Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuishi kwa Woga

Kuishi kwa Woga

Kuishi kwa Woga

ROXANA * anaogopa kumwambia mume wake kwamba anataka kufanya kazi ya muda. Wakati mmoja, alipomwomba mume wake nauli ili akamtembelee mama yake, alimpiga Roxana kwa nguvu sana hivi kwamba alihitaji kutibiwa. Yeye huishi kwa woga daima.

Rolando alizoea kumruhusu mke wake arudi nyumbani usiku kwa kutumia usafiri wa umma, lakini sasa yeye huenda kumchukua kwa gari lao. Kumekuwa na visa vingi sana vya jeuri mahali wanapoishi hivi kwamba anahofia usalama wa mke wake.

Haidé hufanya kazi katikati mwa mji mkuu. Wakati mmoja alipokuwa akirudi nyumbani, alijikuta katikati ya waandamanaji walioanzisha jeuri. Sasa kila mara anaposikia waandamanaji wakipita, yeye huwa na wasiwasi. Anasema hivi: “Sijihisi nikiwa salama. Sitaki kufanya kazi hapa tena. Lakini sina la kufanya.”

Roxana, Rolando, na Haidé wanaathiriwa na woga, na si woga ambao mtu huwa nao wakati tu hali ya dharura inapotokea. Wanaathiriwa na woga huo daima. Watu wanapolazimika kuishi kwa woga, huenda wakahisi hawana nguvu. Woga unaweza kuwanyima furaha kwa kuwazuia wasifanye wanachotaka. Woga unaweza kutawala fikira za watu na kuwazuia kukazia fikira mambo mengine.

Kuishi kwa woga hufadhaisha sana. Mara nyingi kunasababisha mshuko wa moyo na kunaweza kudhuru afya. Gazeti linalozungumzia masuala ya afya linaeleza kwamba “mfadhaiko huzuia mfumo wa kinga usifanye kazi na hilo huchangia magonjwa mengi. Mwili utaonyesha dalili za madhara ya muda mrefu, hasa katika viungo vilivyoathiriwa. Mtu anaweza kupatwa na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa figo, magonjwa ya tumbo, vidonda vya tumbo, kuumwa na kichwa, kukosa usingizi, mshuko wa moyo, na wasiwasi. Kufadhaika kwa muda mrefu chini ya hali hizo huchosha.”

Katika ulimwengu wa leo ni jambo la kawaida kuishi kwa woga. Je, tutawahi kuishi katika ulimwengu ambao watu wataishi bila woga?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Majina fulani yamebadilishwa.