Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Alizeti—Ua Maridadi na Lenye Manufaa

Alizeti—Ua Maridadi na Lenye Manufaa

Alizeti—Ua Maridadi na Lenye Manufaa

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Uswisi

YAMKINI sisi hufurahishwa na nuru na joto la jua. Hivyo, haishangazi kwamba watu katika sehemu mbalimbali za ulimwengu hufurahishwa na ua linalofuata jua! Ua hilo ni alizeti (sunflower). Ua la alizeti lililo katika bustani huvutia sana linapochanua na linaweza kumfanya mtu achangamke. Ikiwa ua moja tu linaweza kufanya hivyo, je, si wazi kwamba maua mengi yenye umbo la duara na rangi ya manjano yaliyo katika shamba kubwa yatafanya mengi zaidi?

Lakini je, unajua jinsi ua hilo zuri lilivyokuja kuwavutia watu wengi sana? Je, kweli ua hilo hufuata jua? Na je, ua hilo hutunufaisha?

Linapelekwa Sehemu Mbalimbali za Ulimwengu

Mwanzoni, ua la alizeti lilipatikana tu katika Amerika ya Kati hadi kusini mwa Kanada. Wenyeji wa asili wa Amerika walipanda alizeti katika eneo hilo. Katika mwaka wa 1510 W.K., wavumbuzi Wahispania walipeleka ua hilo katika maeneo yaliyoko ng’ambo ya Bahari ya Atlantiki, kisha likaenea haraka huko Ulaya. Mwanzoni, watu waliona kwamba ua hilo linafaa tu kurembesha bustani za maua. Lakini kufikia katikati ya karne ya 18, mbegu za alizeti zilianza kuliwa. Pia, watu walitumia majani na maua yake kutayarisha kinywaji cha kutibu homa.

Mnamo 1716, Mwingereza fulani alipata leseni ya kukamua mafuta ya alizeti na kuyatumia katika kiwanda cha kufuma na kulainisha ngozi. Hata hivyo, watu katika maeneo mengi huko Ulaya hawakujua chochote kuhusu mafuta hayo hadi miaka ya 1800. Ama kweli, Maliki Petro Mkuu wa Urusi ndiye aliyetoa mbegu za alizeti huko Uholanzi katika mwaka wa 1698 na kuzipeleka Urusi. Hata hivyo, uzalishaji na uuzaji wa alizeti ulianza muda mrefu baadaye katika miaka ya 1830. Miaka michache baadaye, katika eneo la Voronezh huko Urusi, maelfu ya tani za mafuta ya alizeti yalikuwa yakitengenezwa. Muda si muda, maua ya alizeti yalipandwa katika maeneo jirani ya Bulgaria, Hungary, Rumania, Ukrainia na nchi ambayo zamani iliitwa Yugoslavia.

Inashangaza kwamba kufikia mwishoni mwa karne ya 19, wahamiaji Warusi walirudisha alizeti huko Amerika Kaskazini. Wahamiaji wa mapema wa bara hilo hawakuwa wameanza kulipanda ua hilo kama wenyeji wa asili wa Amerika walivyokuwa wakifanya. Leo, mashamba makubwa ya alizeti yanapamba maeneo mengi ulimwenguni.

Linafuata Jua

Je, kweli ua la alizeti hufuata jua? Bila shaka! Majani na maua yake huchochewa na nuru ya jua. Alizeti huhifadhi auxin, ambayo ni homoni inayodhibiti usitawi wa mimea. Kiasi kikubwa cha homoni zilizo katika sehemu ya mmea ambayo haielekeani na mwangaza wa jua husababisha shina la alizeti ligeuke kuelekea kwenye nuru. Likiisha kuchanua, haliendelei kugeuka kuelekea kwenye nuru, bali hubaki likielekea upande wa mashariki.

Jina la Kilatini la ua la alizeti, yaani, Helianthus annuus, hutokana na maneno ya Kigiriki yanayomaanisha “jua,” na “ua,” na neno la Kilatini linalomaanisha “-a kila mwaka.” Kwa kawaida alizeti hufikia urefu wa meta mbili hivi, lakini mimea mikubwa ya jamii hiyo ya maua hupita meta nne. Shina gumu na majani ya kijani yasiyo laini hufunikwa na ua kubwa lenye umbo la duara na petali za manjano. Petali hizo huzunguka eneo jeusi la katikati lililo na maua madogo yenye mirija. Maua hayo madogo yakichavushwa na wadudu, husitawi na kuwa mbegu ndogo za alizeti ambazo huliwa. Sehemu hiyo ya katikati ya alizeti inaweza kuwa na kipenyo cha kati ya sentimeta 5 na 50, na hutokeza mbegu 100 hadi 8,000 hivi.

Kuna jamii nyingi za Helianthus. Na aina mpya za maua ya jamii hizo zinaendelea kutokezwa kwa kutumia mbegu za aina tofauti-tofauti za jamii hizo. Ni jamii mbili tu ambazo huzalishwa. Jamii moja ni Helianthus annuus, ambayo hupandwa hasa ili kutokeza mafuta ya alizeti. Ile jamii nyingine ni Helianthus tuberosus, ambayo hupandwa hasa kwa ajili ya viazi vyake. Viazi hivyo hutumiwa kulisha mifugo na kutengeneza sukari na pombe.

Ua Linaloleta Faida ya Kiuchumi

Leo, alizeti hupandwa kwa wingi hasa kwa sababu mbegu zake hutokeza mafuta bora. Mafuta ya alizeti hutumiwa katika upishi, katika saladi, na kutengeneza siagi. Mbegu zake zina lishe bora kwani zina kati ya asilimia 18 na 22 za protini na aina nyingine za madini.

Watu wengi hupenda kula mbegu za alizeti zilizokaangwa na kutiwa chumvi. Mbegu za alizeti husagwa na unga wake huchanganywa na unga wa kuokea. Isitoshe, mafuta ya alizeti hutumiwa kutengeneza sabuni za nywele, dawa ya kujipaka midomo inapokauka, mafuta ya kujipaka, na bidhaa za watoto. Hutumiwa pia viwandani kutengeneza mafuta ya magari na mashine nyinginezo. Isitoshe, mbegu za alizeti hutumiwa kulisha ndege na mifugo.

Shamba la alizeti ni mahali panapowafaa sana nyuki, kwani katika shamba lenye ukubwa wa ekari mbili na nusu, unaweza kupata kilo 25 hadi 50 za asali. Baada ya kuvuna maua ya alizeti, mashina yake ambayo huwa na asilimia 43 hadi 48 ya sukari ya mimea, yanaweza kutumiwa kutengeneza karatasi na bidhaa nyingine. Sehemu zilizobaki za alizeti zinaweza kutumiwa kulisha mifugo au kama mbolea.

Bila shaka, alizeti ni zawadi yenye thamani kwa wanadamu. Umaridadi wake umewachochea wasanii kama vile Vincent van Gogh, ambaye alichora picha inayoitwa “Sunflowers” (alizeti). Popote lilipo, ua la alizeti hupamba nyumba na bustani zetu. Huenda tukalifikiria ua hilo linalopendeza na lililo na matumizi mengi tunaposoma maneno haya ya mtunga-zaburi: “Wewe mwenyewe umefanya mambo mengi, Ee Yehova Mungu wangu, naam, kazi zako za ajabu na mawazo yako kutuelekea . . . Zimekuwa nyingi sana kuliko vile ninavyoweza kusimulia.”—Zaburi 40:5.