Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Tukutane Kisimani”

“Tukutane Kisimani”

“Tukutane Kisimani”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MOLDOVA

BIBI-ARUSI anatazama kwa wasiwasi maji yanapochotwa kisimani na kumwagwa barabarani. Anacheka kwa shangwe bwana-arusi anapomwinua na kumbeba kuvuka sehemu hiyo yenye maji. Marafiki na watu wa familia wanakusanyika kuwatazama wanapofanya desturi hiyo ambayo imekuwapo kwa muda mrefu huku wakipiga vigelegele. Desturi hiyo ya arusi isiyo ya kawaida inaonyesha wazi kwamba huko Moldova, kuna mambo mengi zaidi ambayo hutendeka kisimani mbali na kuchota maji.

Moldova, ambayo iko kusini-mashariki mwa Ulaya, imepakana na Ukrainia upande wa kaskazini, mashariki, na kusini na kupakana na Rumania upande wa magharibi. Ina ukubwa wa kilometa 34,000 za mraba.

Ingawa kuna karibu mito 3,100 nchini Moldova, mara nyingi ukame huzuia mito hiyo isitosheleze mahitaji ya wakazi wake 4,300,000. Ili kukabiliana na upungufu huo, zaidi ya asilimia 20 ya maji ya taifa lote hutoka kwenye visima. Inakadiriwa kwamba kuna kati ya visima 100,000 na 200,000 katika bonde la Prut huko Moldova!

Ili kutosheleza kiu ya wasafiri waliochoka, visima vyenye vibanda vilivyo na mapambo hupatikana kotekote kwenye barabara kubwa na ndogo za Moldova. Katika vijiji vingi vya mashambani, marafiki hukutana pia kwenye kisima na kuzungumzia matukio ya siku.

Mila za Kuheshimu Maji

Nchini Moldova, maji ya kisima huheshimiwa katika njia kadhaa. Kwa mfano, vyoo hujengwa umbali unaofaa kutoka kwenye kisima cha familia, na ili kulinda usafi wa kisima zaidi, kuna sheria dhidi ya kumwaga maji ya ziada ndani ya kisima. Mtu akichota maji mengi kuliko anavyohitaji, maji ya ziada humwagwa chini au hutiwa katika chombo fulani karibu na kisima. Isitoshe, inaonwa kuwa tabia mbaya kutema mate karibu na kisima. Hata mila za huko haziruhusu watu kubishana karibu na kisima!

Visima huchangia roho ya ushirikiano nchini Moldova. Kuchimba kisima ni kazi ambayo hufanywa na jamii yote na huonwa kuwa muhimu kama tu kujenga nyumba mpya. Hilo huonekana katika msemo wa kienyeji, Mtu ambaye ameshindwa kujenga nyumba, kulea mwana, kuchimba kisima na kupanda mti amepoteza maisha yake. Wakati kisima kinapomalizwa, wote katika jamii ambao walishiriki kukichimba hualikwa kwa mlo mkubwa.

Kuharibiwa kwa Mazingira

Visima vingi huko Moldova hupata maji yake kutoka kwenye tabaka la maji lililo kati ya meta 5 hadi 12 chini ya ardhi. Tabaka jingine la maji liko kati ya meta 150 hadi 250 chini ya ardhi. Licha ya mambo ambayo yamefanywa ili kulinda maji, kiasi kikubwa cha maji ya Moldova ya chini ya ardhi yamechafuliwa na takataka kutoka viwandani na mbolea zenye kemikali. Kichapo cha mwaka wa 1996 cha Umoja wa Mataifa Republic of Moldova Human Development Report kilisema kwamba nitrati na bakteria inayoweza kusababisha magonjwa zilichafua “angalau asilimia 60 ya visima huko Moldova.” Hata hivyo katika miaka ya karibuni, maji ya kisima yamekuwa bora kwa sababu ya kupungua kwa vitu vinavyotokezwa viwandani na kupungua kwa kiasi cha kemikali na fueli zinazopenya katika tabaka la maji.

Ukitembelea Moldova, huhitaji kumwaga maji kwenye barabara ili uwe na mazungumzo ya kirafiki. Huenda hata ukapata habari za siku unapotosheleza kiu yako kwa kikombe cha maji baridi. Unachohitaji tu ni mwenyeji wa Moldova akualike mkutane kisimani.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26, 27]

KAZI YA KITAMADUNI

Oleg ni muuzaji wa vitu vya chuma, na amekuwa akitengeneza vifuniko vya kisima vyenye mapambo tangu alipomaliza shule. Oleg anasema hivi: “Ninafikiri kwamba kazi ya vyuma iko katika damu yetu. Mwanzoni mwa karne iliyopita, babu yangu alijifunza kutengeneza vitu vya chuma kutoka kwa mmoja wa Wayahudi ambao walitengeneza vitu hivyo na ambao waliishi katika jamii kubwa ya Wayahudi nje ya kijiji ambacho babu aliishi huko Lipcani. Baada ya mauaji yaliyotukia katika Vita vya Pili vya Ulimwengu, wafanyabiashara wachache waliobaki hawakuwa Wayahudi. Wakati huo ndio baba yangu alijifunza kazi hiyo na amenifundisha.”

Anapotengeneza maumbo yenye kutatanisha ambayo hupamba vifuniko vya kisima, Oleg hutumia vifaa vya hali ya chini na mifano kadhaa; utamaduni na fikira zake huongoza mikono yake. Ustadi wake huheshimiwa sana na wenyeji. Oleg anasema: “Wateja wengi hutaka niwauzie vitu vingine kwa bei ya chini zaidi, lakini ninapowatengenezea kifuniko cha kisima, kwa ukawaida wao hufurahia kulipa kiasi nilichoomba.”

[Ramani katika ukurasa wa 26, 27]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UKRAINIA

MOLDOVA

RUMANIA

Bahari Nyeusi