Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mbwa Wenye Maisha Mazuri

Gazeti moja (The Sydney Morning Herald) linasema kwamba “wakazi wa Australia hutumia pesa nyingi sana kwa ajili ya wanyama-vipenzi kuliko misaada ya kigeni. Kwa mwaka mmoja wakazi wa Australia hutumia dola bilioni 2.2 kununua majaketi ya kuokolea ya mbwa, mapambo ya almasi na dawa za kusafisha mdomo kwa ajili ya wanyama-vipenzi wao mbali na vitu vingine.” Jason Gram, mwenye duka la wanyama-vipenzi alisema kwamba maoni ya watu kuelekea wanyama-vipenzi yamebadilika katika miaka kumi iliyopita. Alisema: “Zamani mbwa waliishi nje ya nyumba, wakiwa wamejaa viroboto na walitafuna mifupa. Leo wanaishi nyumbani, wanaketi kwenye vitanda vilivyojaa manyoya na wanavishwa mkanda wa shingo wenye vito.” Hata hivyo, alisema kwamba mabadiliko hayo yamewaletea wafanya-biashara faida, kwa kuwa sasa mbwa wanaonwa kuwa sehemu ya familia na hununuliwa bidhaa za bei ghali. Gazeti hilo lilisema kwamba ingawa wanyama-vipenzi fulani “wanatunzwa kana kwamba wana mahitaji au viwango fulani vya urembo kama wanadamu, mbwa hawajui tofauti kati ya mwanasesere wa dola 50 au wa dola 5. Hata hivyo, yaelekea wamiliki wa wanyama hao hufurahi kufanya hivyo ili kuwaonyesha wanyama wao upendo.”

Kelele Zinazosumbua

Mara nyingi watu wanaoishi jijini husumbuliwa sana na kelele zinazopita kiasi. Kulingana na gazeti la Hispania (ABC), Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kwamba kelele hizo zinaweza hata kudhuru afya yao. Mahakama ya Katiba nchini Hispania ilifanya uamuzi wa kufunga kituo kimoja cha burudani kwa shtaka la kukiuka sheria ya jiji inayokataza kuwasumbua wengine kwa kelele. Mahakama hiyo ilionyesha kwamba inatambua madhara ya kelele. Ilisema kwamba “kelele [inayopita kiasi] hukiuka haki ya msingi ya mtu kulinda afya yake ya kiadili na ya kimwili, faragha yake na ya familia na usalama wa makao yake.” Kulingana na mahakama hiyo, kelele inayopita kiasi inaweza “kupunguza uwezo wa kusikia, kusababisha matatizo ya usingizi, matatizo ya kiakili na ya kihisia, shinikizo la damu na kuongeza ujeuri.”

Watoto Wauawa Vitani

Gazeti la Ujerumani (Leipziger Volkszeitung) linaripoti kwamba Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa linakadiria kwamba kati ya watu 800,000 waliouawa katika mapambano ya kikabila nchini Rwanda, 300,000 walikuwa watoto. Inakadiriwa kwamba watoto zaidi ya 100,000 nchini Rwanda wanajitegemea wenyewe. Gazeti hilo linasema kwamba “wao ni maskini hohehahe.”

Kudumisha Uwezo Mzuri wa Akili

Gazeti moja (Toronto Star) lasema kwamba “kujua lugha mbili huwasaidia watu kudumisha uwezo wao wa akili wanapoendelea kuzeeka.” Mwanasaikolojia wa Chuo Kikuu cha York, Ellen Bialystok alipima uwezo wa akili wa watu 104 wenye umri wa kati ya miaka 30 na 59 na watu 50 wenye umri wa miaka 60 hadi 88, wote walikuwa na kiwango kilekile cha elimu na mishahara. Katika kila kikundi, nusu ya washiriki walijua lugha mbili. Kila mmoja wao alipewa mtihani huku muda anaotumia ukipimwa. Gazeti hilo lasema kwamba “watu waliojua lugha mbili walifanya mtihani huo haraka kuliko watu waliojua lugha moja.” Kulingana na Bialystok, kwa kawaida watu wanaojua lugha mbili huwa na uhuru wa kuchagua, na lazima ubongo wao uamue lugha wanayoweza kutumia kujibu. “Mwishowe mazoezi hayo ya akili hulinda ubongo kwa kuzuia uwezo wa kufikiri usidhoofike kadiri mtu anavyozeeka.”

Biblia “Sahihi Kulingana na Maoni ya Watu”

Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba “sala na zaburi zinazopendwa katika Biblia zimebadilishwa kabisa na kuandikwa katika kitabu kipya cha sala cha Waanglikana ili kuwachochea waumini wafikirie masuala kama vile madeni ya nchi zinazoendelea na biashara ya kirafiki.” Katika kitabu hicho (The Pocket Prayers for Peace and Justice), badala ya maneno haya ya Yesu katika Sala ya Bwana, “Utupe mkate wetu wa kila siku,” kinatumia maneno “Unatupa mkate wetu wa kila siku tunapopata mashamba yetu au kupata mshahara mzuri.” Vivyo hivyo, maneno “Hata ingawa ninatembea katika bonde lenye kivuli kizito,” katika Zaburi ya 23, yameondolewa na badala yake wakatia maneno “Hata mzozo mkali ujapozuka sitaogopa, Bwana.” Watu ambao hawapendi mabadiliko wamekiita kitabu hicho chenye kurasa 96 “uwongo na makufuru,” lasema gazeti moja la London (The Daily Telegraph).

Mimba Zinazotolewa kwa Sababu za Kiuchumi

Tofauti na maoni ya wengi, “nchini Australia, mimba zilizo nyingi zinatolewa na [wanawake] walioolewa wenye mapato ya wastani, wala si wasichana matineja waliopotoka kiadili,” laripoti gazeti moja (The Sydney Morning Herald). Kwa kuwa waume wanafanya kazi siku nzima na wake zao wanafanya kazi za muda, mara nyingi uamuzi wa kutokuwa na watoto hufanywa kwa sababu za kiuchumi. “Kupata watoto huathiri kazi na mapato ya mwanamke,” asema Peter McDonald, profesa wa taaluma ya idadi ya watu katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia. “Mshahara [wa wanawake] ambao hawana watoto ni wa juu sana, lakini wakipata mtoto mshahara huo unapungua.” Kulingana na gazeti hilo, mimba 1 kati ya 3 nchini Australia hutolewa.

‘Jueni Rafiki za Watoto Wenu’

Gazeti moja (The New York Times) linasema kwamba huko Marekani “vijana waliosema kwamba angalau nusu ya rafiki zao walizoea kufanya ngono walielekea kuwa walevi mara 31 zaidi, na kuwa wavutaji wa sigara mara 5 1/2 zaidi na wavutaji-bangi mara 22 1/2 zaidi.” Uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Kitaifa cha Uraibu na Matumizi Mabaya ya Dawa za Kulevya katika Chuo Kikuu cha Columbia, ulihusisha wazazi 500 na vijana 1,000 wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17. Joseph A. Califano, Jr., mwenyekiti na msimamizi wa kituo hicho alisema: “Kuna jambo muhimu ambalo wazazi wenye watoto wa umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 wanapaswa kuelewa: hakikisheni kwamba mnajua rafiki wa kiume na wa kike wa watoto wenu.” Aliongezea hivi: “Wazazi wanaozungumzia wakati wa chakula mambo kama vile matembezi ya wavulana na wasichana na matumizi ya dawa za kulevya wanaweza kufaulu kuwasaidia watoto wao wakue bila kutumia dawa za kulevya.”

Vijana Wanajiumiza

Gazeti moja la London (The Times) lasema, “Kati ya nchi za Ulaya, Uingereza ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaojiumiza.” Kila mwaka, vituo vya hali ya dharura na misiba nchini Uingereza hushughulikia visa 150,000 vya watu wanaojiumiza kimakusudi, kama vile kwa kujikata. Vijana hasa ndio wenye tatizo hilo. Gazeti hilo lasema: “Ingawa idadi ya wasichana wanaojiumiza inazidi ile ya wavulana mara 7 kwa moja, idadi ya wanaume imeongezeka maradufu tangu miaka ya 1980.” Inaonekana kwamba watu hujiumiza “ili kukabiliana na maumivu ya kihisia au kwa sababu hisia zao zimekufa ganzi.” Andrew McCulloch wa Shirika la Afya ya Akili anasema kwamba “huenda idadi hiyo ikaonyesha kwamba vijana wetu wanakabili matatizo mengi zaidi, au wanashindwa kushughulikia matatizo hayo.”