Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Lulu za Bahari za Kusini

Lulu za Bahari za Kusini

Lulu za Bahari za Kusini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NEW ZEALAND

“Watengenezaji wa lulu wanahitaji wafanyakazi huko Manihiki,” ndivyo tangazo moja lilivyosema katika gazeti la “Cook Islands News.” Huenda ukajiuliza, ‘Lulu hutengenezwaje? Na Manihiki ni wapi?’

MANIHIKI ni kimojawapo cha visiwa 15 vinavyoitwa Visiwa vya Cook, ambavyo viko kilometa 2,600 kaskazini-mashariki mwa New Zealand. Kulingana na ripoti fulani, mapema katika miaka ya 1970 majaribio ya kutengeneza lulu yalianza huko. Leo biashara ya kutengeneza lulu imefanikiwa katika maeneo mengi ya nyangwa za Manihiki.

Kazi ya kutengeneza lulu hufanywa kwa mkono, lakini ni lazima ifanywe kwa ustadi. Hatua ya kwanza inahusisha kuchagua kwa uangalifu chaza wa aina fulani. Wale wanaochaguliwa hupasuliwa kwa utaratibu, na nyama ya chaza hukatwa kwa kisu. Kisha kidude cha mviringo, au ushanga, pamoja na sehemu ndogo ya utando wa ndani iliyotolewa katika mwili wa chaza mwingine aliye hai huingizwa ndani ya chaza aliyepasuliwa. Kisha wafanyakazi huwarudisha chaza kwenye wangwa na kuwatunza kwa uangalifu, huku wakiondoa miani na kombe.

Pole kwa pole, sehemu hiyo ya utando iliyoingizwa hufunika kidude hicho cha mviringo na kukitandaza kwa kitu changavu kinachoitwa lulumizi. Mwili wa chaza ukipatana na kidude hicho kilichoingizwa, lulu itatokezwa baada ya mwaka mmoja na nusu au miaka miwili. Utaratibu huo wote umefafanuliwa kuwa “upatano wa ajabu kati ya wanadamu na viumbe wengine.”

Thamani ya Lulu

Aina fulani ya lulu inayopatikana katika Pasifiki Kusini ni mojawapo ya lulu zisizopatikana kwa urahisi na zenye thamani zaidi. Aina hiyo ya lulu huwa na rangi nyangavu kama vile, rangi nyeupe ya fedha na rangi nyeusi sana. Nyingine zina rangi ya waridi, ya dhahabu, shaba, shaba-nyekundu, kijani, bluu, zambarau, au kijivu. Hata kuna lulu zenye mchanganyiko wa rangi kama vile kijani na dhahabu, kijani na nyeusi, bluu na nyeusi, na zambarau na nyeusi.

Thamani ya lulu haikadiriwi kwa kutegemea rangi yake. Badala yake, thamani ya lulu hutegemea jinsi rangi ilivyoenea. Mambo mengine ambayo huangaliwa ni ukubwa, umbo, uso, na uangavu wake.

Ukubwa wa lulu hupimwa kwa kutegemea kipenyo chake. Lulu za kawaida zina kipenyo cha kati ya milimeta 8 hadi 12, lakini lulu chache huwa na kipenyo cha milimeta 18 au zaidi. Bei ya lulu haikadiriwi hasa kwa kutegemea ukubwa, hata hivyo, kwa kawaida bei ya lulu hulingana na uzito na ukubwa wake.

Maumbo ya lulu hutofautiana. Kwa kawaida, watu hupenda lulu za duara. Hata hivyo, lulu zenye umbo la chozi au tone la maji hufanyiza vidani na vipuli maridadi. Pia kuna lulu za mviringo ambazo zina pete au mistari iliyobonyea kuizunguka. Vilevile kuna lulu zilizo na umbo la kifungo, yaani, upande mmoja ni duara na mwingine ni bapa. Isitoshe, lulu nyingine zina maumbo yasiyo ya kawaida.

Lulu zisizo na kasoro hazipatikani kwa urahisi nazo huuzwa kwa bei ghali. Lulu nyingi huwa na kasoro kwenye upande wake wa ndani kwani nyingine huwa zimebonyea, zina vinundu, mikunjo, mikwaruzo, au madoa. Kasoro hizo zikiwa chache au ikiwa hazijaenea sana, zinaweza kufichwa zisionekane wakati lulu inapotumiwa kutengeneza vito.

Utavutiwa hasa na mng’ao wa lulu ambao hutegemea unene wa lulumizi. Jambo jingine ni uwezo wa lulu wa kung’aa, ambao huzifanya zivutie. Watu fulani husema kwamba mng’ao wa lulu ndio huvutia wala si rangi, ukubwa, umbo, au uso wake.

Lulu Zinahitaji Kutunzwa

Tofauti na vito vingine vyenye thamani kama vile almasi au rubi, inasemekana kwamba lulu ni “laini.” Zinaweza kukwaruzwa zinapogusana na vito vingine au vitu vigumu. Hivyo, ukiwa na lulu uwe mwangalifu unapozivaa au kuzihifadhi.

Asidi, kama ile inayopatikana katika jasho la mwanadamu, inaweza kuharibu lulu. Pia, zinaweza kuharibiwa na sabuni, marashi, na vipodozi. Mtaalamu mmoja wa vito katika Visiwa vya Cook anapendekeza njia hii ya kusafisha lulu: “Changanya maji na sabuni ya kuosha vyombo katika bakuli ndogo. Koroga maji hayo kwa brashi ya meno kisha uitumie kusugua kwa wororo chombo cha chuma chenye lulu na lulu yenyewe. Suuza kwa maji safi, na uikaushe kwa kitambaa laini.”

Jinsi Lulu Zilivyoonwa Zamani

Lulu ni mojawapo ya vito vilivyoanza kutumiwa zamani na wanadamu kuwa mapambo, na zimesifiwa katika maandishi ya kale. Wakaaji wa Mashariki ya Kati na Asia walizithamini sana, na inaonekana waliziona kuwa zinawakilisha utakato na wema.

Katika Roma ya kale, lulu zilikuwa na thamani sana hivi kwamba ni watu wa vyeo vya juu tu walioruhusiwa kuzivalia. Pliny the Elder, mtaalamu wa vitu vya asili na mwanafalsafa wa karne ya kwanza, alisema kwamba lulu ndicho “kitu bora zaidi ulimwenguni pote.” Na Yesu alipokuwa akitoa mfano kuonyesha thamani ya Ufalme wa mbinguni, alieleza kuhusu “lulu moja” ya thamani kubwa sana hivi kwamba mwanabiashara msafiri aliyekuwa akitafuta lulu nzuri ‘mara moja aliuza vitu vyote alivyokuwa navyo na kuinunua.’—Mathayo 13:45, 46.

Maneno ya Yesu kuhusu lulu huonyesha jinsi lulu zilivyo maridadi na zenye thamani. Tunamshukuru sana Yehova, Muumba wa vito hivyo, kutia ndani vile vinavyopatikana katika Bahari za Kusini!

[Picha katika ukurasa wa 26]

Lulu (zilizoongezwa ukubwa ili kuonyesha sehemu zake)