Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Barabara ya Giant’s Causeway

Barabara ya Giant’s Causeway

Barabara ya Giant’s Causeway

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI IRELAND

KULINGANA na hekaya ya watu wa Ireland, jitu moja la Ireland lililoitwa Finn MacCool lilitaka kupigana na jitu lingine la Scotland lililoitwa Benandonner. Hata hivyo, kulikuwa na tatizo fulani. Hakukuwa na mashua kubwa ambayo ingeweza kuvusha jitu moja hadi ng’ambo ile nyingine! Hekaya hiyo inasema kwamba Finn MacCool alitatua tatizo hilo kwa kujenga barabara juu ya bahari akitumia nguzo kubwa za mawe.

Benandonner alikubali kupigana na akasafiri kwa kutumia barabara hiyo hadi Ireland. Jitu hilo lilikuwa kubwa na lenye nguvu kuliko Finn MacCool. Mke wa Finn MacCool alipotambua jambo hilo, kwa werevu aliamua kumvisha mume wake kama mtoto. Benandonner alipowasili nyumbani kwao na kumwona “mtoto” huyo, aliogopa akiwazia kwamba, ikiwa mtoto alikuwa mkubwa jinsi hiyo basi hangetaka kupigana na baba yake! Alitoroka na kurudi Scotland! Ili kuhakikisha kwamba Finn MacCool hangeweza kumfuata, aliharibu barabara hiyo alipokuwa akivuka kuelekea ng’ambo ile nyingine. Nchini Ireland, kuna mabaki tu ya mawe ya barabara hiyo ya Giant’s Causeway.

Kwa zaidi ya miaka mia tatu, mamilioni ya watu wamesimuliwa hadithi hiyo yenye kuchekesha kuhusu jinsi barabara ya Giant’s Causeway ilivyojengwa. Lakini kwa kweli, barabara hiyo ilitokeaje, na kwa nini hilo huwavutia watalii? Tuliamua kuchunguza jambo hilo.

Barabara ya Giant’s Causeway!

Barabara ya Giant’s Causeway iko kwenye pwani ya kaskazini ya Ireland karibu kilometa 100 kaskazini-magharibi ya Belfast. Tulipowasili huko, tulitembea kidogo kutoka mahali pa kupokea wageni na kuelekea kwenye ufuo kisha tukapiga kona na kuelekea upande mmoja. Mbele yetu tuliona kitu chenye kushangaza—maelfu ya nguzo kubwa sana za mawe zilizosimama wima zenye kimo cha meta sita hivi. Watu fulani wamekadiria kwamba kuna nguzo zipatazo 40,000. Lakini si idadi hiyo iliyotustaajabisha. Tulishangazwa na jinsi ambavyo pande za nguzo hizo zinatoshana. Zote zina upana wa kati ya sentimeta 38 hadi 51, sehemu ya juu inaonekana kuwa tambarare, na kila moja inaonekana kuwa na pande sita. Nguzo hizo zinatoshana sana hivi kwamba unapozitazama kutoka juu, sehemu ya juu huungana kama sega la asali. Baadaye tuligundua kwamba karibu robo ya nguzo hizo zina pande tano na nyingine chache zina pande nne, saba, nane, na hata tisa.

Barabara hiyo ina sehemu tatu. Sehemu kubwa zaidi inayoitwa Grand Causeway, inaanzia pwani chini ya miamba. Mwanzoni, inaonekana kama mawe makubwa sana ya kukanyagia yaliyopangwa kiholela, mengine yakiwa na kimo cha meta sita hivi. Inapoelekea kwenye bahari, wazo la barabara ya majitu huja akilini kwa sababu sehemu za juu zinazoonekana kama sega la asali huanza kuwa tambarare. Barabara hiyo huwa kama barabara iliyojengwa kwa mawe ambayo ina upana wa kati ya meta 20 na 30. Maji ya bahari yalipopungua, tuliweza kutembea meta mia chache katika barabara hiyo kabla haijapotea chini ya mawimbi na kuonekana kana kwamba inaelekea Scotland.

Sehemu zile nyingine, yaani, Middle Causeway na Little Causeway, ziko kandokando ya Grand Causeway. Hizo huonekana kama marundo badala ya barabara. Sehemu zao za juu zilizo tambarare hufanya iwe rahisi kwa mgeni kutumia mikono na miguu kupanda kutoka rundo moja hadi lingine. Lazima mtu awe mwangalifu sana anapofanya hivyo, tuligundua kwamba nguzo zilizokuwa karibu na maji zilikuwa na unyevunyevu na ziliteleza sana!

Nguzo Nyingine Kubwa

Tuliendelea kutembea kwenye ufuo wenye urefu wa kilometa 6.5 hivi unaoitwa Causeway Headlands, na tukaona maelfu ya nguzo hizo kwenye miamba. Kwa miaka mingi, watu wamezipa baadhi ya nguzo hizo majina. Mbili kati yake zimepewa majina ya ala za muziki. Moja yake, inaitwa Organ (Kinanda), kwa sababu nguzo zake ndefu zinazolingana zinafanana na mifereji ya kinanda kikubwa. Ile nyingine, Giant’s Harp (Kinubi cha Jitu), ina nguzo kubwa zilizojipinda ambazo zinaelekea chini hadi kwenye ufuo.

Hekaya ya kwamba kulikuwa na majitu inaonekana katika majina mengine yaliyopewa nguzo hizo. Kwa mfano, kuna Giant’s Loom (Kitanda cha Kufuma cha Jitu), Giant’s Coffin (Jeneza la Jitu), na Giant’s Cannons (Mizinga ya Jitu), na pia Giant’s Eyes (Macho ya Jitu). Hata kuna Giant’s Boot (Kiatu cha Jitu)! Kwenye ufuo ulio mbali kidogo kutoka Giant’s Causeway, tuliona nguzo hiyo yenye umbo la kiatu. Ina kimo cha meta mbili hivi. Watu fulani wamekadiria kwamba jitu linalosemekana kuwa lilivaa “kiatu” hicho lilikuwa na kimo cha meta 16 hivi.

Nguzo nyingine zinazoitwa Chimney Tops (Vifuniko vya Dohani), humkumbusha mtu uhusiano kati ya barabara ya Giant’s Causeway na Manowari za Hispania zinazojulikana sana. Zikiwa zimetenganishwa na mwamba mkuu kwa sababu ya kumomonyolewa na kuvunjika-vunjika, nguzo hizo chache huonekana waziwazi kutoka kwenye rasi inayoelekeana na pwani ya Causeway. Ni rahisi kuona sababu ambayo ingeweza kuwafanya mabaharia waliozitazama kutoka baharini wadhani kuwa ni vifuniko vya dohani za kasri kubwa. Inasemekana kwamba baada ya Manowari za Hispania kushindwa mnamo 1588, meli moja ya kivita ya Hispania iliyoitwa Girona, iliyokuwa ikikimbia ilifyatulia nguzo hizo mizinga yake yote kwa sababu mabaharia wake walidhani kwamba ni kasri ya adui.

Mwisho Ule Mwingine wa Barabara ya Causeway

Inasemekana kwamba barabara ya Giant’s Causeway ilijengwa ili kuunganisha Ireland na Scotland. Basi mwisho ule mwingine uko wapi? Nguzo zinazofanana za mawe ya volkano zinapatikana kilometa 130 kaskazini-mashariki katika Kisiwa cha Staffa, kisiwa kidogo sana kisicho na watu kilichoko pwani ya magharibi ya Scotland. (Jina Staffa linamaanisha “Kisiwa cha Nguzo.”) Jina lingine la Benandonner, lile jitu la Scotland lililomtoroka Finn MacCool, lilikuwa Fingal. Pango kubwa la baharini ambalo huwavutia watu katika Kisiwa cha Staffa, lililofanyizwa ndani ya nguzo hizo za mawe ya volkano ambalo linaingia meta 80 hivi ndani ya mwamba lilipewa jina la jitu hilo, yaani, Fingal’s Cave (Pango la Fingal). Kuvuma kwa mawimbi juu ya pango hilo kulimchochea mtungaji Mjerumani, Felix Mendelssohn, atunge muziki wake wa “Hebrides,” ambao pia uliitwa “Fingal’s Cave,” katika mwaka wa 1832.

Nguzo Hizo Zilifanyizwaje?

Ikiwa nguzo hizo zenye pande zinazolingana hazikutengenezwa na majitu hayo yaliyokuwa yakipigana, basi zilitokeaje? Tulitambua kwamba ili kupata jibu kamili, tulihitaji kuelewa jinsi ambavyo miamba fulani hufanyizwa.

Ireland Kaskazini iko katika eneo lenye chokaa ngumu. Zamani, utendaji wa volkano katika tabaka la nje la dunia ulifanya miamba iliyoyeyuka, ambayo ilikuwa na joto linalozidi nyuzi 1,000 Selsiasi, ipenye kwenye mianya katika chokaa hiyo. Miamba hiyo ilipotokea juu na kupigwa na hewa, ilipoa na kuwa ngumu. Lakini kwa nini haikukauka na kufanyiza mawe yasiyo na umbo lolote?

Miamba iliyoyeyuka ina kemikali nyingi na kwa hiyo inaweza kutokeza mawe ya aina mbalimbali. Utendaji huo ulifanyiza mawe ya volkano katika barabara ya Giant’s Causeway. Mawe hayo yalipopoa polepole, ukubwa wake ulipungua, na kwa sababu ya kemikali zake, mianya inayofanana yenye pande sita ilitokea kwenye sehemu ya nje ya mawe hayo. Kadiri sehemu ya ndani ya mawe hayo ilivyoendelea kupoa, ndivyo mianya hiyo ilivyozidi kuteremka polepole na kutokeza nguzo nyembamba za mawe ya volkano.

“Msanifu wa Ujenzi Ana Jambo Gani la Kujivunia?”

Nguzo kama hizo hazipatikani tu nchini Ireland au Scotland. Hata hivyo, katika sehemu nyingine ulimwenguni, hazipo mahali ambapo zinaweza kufikika kwa urahisi. Ni mara chache sana mtu atapata nguzo zenye pande sita zilizohifadhiwa vizuri mahali ambapo zinaweza kuonekana na kila mtu.

Mwishoni mwa karne ya 18, Bwana Joseph Banks alivutiwa sana na umaridadi wa ajabu wa nguzo chache ambazo aligundua katika Kisiwa cha Staffa hivi kwamba alisema hivi: “Makanisa makubwa na majumba ya kifalme yaliyojengwa na wanadamu si kitu yanapolinganishwa na nguzo hizi! . . . Msanifu wa ujenzi ana jambo gani la kujivunia?”

Tulipotembelea barabara ya Giant’s Causeway, mojawapo ya maajabu ya asili ya Ireland, tulichochewa kuwa na hisia kama hizo. Tulitembea-tembea katika sehemu hiyo ya asili na kutafakari uwezo na nguvu za Muumba na Mbuni Mkuu, Yehova Mungu.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Tukio la asili—Sehemu nyingi za juu za nguzo hizi za mawe zina pande sita

[Hisani]

Courtesy NITB

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nguzo za mawe ya volkano ziko kwenye pwani yenye urefu wa kilometa sita

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nguzo ya Giant’s Boot (Kiatu cha Jitu), yenye kimo cha meta mbili hivi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nguzo hizi zenye kimo cha meta 12 zinafanana na mifereji ya kinanda kikubwa

[Picha katika ukurasa wa 16]

Top left: Courtesy NITB; bottom: © Peter Adams/Index Stock Imagery