Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Farasi Wanaocheza Dansi Hewani”

“Farasi Wanaocheza Dansi Hewani”

“Farasi Wanaocheza Dansi Hewani”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

“Ni nani anayeweza kutazama hatua zako zenye utaratibu, zilizo sahihi kabisa, uwezo wako wa kujidhibiti, uwezo wako wa kugeuka kwa usahihi, na asifurahi?”—RAFAEL ALBERTI, MSHAIRI WA HISPANIA.

TAA zinazimwa na muziki unaanza. Kutoka nyuma ya uwanja, mpanda-farasi anaingia akiwa amepanda farasi mweupe akicheza kupatana na muziki. Baadaye, wapanda-farasi wengine wenye farasi wanaojipinda-pinda taratibu na kugeuka pamoja kwa upatano kamili wanajiunga naye. Watazamaji wanastaajabu kuona jinsi wanyama hao wenye kuvutia wanavyocheza kwa madaha.

Shule ya Kifahari ya Sanaa ya Mafunzo ya Farasi, huko Jerez de la Frontera, Hispania, imekuwa maarufu ulimwenguni kwa sababu ya farasi wake wanaocheza dansi. Tamasha hiyo huonyesha farasi wakicheza miondoko ya kawaida waliyofunzwa. Wapanda-farasi huwaongoza farasi kwa kuwagusa taratibu kwa mkono, mguu, au kwa kuwadukua kwa miili yao. Muziki wa kitamaduni wa Hispania na wapanda-farasi waliovalia mavazi ya karne ya 18 hufanya tamasha hiyo ipendeze hata zaidi.

Farasi wa Kiasili wa Hispania

Farasi wanaotumiwa katika tamasha hiyo ni farasi wa kiasili wa Hispania, ambao pia huitwa farasi wa Andalusia. Farasi wa Hispania ni aina ya farasi wa kale aliyeishi maelfu ya miaka iliyopita katika Rasi ya Iberia. Waroma walimwona farasi huyo kuwa anafaa hasa kwa ajili ya vita.

Sifa zenye kutokeza za farasi wa Andalusia ni nguvu, wepesi, fahari, na utiifu. Ni wenye thamani kwa sababu ya utu wao wa pekee wa kuwa jasiri lakini watiifu. Kwa sababu ya nguvu na wepesi wao, farasi hao wanaweza kucheza miondoko yenye hatua na miruko migumu. Hata hivyo, si rahisi kumfunza mnyama wa kifahari kucheza dansi kwa madaha.

Kumfunza Mnyama Huyo wa Kifahari

Shule ya Kifahari ya Sanaa ya Mafunzo ya Farasi ilianzishwa na Álvaro Domecq mwaka wa 1972. Shule hiyo huwafunza farasi kwa kuwafanyisha mazoezi ya viungo ili wawe na misuli yenye nguvu. Mwishowe, wataweza kufanya mazoezi magumu kwa upatano kamili. Mafunzo hayo hutolewa katika shule mbili mashuhuri: Shule ya Hispania ya Kuendesha Farasi ya Vienna, Austria, na Shule ya Kifahari huko Hispania. Katika shule hizo, wageni na hata watu wanaofanya kazi ngumu ya kuwazoeza farasi huvutiwa sana na maonyesho hayo.

Mpanda-farasi na farasi wake wanahitaji kufanya mazoezi mengi ili wafaulu kucheza kwa upatano kabisa. Kwa kawaida, mpanda-farasi na farasi hufanya mazoezi pamoja siku tano kwa juma, saa saba kwa siku, kwa kipindi cha miaka zaidi ya minne. Mafunzo huanza kwa mazoezi ya msingi ambapo mpanda-farasi humfunza farasi atii na atembee kuelekea mahali alipo anapomwita. Baada ya farasi kujifunza hatua hiyo ya kwanza, anapaswa kujifunza kuegemea nyuma anapotembea, na kutegemeza uzito wake kwa sehemu yake ya nyuma. Mazoezi hayo humwezesha farasi kuelekeza nguvu zake kwenye miguu yake ya nyuma, mbinu ambayo ni muhimu ili kufanya miondoko migumu zaidi.

Farasi hujifunza miondoko ya aina mbili: ya asili na ya kufundishwa. Miondoko ya asili huhitaji farasi aboreshe hatua zake za kawaida, yaani, kutembea, kukimbia kwa hatua fupifupi, na kukimbia kwa kasi. Miondoko inayofunzwa katika Shule ya Kifahari hutaka mpanda-farasi ashirikiane kwa ukaribu sana na farasi. Miondoko hiyo inahitaji usahihi wa hali ya juu na nguvu nyingi.—Ona “Miondoko ya Msingi ya Farasi Wacheza-Dansi.”

José María Sánchez Cobos, ambaye ni msimamizi wa maonyesho katika Shule ya Kifahari asema hivi: “Ili kufanya mazoezi magumu kwenye Shule hiyo ya Kifahari, farasi na mpanda-farasi wanahitaji kushirikiana kwa ukaribu. Farasi wa Andalusia huonwa kuwa mojawapo wa farasi mwenye sifa nzuri sana kati ya jamii zote za farasi, na baadhi ya wanyama hao wanaweza kuwa marafiki wakubwa wa mpanda-farasi. Hata hivyo, nyakati nyingine farasi na mpanda-farasi hawapatani, na hivyo inakuwa lazima mabadiliko yafanywe.”

Alipoulizwa jinsi ambavyo farasi huitikia muziki unapochezwa, José María anaeleza: “Farasi hawaelewi muziki kama sisi, lakini yaonekana kwamba wao huathiriwa na muziki wanaousikia kwenye maonyesho. Bila shaka, wao huitikia muziki wa kitamaduni ambao huwa sehemu ya maonyesho hayo, na inaonekana pia wao huitikia wakati watazamaji wanapopiga makofi.”

Farasi hufurahia utunzaji wa pekee ambao wao hupata katika shule hiyo. Wao hupambwa kwa uangalifu kwa ajili ya maonyesho, na kuoshwa kila siku baada ya maonyesho ili waondoe jasho na ili waburudike. Kwa kuwa ngozi yao huathirika kwa urahisi kuliko ya wanadamu, inahitaji kutunzwa kwa njia ya pekee.

José María anaongezea hivi: “Kuna msemo wa Kihispania unaosema kwamba, katika miaka 7 ya kwanza farasi huwa rafiki yako, miaka 7 hadi 14 unamfurahia, kisha baada ya miaka 14, hakufai chochote. Lakini hiyo si kweli katika shule yetu. Mmoja wa farasi wetu anayeitwa Zamorano, alikuwa bado akicheza akiwa na umri wa miaka 22!”

Baada ya kutunzwa na kuzoezwa kwa uangalifu, farasi hao huonyesha miondoko yao ya kipekee mbele ya watazamaji. Watazamaji wanaweza kujionea jinsi farasi na mpanda-farasi wanavyoshirikiana na jinsi farasi hao wenye fahari na wenye nguvu wanavyopiga hatua kwa kuzipatanisha na muziki wa kitamaduni wa Hispania. Hivyo, haishangazi kwamba katika mstari wa mwisho wa shairi lake lililonukuliwa awali, Alberti aliwaita wanyama hao wa kifahari, “farasi wanaocheza dansi hewani.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Miondoko YA Msingi ya Farasi Wacheza-dansi

Neno “miondoko” hurejelea hatua mbalimbali ambazo farasi hufanya. Ifuatayo ni baadhi ya miondoko mikuu.

Piaffe: Farasi husimama mahali pamoja akiruka-ruka kwa utaratibu fulani, ni kana kwamba anakimbia akiwa amesimama mahali pamoja.

Passage: Farasi hukimbia polepole huku akiinua kwato zake juu kana kwamba anacheza dansi.

Levade: Farasi huinua juu miguu yake ya mbele na kubaki katika mkao huo. Ili afanye hivyo, anahitaji kuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti misuli na kudumisha usawaziko kamili.

Curvet: Farasi huruka mara kadhaa kwa miguu yake ya nyuma bila miguu yake ya mbele kugusa chini.

Capriole: Farasi huruka hewani na anapofika kiwango cha juu zaidi huvuta miguu yake ya mbele chini ya kifua chake huku akirusha miguu yake ya nyuma.

Farasi Waliofungwa Lijamu

Mchezo mwingine unaokuwa katika tamasha hiyo ni enganche. Farasi hao huvuta magari ya farasi ya zamani kwa kupiga hatua zinazopatana kabisa. Jambo hilo pia huhitaji mazoezi ya miaka mingi. Wakiwa wamevikwa vizuri sana, farasi hao na wapanda-farasi huwa tamasha yenye kuvutia ambayo hufanya watazamaji wakumbuke wakati ambapo magari ya farasi yalitumiwa hasa katika usafiri.

[Hisani]

Piaffe, passage, and capriole: Fotografía cedida por la Real Escuela Andaluza; curvet, levade, and carriage: Fundación Real Escuela Andaluza del Arte Ecuestre

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Fotografía cedida por la Real Escuela Andaluza