti la Ujerumani Die Welt. Sifongo huyo ni mdogo sana lakini anaweza kujirusha umbali wa sentimeta kadhaa kwa siku, na hilo humfanya kuwa sifongo mwenye kasi zaidi kuwahi kuvumbuliwa. Anapojikunyata na kujitanua kwa utaratibu, mnyama huyo hutoa maji mwilini, na anaweza kupunguza ukubwa wake kwa asilimia 70. Yeye hufyonza maji ili kuingiza chakula na oksijeni mwilini mwake. Watafiti walivumbua kwamba mnyama huyo hujikunyata na kujitanua kwa nguvu zaidi wakati viumbe wengine wadogo wanapowekwa karibu naye. Mtafiti Michael Nickel anasema, “Hili ni jambo la ajabu sana” kwa kuwa sifongo “hana mfumo wa neva.” Sifongo hujisogezaje au hutambuaje kwamba kuna viumbe wengine karibu naye hali hana mfumo wa neva? Watafiti wanamchunguza sifongo kwa makini sana wakitumaini kutambua jinsi anavyofanya mambo hayo.

Uduvi wa Antaktika Wanapungua

Kulingana na gazeti Guardian la London, David Adam anasema kwamba uduvi ambao ni viumbe wadogo sana wa baharini na chakula muhimu cha viumbe fulani wa majini, wamepungua kwa asilimia 80 huko Antaktika tangu miaka ya 1970. Uduvi hula miani ambayo hupatikana chini ya barafu iliyoko baharini. Lakini tangu miaka ya 1950, kiwango cha joto karibu na Antaktika kimepanda kwa nyuzi 2.5 Selsiasi na kuyeyusha kiasi fulani cha barafu hiyo. Angus Atkinson, wa Shirika la Uingereza la Wachunguzi wa Antaktika, anasema: “Hatuelewi vizuri jinsi kuyeyuka kwa barafu kunavyohusiana na kuongezeka kwa joto, lakini tunaamini kwamba upungufu wa uduvi umesababishwa na kuyeyuka kwa barafu hiyo.” Watafiti wa shirika hilo walichunguza rekodi za kisayansi za uvuvi za nchi tisa zilizovua samaki huko Antaktika kuanzia mwaka wa 1926 hadi 1939, na kuanzia 1976 hadi 2003. Wanasema kwamba idadi ya uduvi wanaopatikana leo katika eneo la Antaktika ni asilimia 20 hivi ya idadi ya uduvi waliopatikana huko miaka 30 iliyopita.

Kuzungumza kwa Kupiga Mbinja

Wachungaji wa La Gomera katika Visiwa vya Canary huongea Kisilbo ambacho huzungumzwa kwa kupiga mbinja. Kwa kutumia mfumo wa sauti wenye vokali mbili na konsonanti nne ili kupiga mbinja zenye sauti tofauti-tofauti, wachungaji hao wanaweza kuwasiliana wakiwa mbali sana. Hivi karibuni, watafiti walitumia mashine inayopima jinsi ubongo unavyofanya kazi ili kulinganisha utendaji wa ubongo kati ya Wahispania watano wanaozungumza Kihispania na wachungaji watano wanaozungumza Kihispania na Kisilbo. Kulingana na gazeti la Hispania, El País, watafiti hao waligundua kwamba wachungaji hao wanapowasiliana, iwe ni kwa kupiga mbinja au kwa kuongea, “ubongo wao hutoa ishara zilezile.” Gazeti hilo linamnukuu mtafiti mmoja aliyesema: “Uchunguzi wetu umetoa uthibitisho zaidi kwamba mwanadamu ana uwezo mkubwa wa kujifunza lugha za aina mbalimbali.”

Gharama Inayopanda ya Kutafsiri

Mnamo Mei 2004 idadi ya nchi katika Muungano wa Ulaya iliongezeka hadi 25 baada ya nchi kumi nyingine kujiunga na Muungano huo. Hata hivyo, ongezeko hilo limesababisha matatizo ya lugha ambayo yamefanya gharama zipande. Lugha 20 zinazotumiwa katika nchi hizo 25 zinaonwa kuwa rasmi. Kwa hiyo, ni lazima hati zitafsiriwe katika kila lugha. Gazeti la Ufaransa Valeurs Actuelles linasema: “Kabla ya ongezeko hilo, Tume ya Ulaya ilitafsiri [habari] zilizojaza kurasa 1,416,817 katika mwaka wa 2003.” Hata hivyo, idadi ya kurasa za habari zitakazotafsiriwa zitaongezeka haraka. Kwa kuwa kuna lugha tisa mpya, uhitaji wa kutafsiri habari kutoka lugha moja hadi nyingine (kwa mfano, Kimalta hadi Kifini, au Kiestonia hadi Kigiriki) umeongezeka mara tatu hivi. Imekuwa vigumu kupata watafsiri na wafasiri stadi. Robert Rowe wa idara ya utafsiri ya Tume ya Ulaya anasema gharama za kutafsiri ambazo sasa ni dola milioni 670 za Marekani “zinatarajiwa kupanda sana na zinaweza kufikia dola milioni 990.”

Moshi Wenye Kudhuru

Gazeti The Sydney Morning Herald linasema kwamba chembe za moshi wa mishumaa na ubani huenda zikahatarisha afya ya makasisi na waumini wanaokaa muda mrefu katika makanisa yasiyo na hewa ya kutosha. Uchunguzi fulani ulionyesha kwamba katika makanisa mawili, viwango vya chembe za moshi vilikuwa “mara 20 zaidi ya viwango vinavyoonwa kuwa salama kulingana na viwango vya uchafuzi wa hewa vya Ulaya,” linasema gazeti hilo. Ripoti hiyo ilisema kwamba viwango hivyo ni sawa na vile “vinavyopatikana katika hewa karibu na barabara ambazo hutumiwa na magari 45,000 kwa siku.” Mmoja wa wale walioanzisha uchunguzi huo anasema kwamba watu wanaovuta kwa ukawaida hewa hiyo iliyochafuliwa wanakabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kansa au magonjwa ya mapafu.

Nguzo ya Ukumbusho kwa Wanyama Waliotumika Vitani

Gazeti The Times linasema kwamba “nguzo ya kitaifa kwa wanyama waliotumika, wakateseka, na kufa pamoja na wanajeshi wa Uingereza na wale wa Muungano kwenye vita na mapambano ya karne zilizopita,” imezinduliwa katikati ya London. Nguzo hiyo ina sanamu ya farasi wa shaba, mbwa, na nyumbu wawili wanaobeba mizigo, ambao wanazungukwa na ukuta wa mawe wenye michongo ya wanyama wengine waliotumika katika vita mbalimbali. Kwa mfano katika Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, farasi milioni nane hivi, na pia punda na nyumbu wasio na hesabu, walikufa. Gazeti Guardian linasema kwamba wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu askari walitumia vimulimuli kusoma ramani usiku. Mbwa wa pekee aliyeitwa Rob alishuka kwa parachuti zaidi ya mara 20 huko Afrika Kaskazini na Italia. Isitoshe, wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, njiwa aliyeitwa Cher Ami “alipeleka ujumbe mara 12 hivi na hakukosa kamwe kufikisha ujumbe,” linasema gazeti The Times. Hata hivyo, kulingana na chanzo kimoja inakadiriwa kwamba njiwa 20,000 walikufa katika vita hivyo.