Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kimchi—Chakula cha Wakorea Chenye Ladha Kali

Kimchi—Chakula cha Wakorea Chenye Ladha Kali

Kimchi—Chakula cha Wakorea Chenye Ladha Kali

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Korea

Wakorea wanapenda vyakula vyenye ladha kali, labda kimchi ndicho chakula wanachokipenda zaidi. Wengi wao hata hawawezi kuwazia kula chakula bila kimchi, wangekiona kuwa si kamili. Lakini kimchi ni nini hasa?

Kimchi ni mojawapo ya mboga zinazohifadhiwa kwa siki na chumvi ambazo hutumiwa katika nchi nyingi. Inafanana na sauerkraut ya Ujerumani, paocai ya China, tsukemono ya Japani, achar ya India, na mchanganyiko wa mboga zilizohifadhiwa kwa siki na chumvi unaotengenezwa sehemu nyingine. Aina zote tofauti za kimchi huwapa Wakorea vitamini muhimu na vilevile ladha ya pekee ambayo hufanya watu wanaoionja kwa mara ya kwanza wawe na maoni mbalimbali kuihusu. Watu wasiopenda kimchi hulalamika kuhusu ladha kali ya kitunguu-saumu na pilipili nyekundu. Hata hivyo, watu wanaopenda kimchi hupendezwa na ladha hiyo kali, nao hufurahia kuila mara kwa mara.

Kadiri watu wanavyozidi kutumia vikolezo katika vyakula vyao, ndivyo kimchi inavyozidi kujulikana ulimwenguni. Wafanyakazi wa kurekebisha vitu kutoka nchi za Magharibi, wafanyakazi-wahamiaji, na maelfu ya watu walioenda kwenye michezo ya Olimpiki huko Seoul mnamo 1988 waliionja. Kwa sababu ya hilo, katika nchi fulani sasa kimchi inaanza kutumiwa pamoja na vyakula vyepesi vinavyoliwa sehemu mbalimbali ulimwenguni kama vile hambaga, tacos, chow mein, sushi, na soseji. Mashirika fulani ya ndege yasiyo ya Korea huandaa kimchi pamoja na vyakula vyao. Katika maduka mengi makubwa ya Japani, chupa ndogo milioni kumi hivi za kimchi ya Korea, ziliuzwa katika kipindi cha miaka mitatu. Lakini kimchi hutayarishwaje?

Chakula Kilichochachishwa

Mboga zinapohifadhiwa katika chumvi huwa ngumu zaidi. Chumvi huzuia ukuzi wa viini hatari na kuchochea ukuzi wa viini vinavyofaa. Uchachishaji huo hutokeza asidi-amino na asidi ya laktiki, kwa hiyo kimchi huwa na ladha ya pekee iliyo tofauti sana na ladha ya kawaida ya mboga.

Mchanganyiko huo hutiwa vikolezo. Si vitunguu-saumu na pilipili nyekundu pekee ambazo hutumiwa kutayarisha kimchi. Viungo vingine vingi vinavyopatikana kwa urahisi na visivyopatikana kwa urahisi pia hutumiwa. Vinatia ndani vitunguu vya majani, karoti, liki, tangawizi, mbegu za ufuta, pea, chaza, uduvi wadogo wenye chumvi, chestinati, moluska, kokwa za msonobari, na majani ya baharini.

Kumbuka kwamba kimchi ni mlo unaoliwa na mlo mkuu. Hata mtu awe anapenda kimchi kadiri gani, mara nyingi kimchi huliwa na vyakula vingine, hasa wali. Wakorea hula kimchi kwa wali kama vile sisi hula ugali kwa mboga. Ladha ya wali na ladha kali na yenye chumvi ya kimchi hupatana.

Ina Vitamini na Madini Mengi

Kimchi imezidi kuwa maarufu kwa sababu watu wanazidi kupendezwa na vyakula vinavyoboresha afya. Zamani, manufaa ya afya ya kimchi yalipuuzwa kwa sababu ya ladha yake. Hata hivyo, kwa sababu ya watu kutiwa moyo wale mboga nyingi zaidi, sasa kimchi inasifiwa kwa sababu ya manufaa yake kwa afya. Kwa mfano, kabichi ya Kichina, figili, na pilipili nyekundu zina vitamini A nyingi. Pilipili nyekundu iliyosagwa ina vitamini C nyingi. Sehemu ya kijani kibichi ya liki ina vitamini A na C. Isitoshe, nyuzinyuzi za kabichi husaidia umeng’enyaji wa chakula.

Vyakula mbalimbali vya baharini vilivyochachishwa ambavyo huongezwa kwenye kimchi huwa na protini na asidi-amino nyingi ambazo kwa kawaida hazipatikani katika mboga. Chaza, ambacho ndicho chakula cha baharini kinachotumiwa sana kutayarisha kimchi huwa na kiasi kikubwa cha kalisi, chuma, glycogen, vitamini, na asidi-amino muhimu.

Inaaminiwa kwamba kuna zaidi ya aina 100 za kimchi. Kimchi zinaweza kutofautiana ikitegemea vitu vinavyotumiwa kuitayarisha, eneo ambako inatayarishiwa, muda wa kuichachisha, na kiwango cha halijoto na unyevu wakati wa kuitayarisha. Mabinti hujifunza siri ya kutayarisha kimchi yenye ladha nzuri kutoka kwa mama zao na familia nyingi hujivunia siri hizo. Kwa kweli, ustadi wa kutayarisha kimchi hutumiwa kuamua mpishi bora.

Kimchi Inafaa Maisha ya Kisasa

Siku hizi si lazima kutayarisha kimchi nyumbani. Vyumba vya kukuzia mimea huzalisha mboga mwaka mzima. Kimchi iliyotayarishiwa kiwandani inaweza kupatikana karibu katika duka lolote la kuuzia mboga. Haiwezekani kutayarisha kimchi nyingi katika nyumba za kisasa za jijini, lakini kiasi kidogo cha kimchi kinaweza kutayarishwa na kuwekwa kwenye friji badala ya kuwekwa kwenye vyungu.

Kimchi imekuwepo kwa muda mrefu. Inahimili majira marefu ya baridi kali na pia yaelekea itahimili mabadiliko ya maisha, kama vile imefanya kwa karne nyingi. Je, ungependa kuionja? Usivunjwe moyo na harufu yake kali. Yaelekea utapendezwa na moja kati ya aina zaidi ya 100 za kimchi. Basi ikiwa utapendezwa nayo, “Mat-itkae duseyo!” Maneno hayo yanamaanisha “Furahia mlo wako!” katika Kikorea.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]

Kutayarisha Kimchi Wakati wa Majira ya Baridi Kali

Zamani wakati ambapo hakukuwa na friji na halijoto ilipokaribia kiwango cha kuganda wakati wa majira marefu ya baridi kali huko Korea, watu walilazimika kutayarisha vyakula ambavyo vingedumu kwa muda mrefu. Suluhisho lilikuwa kimchi. Kutayarisha kiasi kikubwa cha kimchi kunaitwa kimjang. Chakula hicho kilitayarishwa karibu mwisho wa Novemba hadi katikati ya Desemba.

Watu wa ukoo walipoishi pamoja, kabichi za Kichina 100 hivi zingeweza kutumiwa kutayarisha kimjang! Pia kiasi cha viungo vingine vya kutayarisha kimchi kingeweza kuwa kikubwa unapofikiria aina mbalimbali za kimchi. Nyakati nyingine familia, marafiki, na majirani wangekusanyika pamoja katika nyumba ya familia fulani ili kusaidia kutayarisha kimjang kisha wangeenda kwenye nyumba ya familia nyingine na kufanya vivyo hivyo. Bado kampuni nyingi huwapa wafanyakazi wao ‘marupurupu ya kimchi’ wakati fulani katika mwaka ili kugharimia viungo vyote vya kutayarisha kimchi kwa ajili ya majira ya baridi kali.

Kiasi kikubwa cha kimchi kilihifadhiwaje? Katika vyungu. Mwezi mmoja kabla ya kimjang, vyungu vilivyotumiwa kutayarisha kimchi vilizikwa ardhini. Baada ya kabichi za kimchi kuwekwa vizuri ndani ya vyungu hivyo, zilisindiliwa kwa jiwe na kufunikwa. Kwa kuwa vyungu vina matundu madogo, kimchi ingedumu kwa muda mrefu.

[Picha]

Kutoa kimchi kwenye chungu

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Aina Moja ya Kimchi ya Korea Yenye Vikolezo

VIUNGO VIKUU

Nusu kilo ya kabichi ya Kichina

Vijiko 2 vikubwa vya chumvi

Vikombe 4 vya maji baridi

Vikombe 2 vya maji moto

VIKOLEZO

Kijiko 1 kikubwa cha kitunguu-saumu kilichokatwa-katwa

Kijiko 1 kikubwa cha tangawizi iliyokatwa-katwa

Kijiko 1 kikubwa cha kitunguu cha majani kilichokatwa-katwa

Vijiko 2 vidogo vya pilipili nyekundu iliyokatwa-katwa na kukaushwa

Vijiko 2 vidogo vya sukari

Kijiko 1 kikubwa cha chumvi

UTAYARISHAJI: Ondoa jani mojamoja la kabichi na uyanyunyizie chumvi. Yamwagie maji baridi, na kuacha mchanganyiko huo mahali baridi kwa saa nane au usiku mzima. Suuza kabichi vizuri na ukamue maji. Mwaga maji moto sana kwenye vikolezo na kuvichanganya vizuri. Changanya vikolezo hivyo na majani ya kabichi. Weka mchanganyiko huo kwenye bakuli kubwa ya glasi. Unaweza kukata-kata majani ya kabichi mara mbili ili yatoshee. Funika bakuli hiyo kwa plastiki na kuiweka mahali baridi kwa siku mbili hivi. Mwaga maji na ukate-kate majani hayo vipande vidogo. Yaweke ndani ya chupa hadi wakati wa kuliwa. Vipimo hivi vinatosha nusu kilo ya kimchi.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Figili zilizokatwa-katwa, figili nzima, tango, na kabichi ya Kichina ndivyo viungo vikuu ambavyo hutumiwa kutayarisha ‘kimchi’