Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jihadhari na “Dragoni Weupe”!

Jihadhari na “Dragoni Weupe”!

Jihadhari na “Dragoni Weupe”!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI USWISI

Ni nini huruka bila mabawa, hupiga bila mikono, na kuona bila macho?—Kitendawili cha dragoni wawili weupe kilichotegwa tangu Zama za Kati.

MAPOROMOKO ya theluji yanayoitwa kwa kufaa, dragoni weupe, yanaweza kumfunika mpanda-mlima, au hata kuzika kijiji kizima kwa ghafula. Kwa sababu hiyo, watu waliita maporomoko ya theluji kifo cheupe. Ni nini hutokeza maporomoko hayo ya theluji yenye kutisha? Ikiwa unaishi karibu na milima yenye vilele vilivyo na theluji unajua jibu. Huenda usiwe na wasiwasi ikiwa unaishi katika maeneo ya tropiki au kwenye nyanda za chini, kwani maporomoko ya theluji hayatawahi kuwa tisho kwako isipokuwa usafiri kwenye nchi iliyo na dragoni hao weupe.

Maporomoko ya theluji hutokea kwenye milima mirefu ambako theluji humwagika kwa wingi na mara nyingi. Maporomoko hayo hutokea kwa ghafula wakati theluji nyingi, barafu, udongo, mawe, na vitu vingine kama vile magogo yanapoteremka kwa kasi kutoka mlimani, na mara nyingi kuharibu kila kitu njiani. Uzito na nguvu za poromoko la theluji husababisha uharibifu mkubwa, na pia shinikizo la hewa ambalo hulitangulia linaweza kuharibu msitu mkubwa na vitu vingine vilivyo njiani kama vile madaraja, barabara, au reli.

Tukio la Asili

Rundo kubwa la theluji hufanyizwa hasa kwa chembe ndogo za theluji. Chembe maridadi za theluji zinazomwagika zinawezaje kuwa poromoko lenye kusababisha uharibifu mkubwa? Jibu linapatikana katika muundo wa theluji. Theluji imefanyizwa kwa maumbo mbalimbali: fuwele, vidonge, na punje. Theluji zenye umbo la fuwele ni kama nyota iliyo na ncha sita yenye miundo mbalimbali. Kila moja hustaajabisha! Zinaweza kubadili umbo zinapoanguka chini. Kiasi cha halijoto na shinikizo lililopo kutokana na theluji iliyokusanyika hufanya fuwele hizo kuwa ndogo zinapoanguka. Sentimeta 30 za theluji iliyotoka kumwagika inaweza kuganda na kuwa sentimeta 10 katika muda wa saa 24 tu.

Uthabiti wa theluji iliyo juu hubadilika kwa kutegemea umbo la chembe za theluji. Fuwele zenye umbo la ncha sita huungana, lakini punje na vidonge huanguka moja juu ya nyingine na kufanyiza rundo lisilo imara. Zinaweza kusonga kwa urahisi juu ya rundo la chini lililo imara. Kwa hiyo, aina ya theluji, kiasi kilichomwagika, mteremko wa mahali, halijoto, na nguvu za upepo huamua kama poromoko litatokea. Pia poromoko linaweza kuanzishwa mtu au mnyama anapopita kwenye mteremko mkali wenye theluji. Hata hivyo, maporomoko ya theluji yanaweza kuanza kwa njia nyingine.

Maporomoko ya theluji yanayosababishwa na upepo huanza wakati vidonge na fuwele za theluji iliyotoka tu kumwagika, yaani, theluji nyepesi inayopendwa na watu ambao huteleza kwenye theluji, inapopeperushwa na upepo mkali. Kwa kuwa ni nyepesi, theluji hiyo huinuliwa hewani na inaweza kupeperushwa chini kwa mwendo wa kilometa 300 kwa saa. Kwa hiyo, shinikizo la hewa linaloitangulia huongezeka hivi kwamba poromoko hilo lililo hewani linaweza kung’oa paa na hata kuharibu nyumba kwa sekunde chache tu.

Poromoko hatari zaidi ni lile linalosababishwa na theluji iliyoganda. Maporomoko ya aina hiyo husababishwa na rundo la theluji iliyomwagika na kuganda kwa muda mrefu. Tabaka la juu la theluji hiyo linapovunjika, vipande vikubwa vya barafu vinaweza kuteremka kutoka mlimani kwa mwendo wa kati ya kilometa 50 na 80 kwa saa. Marundo kama hayo yanaweza pia kuning’inia kwenye ncha ya jabali. Marundo hayo yanaweza kuwa hatari kwa watu wanaoteleza kwenye theluji kwani uzito wa mtu mmoja tu unaweza kuvunja rundo hilo na kuanzisha poromoko ambalo linaweza kumzika kwa sekunde chache tu.

Wakati wa majira ya kuchipua kunakuwa na hatari kubwa zaidi ya maporomoko ya theluji. Mvua au jua kali hufanya theluji iwe laini, ambayo mara nyingi hutokeza maporomoko ya theluji iliyoyeyuka. Maporomoko hayo husonga polepole, lakini yanaweza kufanya theluji yote kwenye mteremko iporomoke. Theluji hiyo inapoporomoka, hubeba mawe, miti, na udongo, ambazo hufanyiza kuta za takataka poromoko hilo linapokwisha.

Mabamba ya barafu pia huporomoka kama theluji. Mabamba makubwa ya barafu hutokea kwenye maeneo baridi sana, kwenye mabonde, au kwenye miteremko isiyopigwa na jua ambako theluji haiyeyuki kamwe. Hata hivyo, baada ya muda theluji huganda na kuwa barafu ngumu. Barafu huteremka polepole sana. Haitokezi madhara makubwa kwa kuwa maporomoko hayo yanaweza kutabiriwa.

Maporomoko ya Theluji Hutokea Wapi?

Si maeneo yote yenye theluji hutokeza maporomoko ya theluji. Ili yatokee, lazima kuwe na milima yenye urefu wa kadiri fulani na hali ya hewa inayoweza kufanya kuwe na theluji na barafu. Takwimu zinaonyesha kwamba kila mwaka maporomoko ya theluji yapatayo milioni moja hutokea ulimwenguni pote. Kuna maeneo fulani hatari katika Milima ya Andes ya Amerika Kusini, Milima ya Rocky ya Amerika Kaskazini, Milima ya Himalayas ya Asia, na bila shaka, Milima ya Alps ya Ulaya, inayoanzia Ufaransa na kuelekea kaskazini-mashariki hadi Uswisi, Ujerumani, na Austria. Katika sehemu fulani za maeneo hayo ambako watu huishi, wastani wa watu 200 huuawa na maporomoko ya theluji kila mwaka. Kati yao, wastani wa watu 26 huuawa nchini Uswisi.

Maporomoko mawili yaliyosababisha uharibifu mkubwa yalitukia katika Milima ya Andes ya Peru. Mnamo 1962, bamba la barafu lenye urefu wa kilometa moja lilivunjika kutoka kwenye kilele chenye barafu ya meta 50 cha Mlima Huascarán wenye urefu wa meta 6,768. Bamba hilo la barafu lenye uzito wa tani milioni nne lilikuwa kubwa mara nne kupita jengo la Empire State Building la New York! Barafu hiyo ilisafiri kwa mwendo wa kilometa 18 kwa dakika 15. Vijiji saba vilizikwa na theluji, na kati ya watu 3,000 na 4,000 waliuawa na vifusi vilivyokuwa na kina cha meta 13 ambavyo vilifunika eneo lenye upana wa kilometa mbili. Mnamo 1970, jambo kama hilo lilitukia tena kwenye mlima huo. Hata hivyo, wakati huo tetemeko la nchi lilitikisa barafu iliyokuwa kwenye kilele cha kaskazini. Mlima wenyewe uliporomoka. Tani elfu kadhaa za theluji, mawe, na barafu ziliteremka kwa mwendo wa kilometa 300 kwa saa kupitia korongo nyembamba, na kusomba mawe makubwa na nyumba zilizokuwa njiani. Ilikadiriwa kwamba watu 25,000 walikufa. Ni nini kinachoweza kufanywa ili kulinda wakazi wa milimani na misiba hiyo?

Je, Maporomoko ya Theluji Yanaweza Kuzuiwa?

Maporomoko fulani ya theluji yanaweza kuzuiwa. Mengine hayawezi. Maporomoko ya theluji yanayosababishwa na hali ya hewa hayawezi kuzuiwa; ni ya kawaida kama maji ya mvua yanayotiririka kutoka kwenye paa. Ni matukio ya asili yanayosababishwa na misimu mbalimbali. Lakini maporomoko ya theluji yaliyotukia katika maeneo fulani yamewafanya wenye mamlaka serikalini wapige marufuku ujenzi wa nyumba katika maeneo hatari na kulinda barabara kwa kujenga barabara za chini ya ardhi au zilizoezekwa juu. Kwa upande mwingine, maporomoko ya theluji yanayosababishwa na watu wasiojali kama vile watelezaji kwenye theluji ambao hupuuza maonyo, yanaweza kuzuiwa.

Nchini Uswisi, serikali ililazimika kuchukua hatua za tahadhari kwa sababu ya mambo yaliyotukia zamani. Mnamo 1931, tume ya utafiti ya Uswisi ilianzishwa, na katika mwaka wa 1936, kikundi cha kwanza cha watafiti jasiri kilianza kufanya uchunguzi wa kisayansi kwenye eneo la Weissfluhjoch lililo meta 2,690 juu ya mji wa Davos. Baadaye, mnamo 1942, Taasisi ya Kitaifa ya Uswisi ya Utafiti wa Theluji na Maporomoko ya Theluji ilianzishwa. Vituo kadhaa vya kuchunguza milima vilianzishwa katika sehemu mbalimbali milimani. Taasisi hizo hufanya iwezekane kutabiri badiliko la hali ya hewa, na hutoa onyo mara kwa mara kuhusu hatari ya maporomoko ya theluji kwenye miteremko isiyo na chochote.

Hata hivyo, bado kuna uwezekano wa hali ya hewa kubadilika bila kutarajiwa, na hatari zote haziwezi kuepukwa. Kwa hiyo, kila mtu anayeishi katika eneo hatari au aliye likizoni katika eneo la mlimani wakati wa majira ya baridi kali anapaswa kuwa mwangalifu asisababishe maporomoko ya theluji. Kwa kupendeza, nchini Ufaransa, majaribio yalionyesha kwamba mivumo ya ndege na pia sauti za wanadamu haziwezi kusababisha maporomoko ya theluji tofauti na ilivyoaminiwa hapo awali.

Mbinu za Serikali za Kuandaa Ulinzi

Punde tu baada ya watu kuanza kuishi katika maeneo ya mlimani, walitambua hatari ya maporomoko ya theluji. Ili kuzuia nyumba zao zisizikwe na theluji, walipanda misitu mikubwa kwenye miteremko iliyokuwa juu ya nyumba zao na hakuna mtu aliyeruhusiwa kukata miti hiyo. Katika visa vingi misitu hiyo ilisaidia na hiyo ndiyo sababu hadi leo hii bado inalindwa na kutunzwa na serikali. Misitu hiyo ndiyo ulinzi bora wa asili dhidi ya maporomoko ya theluji. Hata hivyo, imeonekana kwamba lazima misitu hiyo iwe na miti mingi, yaani, mamia ya miti katika kila eneo la ekari 2.5, na iwe na mchanganyiko wa miti ya zamani na miti michanga ya aina mbalimbali.

Hivi karibuni mainjinia wamejenga vizuizi vya chuma vilivyoimarishwa kwa saruji. Vimejengwa katika maeneo ambayo theluji au barafu huvunjika juu ya kizuizi cha kwanza cha miti. Vizuizi hivyo vinaweza kujengwa kufikia kimo cha meta nne, lakini inagharimu pesa nyingi kujenga vizuizi hivyo kwenye kila mteremko. Ili kuzuia majengo yasifagiliwe, vizuizi vingine vilivyotengenezwa kwa marundo makubwa ya mawe na udongo huwekwa chini ya miteremko. Marundo hayo yanaweza kugeuza mkondo wa poromoko na kuuzuia usielekee kwenye vijiji na nyumba zilizo bondeni. Vizuizi vingine hutengenezwa kwa kuta za udongo zenye umbo la V ambazo zina upana wa meta mbili na kimo cha meta tano. Ncha ya umbo hilo la V huelekea mlimani, ili kugawanya poromoko la theluji katika sehemu mbili na kuelekeza theluji pande zote mbili. Sehemu ya chini ya V hiyo huwa na urefu wa meta 90 au 120 na inaweza kulinda mji mzima usiharibiwe. Hata hivyo, wakati barabara au reli muhimu katika bonde hilo zinapohatarishwa, ulinzi bora na unaogharimu pesa nyingi ni kujenga barabara za chini ya ardhi au zilizoezekwa juu kwa mbao, chuma, na saruji.

Njia nyingine ya kuzuia maporomoko ya theluji ni kuvunja marundo mazito ya theluji. Kwa mfano, jeshi la Kanada hupiga doria katika kila mji wakati wa majira ya baridi kali na kulipua theluji. Kwa kufanya hivyo wao hulinda Barabara Kuu Inayovuka Kanada, kwa kuvunja theluji kabla haijaporomoka na kufunika barabara. Kwa kadiri fulani, mbinu hiyo hutumiwa pia nchini Uswisi, ambako baruti hulipuliwa au kuangushwa kutoka kwenye helikopta juu ya miteremko fulani ili kuondoa theluji.

Kuokolewa Kutoka Kwenye Poromoko la Theluji

Watu wanaoteleza kwenye theluji na wapanda milima wanapaswa kusubiri hadi miteremko ijaribiwe na kuonwa kuwa salama. Usipuuze maonyo yaliyobandikwa! Kumbuka kwamba hata mtelezaji stadi anaweza kuzikwa na theluji. Ukijikuta katika poromoko la theluji usiwe na wasiwasi! Wataalamu wanashauri usonge kana kwamba unaogelea baharini. Hilo litakusaidia ubaki karibu na sehemu ya juu ya poromoko hilo. Au nyoosha mkono mmoja juu kabisa iwezekanavyo. Hilo linaweza kuwajulisha waokoaji mahali ulipo. Funika mdomo na pua lako kwa kutumia mkono ule mwingine. Takwimu za watu waliookolewa zinaonyesha kwamba ni asilimia 50 pekee ya watu wanaozikwa na maporomoko ya theluji ambao huokoka baada ya kuzikwa kwa zaidi ya dakika 30. Siku hizi, baadhi ya watu wanaoteleza kwenye barafu hubeba taa za aina fulani kama vile transmita zinazotumia betri. Kwa kuwa kila mara kunakuwa na uwezekano wa mtu kufa kutokana na poromoko la theluji katika maeneo ya milimani, jitihada za haraka za kuwaokoa watu zinahitajika.

Kwa karne nyingi, mbwa waliojulikana sana wanaoitwa Saint Bernard walifugwa na watawa wa kiume wa Augustine katika Milima ya Alps ya Uswisi. Mbwa hao walikuwa na nguvu za kutembea katika theluji nyingi na kuhimili upepo na baridi kali. Walikuwa na uwezo mzuri wa kujua njia na kunasa sauti na kuona kwa haraka kitu kinaposonga, uwezo ambao mwanadamu hakuwa nao. Hivyo waliokoa watu wengi! Leo mbwa wengi wanaookoa watu ni wale wanaoitwa German shepherd, lakini aina nyingine ya mbwa wamezoezwa kufanya kazi hiyo. Isitoshe, vifaa vya elektroniki husaidia sana, na waokoaji wanapovitumia kwa makini, vinaweza kuokoa uhai. Hata hivyo, haviwezi kuokoa watu wengi kama vile mbwa waliozoezwa.

Kama vile tumeona, kile ambacho “huruka bila mabawa, hupiga bila mikono, na kuona bila macho” ni kitu chenye kutisha kilicho na nguvu nyingi za asili. Tunapaswa kujihadhari na dragoni weupe.

[Blabu katika ukurasa wa 19]

Ukijikuta katika poromoko la theluji songa kana kwamba unaogelea baharini

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kwa karne nyingi, mbwa wanaoitwa “Saint Bernard” wametumiwa kuokoa watu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

AP Photo/Matt Hage