Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Dragoni Wanapotoweka

Dragoni Wanapotoweka

Dragoni Wanapotoweka

DAVID Hall anasema hivi katika gazeti Ocean Realm: “Nilipokaribia futi tatu, dragoni huyo alibadili tabia yake mara moja. Aliacha kula, akageuka na kutoweka mara moja kwenye magugu-maji yaliyokuwa karibu.” Hall alishangaa: “Mnyama huyo ana uwezo wa kipekee wa kujibadili rangi.” Katika tukio hilo, Hall alipata nafasi ya pekee sana ya kuona mojawapo wa viumbe wa majini anayeweza kujibadili rangi kwa njia ya ajabu, yaani, dragoni wa baharini wa Australia anayefanana na jani.

Dragoni hao husonga polepole na hutegemea sana uwezo wao wa kujibadili rangi ili wasiliwe na samaki. Miili yao yenye milia ya manjano na kijani-kibichi na viungo vya mwili vya ajabu vinavyofanana na jani, huwawezesha kubadili kabisa rangi na kufanana na nyasi za baharini zinazowazunguka. Wao huogelea wakitikisika kwa kuiga kikamili mwendo wa magugu-maji yanayoelea.

Uwezo huo wa ajabu wa kujibadili rangi huwawezesha kuvizia chakula wanachokipenda, yaani, uduvi wadogo. Mchunguzi mmoja anasema: “Wanajua sana kubadili rangi yao hivi kwamba uduvi hawawaoni kuwa tisho.” Dragoni wa baharini hubugia uduvi wanapoogelea, akiwamumunya kwa mdomo wake mrefu na kuwameza wakiwa wazima. Baada ya kuwinda kwa muda mfupi, yeye hutulia mahali pamoja kwa muda mrefu, siku tatu hivi, akishika tu viumbe wanaopita karibu naye.

Dragoni wa baharini wanaofanana na jani wanaweza kupatikana tu kwenye maji yasiyo na kina kando ya pwani ya Australia kusini. Miili yao iliyojipinda na yenye viungo vinavyofanana na majani huonekana kama dragoni wanaotumiwa wakati wa sherehe nchini China. Wao wanaweza kukua kufikia sentimeta 43, nao ndio viumbe wakubwa wa jamii ya samaki wanaotia ndani farasi-maji.

Wakati wa kuzaa, dragoni wa baharini wa kiume na wa kike hubadilishana madaraka. Naam, dragoni wa kiume hupata mimba na kuzaa watoto! Hali ya hewa inapoanza kuwa na joto, dragoni wa kiume hufanyiza kifuko cha uzazi chenye damu nyingi kilicho na mashimo madogo 120 hivi kwenye mkia wake. Kisha dragoni wa kike hutia mayai yake ya rangi ya waridi kwenye kifuko hicho, akitia kila yai kwenye shimo lake. Baada ya majuma manne au sita hivi, watoto wa dragoni wa baharini wenye urefu wa milimeta 20 hivi huzaliwa, kila mmoja akifanana na wazazi wake.

Kwa kweli, viumbe hao wenye kupendeza ni mfano mwingine wa uumbaji na ubunifu wa hali ya juu wa Yehova Mungu!—Zaburi 104:24, 25.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Dragoni wa baharini wa kiume anayefanana na jani akiwa amebeba mayai; picha ndogo inaonyesha kifuko chenye mayai

[Picha katika ukurasa wa 25]

Dragoni wa baharini aliyejibadili rangi; picha ndogo inaonyesha kiumbe huyo

[Picha katika ukurasa wa 25 zimeandaliwa na]

All photos except brood patch: Michael Morris-Immersedimagery@scubadiving.com