Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Maji ya Bei Ghali

Gazeti la Ujerumani Natur+Kosmos linasema hivi: “Ni dalili ya watu wa kisasa. Vijana wanaoonekana kuwa wa kisasa nyakati zote hubeba maji ya chupa yenye jina la kampuni fulani maarufu. Huko New York, watu ambao huonekana kuwa wa kisasa hukutana katika baa za kunywea maji. Nazo hoteli maarufu zilizo na wahudumu huwa na maji yenye madini kutoka kampuni mbalimbali za kimataifa, nayo maji hayo huonwa kuwa ya hali ya juu kama tu mvinyo fulani unavyoonwa kuwa wa hali ya juu kabisa.” Maji hayo ni bei ghali sana. Makala hiyo inasema kwamba “watu hutoa pesa nyingi sana kwa ajili ya maji yenye madini ambayo wao hunywa yakiwa katika chupa zenye jina la kampuni maarufu.” Katika hoteli fulani lita moja ya maji kama hayo inaweza kugharimu dola 81. Ingawa maji ya chupa yanatumiwa sana na watu wanaoonekana kuwa wa kisasa, haimaanishi kwamba yanakufaa. Watengenezaji fulani huahidi kwamba yatamfanya mtu awe na afya nzuri ya kiakili na ya kimwili, na atakuwa mrembo. Lakini wataalamu wengi hawaoni faida yoyote ya maji hayo yanapolinganishwa na maji ya kawaida. Kwa mfano, gazeti hilo linasema kwamba nchini Ujerumani maji ya kawaida ya bomba ni mazuri tu kama maji yenye madini kutoka sehemu nyingine ulimwenguni. Nayo maji ya bomba hayahitaji kutiwa katika chupa za plastiki wala kusafirishwa kwa maelfu ya kilometa.

Siri za Ulaji wa Wafaransa

Gazeti UC Berkeley Wellness Letter linasema kwamba “Wafaransa hula vyakula vyenye mafuta mengi. Lakini wao ni wembamba kuliko Wamarekani wala haielekei kwamba watakuwa wanene kupita kiasi kama Wamarekani. Idadi ya Wafaransa wanaokufa kutokana na ugonjwa wa moyo ni nusu ya ile ya Wamarekani na ni ya chini zaidi ya nchi nyingine yoyote katika [Muungano wa Ulaya].” Kwa nini iko hivyo? Gazeti Wellness Letter linasema inawezekana kwamba Wafaransa “hula vyakula vyenye kalori chache.” Utafiti uliofanywa katika mikahawa ya Paris na ya Philadelphia, Pennsylvania, Marekani, ulionyesha kwamba watu walipakuliwa chakula kidogo zaidi katika mikahawa ya Ufaransa. Pia vitabu vya upishi vilitofautiana. Kwa mfano, kiasi cha nyama ambacho mtu alipaswa kupakuliwa kilikuwa kidogo zaidi katika vitabu vya upishi vya Wafaransa. Makala hiyo inasema hivi: “Labda jambo linalopendeza zaidi ni kwamba Wafaransa hutumia muda mwingi zaidi kula chakula kidogo walichopakuliwa. Mfaransa hutumia angalau dakika 100 kwa siku akila, huku Mmarekani akila mkate (na chochote kingine) kwa dakika 60 tu.” Kwa hiyo tuseme nini? Usile kalori nyingi. Kula kwa kiasi chakula kinachofaa. Usile haraka. Furahia chakula. Ukipakuliwa chakula kingi, mgawie rafiki au beba nusu ya chakula hicho na kukipeleka nyumbani. Na “furahia kula vyakula vilivyotayarishwa nyumbani.”

Tunza Vitabu Vyako

Makala katika gazeti Día Siete la Mexico inasema kwamba “adui mkubwa [wa vitabu] vyako ni wakati na unyevu.” Ili kuhifadhi vitabu vyako katika hali nzuri, makala hiyo inapendekeza uvipanguse vumbi angalau mara moja kwa mwaka. Hata hivyo, hakikisha kwamba umekibana vizuri ili vumbi isipenye ndani ya kurasa zake unapokipangusa. Katika maeneo yenye joto, unyevu unaweza kuzuiwa kwa kunyunyiza poda ya ulanga kwenye kila kurasa, kuweka kitu kizito juu yake kwa siku kadhaa, kisha kuondoa poda hiyo kwa brashi. Ikiwa kitabu kitapata kuvu kutokana na unyevu, kikwangue polepole kwa wembe na kukisafisha kwa alkoholi. Usitoe kitabu kwenye rafu yake kwa kukivuta kutumia sehemu ya juu. Njia bora ya kutoa kitabu katika rafu ni kukishika katika sehemu yake ya katikati kwa vidole viwili, kukisukasuka ili kukitenganisha na vitabu vingine, kisha kukivuta kwa wororo. Vitabu vikubwa sana vya zamani vinaweza kuharibika kwa sababu ya uzito wake. Hilo linaweza kuepukwa kwa kuviweka kwenye rafu vikiwa vimelazwa.

Wanaoamini Mungu Ni Mmoja Wanatoweka

Gazeti The Times la London linasema kwamba “madhehebu ya zamani zaidi [nchini Uingereza] . . . yanazidi kupungua na baada ya miongo kadhaa yatatoweka.” Madhehebu ya wanaoamini kwamba Mungu ni mmoja yana waumini wanaopungua 6,000 nchini Uingereza. Nusu yao wana umri wa zaidi ya miaka 65. Utabiri huo ulitolewa na Peter Hughes ambaye ni kasisi mkuu wa madhehebu hayo. Akitumia mfano wa kanisa la zamani zaidi lililoko Liverpool, Hughes alisema hivi: “Hawajawa na kasisi tangu mwaka wa 1976 na ni kama madhehebu ya wanaoamini kwamba Mungu ni mmoja yamekwisha kutokomea.” Gazeti The Times linasema kwamba madhehebu hayo yamekuwapo nchini Uingereza tangu 1673. “Wapresbiteri wengi wa Uingereza walijiunga na madhehebu ya wanaoamini Mungu ni mmoja katika karne ya 18 walipopinga fundisho la Utatu katika mjadala wa kitheolojia uliojadili ikiwa kweli Kristo ni Mungu, na ambao ulizusha machafuko katika Kanisa la Anglikana.” Gazeti hilo linaongeza hivi: “Lakini kwa kuwa sasa mtu anaruhusiwa kuamini kwamba Mungu si Utatu, na makanisa mengi hayajishughulishi na ‘waamini’ wasioshikilia sana imani ya msingi, madhehebu ya wanaoamini Mungu ni mmoja hayahitajiki.”

Mtu Huzidi Kuwa Mfupi Kadiri Anavyozeeka

Kadiri watu wanavyozeeka ndivyo wanavyokuwa wafupi zaidi. Gazeti The Daily Telegraph la Australia linaripoti hivi: “Nguvu za uvutano ndizo husababisha hilo.” Nguvu za uvutano hufanya kimo cha mtu kibadilike siku nzima. Mtu hurudia kimo chake kamili anapolala. Gazeti hilo linasema hivi: “Hata hivyo, miili yetu inapozeeka na kuwa dhaifu, hali hiyo ya kuwa mfupi inadumu. Watu wanapozeeka, misuli na mafuta hupungua. Hiyo ni sehemu ya kiasili ya kuzeeka na inahusiana sana na mabadiliko ya homoni. Mapingili ya uti wa mgongo yanaweza kuanza kudhoofika na kushindwa kufanya kazi na hilo linaweza kufanya uti wa mgongo uwe mfupi kwa zaidi ya sentimeta 2.5 [inchi moja].” Huenda kudhoofika kwa mifupa ndicho kisababishi kikuu cha tatizo hilo.

Kulea Watoto Wanaosema Lugha Mbili

Gazeti Milenio la Mexico City linasema hivi: “Watoto wanapolelewa kwa subira na uangalifu mkubwa, uwezo wao wa kusema lugha zaidi ya moja unaweza kuwafaidi wao, familia zao, na jamii.” Uchunguzi “unaonyesha kwamba watoto wanaosema lugha mbili hufanya vizuri shuleni kuliko wale wanaosema lugha moja.” Nyakati nyingine wazazi huwa na wasiwasi watoto wao wanapochanganya maneno ya lugha mbili katika sentensi moja au wanapokosea na kutumia sheria za sarufi za lugha moja katika lugha ile nyingine. Profesa Tony Cline, mwanasaikolojia ambaye huchunguza jinsi watoto hujifunza lugha anasema: “‘Makosa’ hayo ya kisarufi ni jambo dogo nayo yanaweza kurekebishwa haraka.” Mtoto akifunzwa lugha za wazazi wote wawili kuanzia anapozaliwa, atazifahamu bila tatizo, na baada ya muda, ataweza kuzitofautisha.