Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wakati Ambapo Damu Ilimwagwa Katika Jina la Kristo

Wakati Ambapo Damu Ilimwagwa Katika Jina la Kristo

Wakati Ambapo Damu Ilimwagwa Katika Jina la Kristo

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Mexico

“Wakati wa Misa, makasisi walikuwa wakipaaza sauti toka kwenye mimbari na kusema: ‘Wana wa [Kanisa Katoliki], ingieni vitani! Serikali inataka kunyakua makanisa!’” —Pedro Rosales Vargas, aliyeshuhudia.

KWA nini watu wa dini wachukue silaha kupigania imani yao? Matokeo yaweza kuwaje watu wakigeukia jeuri ili kulinda dini yao? Twaweza kupata majibu ya maswali hayo kwa kuchunguza yale Maasi ya Kristero yaliyotokea nchini Mexico, ambayo pia huitwa Makristero kufuatia jinsi walivyoitwa wale walioshiriki katika maasi hayo.

Kichapo Enciclopedia Hispánica chaeleza hivi: “Makristero ni jina walilopewa Wakatoliki wa Mexico walioasi dhidi ya Rais Plutarco Elías Calles mwaka wa 1926 kwa sababu ya hatua alizochukua dhidi ya kanisa hilo, kama vile kufunga vituo na majengo ya kidini.” Mwanzoni serikali ndiyo iliyowaita Makristero kwa sababu ya kelele zao za kutiana shime, “Na aishi maisha marefu Kristo Mfalme!” Hata hivyo, mzozo wenyewe ulikuwa umeanza hata kabla ya wakati huo.

Chanzo cha Mzozo

Zile sheria za Marekebisho, zilizokuwa zimepitishwa kwa mara ya kwanza mnamo miaka ya 1850, hatimaye zilihalalishwa mwaka wa 1917. Mojawapo ya malengo ya sheria hizo lilikuwa “kutaifisha mali zilizokuwa zikimilikiwa na kanisa.” (Historia de México) Serikali ilitunga sheria hizo ili kulizuia Kanisa Katoliki lisijilundikie mali na mashamba. Kupitishwa rasmi kwa sheria hizo kulizusha malalamiko mengi kutoka kwa makasisi. Nayo serikali ikachukua hatua kwa kuwakamata makasisi kadhaa.

Mojawapo ya malengo ya Mapinduzi ya Mexico (1910-1920) lilikuwa kuwapa maskini mashamba. Kwa hiyo, sheria hizo mpya zilipendekeza wenye mashamba makubwa-makubwa wanyang’anywe na maskini wagawiwe mashamba hayo katika yale yaliyoitwa marekebisho ya ardhi. Kwa ujumla, makasisi walitaka kuingilia mambo hayo kwa kuwa sheria hizo zingewaathiri makasisi waliokuwa na uvutano mkubwa ambao walikuwa na mashamba makubwa-makubwa. Kanisa lilidai kwamba halikupinga kugawanywa kwa mashamba, bali liliunga mkono mpango tofauti na ule uliopendekezwa na serikali.

Hata hivyo, watu fulani waliamini kwamba kanisa lilinuia tu kutetea masilahi ya wenye mashamba makubwa-makubwa, kutia ndani makasisi waliokuwa matajiri. Kwa upande mwingine, kulikuwa na makasisi walioitwa agrarians waliotaka maskini wagawiwe mashamba. Mzozo huo kanisani ukapanua pengo lililokuwapo kati ya kanisa na serikali.

Mapema mwaka wa 1925, Plutarco Elías Calles, aliyekuwa tu ameshika hatamu za urais wa Jamhuri ya Mexico, akaanza kutekeleza kwa uthabiti vifungu vya katiba mpya vilivyohusu kanisa. Kwa mfano, aliwafukuza makasisi wengi wa kigeni wa Kanisa Katoliki kutoka nchini Mexico. Isitoshe, askofu mkuu wa Mexico alikamatwa baada ya kutangaza kwamba makasisi wangepinga vifungu vya katiba vilivyowapinga. Pia baadhi ya majengo ya kanisa yakanyakuliwa. Watu wengi waliamini kwamba hatua hizo zilichukuliwa ili kuzuia pesa nyingi za Mexico zisipelekwe Roma.

Mnamo Julai 1926 maaskofu wa Mexico walisimamisha kwa muda misa za kanisa. Serikali iliiona hatua hiyo kuwa mbinu ya kuchochea umma dhidi ya serikali. Vyovyote vile, kusimamisha misa za kanisa kulichochea mwanzo wa maasi mabaya ya Kristero

Vita Vyazuka

Maelfu ya Wakatoliki waliochochewa na makasisi wao waliingia vitani ili kutetea dini yao. Waliibeba sanamu ya Bikira wa Guadalupe kama bendera yao. Ingawa baadhi ya Makristero walitazamia viongozi wao wapiganie kanisa lao, maaskofu na makasisi wengi hawakujihusisha katika mapigano hayo kwa kuwa walihofu kwamba serikali ingewachukulia hatua. Badala yake, wengi wao walijificha katika nyumba za familia zilizokuwa tajiri, pasipo kushiriki katika mapambano huku watu wa kawaida wakiendeleza maasi yenye jeuri.

Hata hivyo, makasisi fulani waliunga mkono upande mmoja au mwingine. Kulingana na kitabu The Cristiada, (Buku la Kwanza, Vita vya Makristero), makasisi 100 wa Katoliki waliwapinga Makristero, huku wengine 40 wakiunga mkono vita hivyo. Makasisi wengine tano walijiunga na mapigano hayo.

Maasi hayo yalikuwa na matokeo mabaya sana. Watu katika maeneo mengi wakawa mafukara. Isitoshe, kuna vijana wengi waliolazimishwa na Makristero kuingia vitani. Pia, mara kwa mara vikosi vya Makristero na vya serikali vilivamia familia mbalimbali na kudai chakula. Isitoshe vikosi vyote viwili viliwalala wanawake kinguvu na familia nyingi zikafiwa.

Makristero na wanajeshi wa serikali pia walitenda kijeuri kupita kiasi, kutia ndani kuwaua watu wengi ambao hawakuhusika katika maasi hayo. Mwishoni mwa vita hivyo, idadi ya wale waliouawa inaonyesha matokeo yenye kusikitisha ya vita hivyo. Watu 70,000 hivi waliuawa katika vita hivyo vilivyodumu kwa miaka mitatu.

Vita Vyasimamishwa

Baada ya mapatano rasmi kati ya Kanisa Katoliki na serikali kufikiwa mnamo Juni 1929, uhasama ulipungua, na kufikia Agosti vita vikasimamishwa. Hata hivyo, Makristero hawakuwa wamehusishwa katika mapatano hayo, na hawakuelewa kwa nini kanisa lilikubali kufanya mapatano na watu ambao walionwa kuwa adui za mamlaka ya mbinguni. Hatimaye, Makristero walitii amri za makasisi, wakasalimu amri na kurejea makwao wakiwa wamekata tamaa. Serikali iliahidi kutowakandamiza na ikawaruhusu waanze tena kufanya Misa. Hata hivyo, zile sheria za vikwazo vya kidini hazikubadilishwa.

Watu fulani wamesema kwamba Maasi ya Kristero yalitumiwa na baadhi ya wafuasi wa Kanisa Katoliki kunyakua tena mamlaka ambayo kanisa lilikuwa nayo wakati wa ile enzi iliyotangulia sheria za Marekebisho. Licha ya vita hivyo, sheria hizo zilitekelezwa nchini Mexico hadi mwaka wa 1992, wakati ambapo sheria inayohusu mashirika ya kidini ilipopitishwa. Hata leo hii, bado watu hawana imani na mashirika ya kidini. Bado makasisi na viongozi wa kidini hawaruhusiwi kujiunga na siasa, na ingawa mashirika ya kidini yanaweza kumiliki mali, mali ambayo kanisa lilimiliki kabla ya 1992 inamilikiwa na serikali. Hata hivyo, sheria hizo hazijawazuia makasisi wengi kujihusisha na mambo ya kisiasa nchini Mexico.

Maasi Hayo Yalitimiza Nini?

Je, Makristero walipata faida yoyote ya kudumu kwa kwenda vitani kupigania imani yao? María Valadez, aliyeokoka msukosuko huo, anasema hivi: “Naamini kwamba mauaji yote hayo yalikuwa bure. Yalikuwa ya kipumbavu.” Pedro Rosales Vargas, aliyenukuliwa mwanzoni, alisema hivi kuhusu matokeo yenye kusikitisha ya vita hivyo: “Watu waliuana wao kwa wao, hata waliwaua watu wa dini yao wenyewe. Hivyo ndivyo nilivyopata kuwa yatima—walimuua babangu.”

Matokeo mabaya ya Maasi ya Kristero hayajazuia maoni ya wanadini kuchochea mapambano zaidi kama yale ya Ireland Kaskazini na nchi iliyokuwa ikiitwa Yugoslavia. Msiba kama huo waweza tu kuzuiwa kwa kuwa wafuasi wa dini ya kweli ya Kristo. Yesu aliwaamuru wafuasi wake wasijiingize katika siasa, wasiwe “sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:16; 18:36) Alimwambia hivi mtume Petro ambaye alijaribu kutumia nguvu ili kuzuia Yesu asikamatwe: “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wale wote wanaouchukua upanga wataangamia kwa upanga.”—Mathayo 26:52.

Wakristo Hutendaje Wanapokandamizwa?

Je, hilo linamaanisha kwamba Wakristo wa kweli hawapaswi kuchukua hatua yoyote wanapoona kwamba uhuru wao wa kuabudu unahatarishwa? Hapana. Wakristo wa karne ya kwanza waliponyanyaswa, walijitetea mara kadhaa kupitia mifumo ya sheria iliyokuwapo. Waliwasilisha kesi zao mahakamani. Ingawa nyakati nyingine walifungwa, hawakuacha imani yao wala kujiingiza katika mambo ya kisiasa.—Matendo 5:27-42.

Wakristo wa kwanza hawakuchukua silaha kamwe ili kutetea haki zao za kidini kupitia jeuri. Wakristo wa kweli hawaui watu wa dini nyingine yoyote wala watu wa dini yao. Badala yake wanatii fundisho hili la Bwana wao: “Kwa jambo hili wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo kati yenu wenyewe.”—Yohana 13:35.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Kasisi akiwa pamoja na Makristero wawili

[Hisani]

© (Inventory image number: 422036) SINAFO-Fototeca Nacional

[Picha katika ukurasa wa 13]

Rais Plutarco E. Calles

[Hisani]

© (Inventory image number: 66027) SINAFO-Fototeca Nacional

[Picha katika ukurasa wa 13]

Baadhi ya viongozi wa Makristero

[Hisani]

© (Inventory image number: 451110) SINAFO-Fototeca Nacional