Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Wanyama Wanavyowalisha na Kuwatunza Watoto Wao

Jinsi Wanyama Wanavyowalisha na Kuwatunza Watoto Wao

Jinsi Wanyama Wanavyowalisha na Kuwatunza Watoto Wao

Na mwandishi wa Amkeni! Nchini Hispania

KWA kawaida wanadamu hutumia miaka 20 hivi kuwalea watoto wao. Lakini wanyama wengi huwalisha na kuwazoeza watoto wao kwa miezi michache tu katika majira ya kiangazi. Hebu tuzungumzie mifano michache inayoonyesha kazi ngumu ambayo wanyama fulani hufanya kila mwaka.

1. Korongo Korongo aliye katika picha hapumziki katika majira ya kiangazi. Kwa kuwa ana makinda wanaohitaji kulishwa, ni lazima aende ziwani kutafuta vyura, samaki wadogo, mijusi, na panzi. Pia, anahitaji kurekebisha kiota chake mara kwa mara. Ndege dume na jike huja na kwenda mchana kutwa. Makinda hao hula chakula kingi sana. Katika majuma machache ya kwanza, wanaweza kula chakula kinacholingana na nusu ya uzito wao! Hata baada ya kujua kuruka, ndege hao wachanga huendelea kuwategemea wazazi wao kwa majuma kadhaa.

2. Duma Kwa kawaida familia ya duma huwa ya mzazi mmoja, kwani duma-jike ndiye anayewatunza watoto. Yeye huwinda kila siku ili apate chakula cha kutosha kwani anahitaji kuwanyonyesha watoto wake ambao kwa kawaida huwa watatu hadi watano. Hilo si jambo rahisi kwa kuwa mara nyingi jitihada zake za kuwinda huambulia patupu. Isitoshe, anahitaji kuwahamisha watoto wake mara kwa mara kwani simba huwawinda. Wanapokuwa na umri wa miezi saba, yeye huanza kuwafunza kuwinda. Hiyo ni kazi ngumu inayochukua mwaka mmoja hivi. Kwa kawaida watoto hao huishi na mama yao kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu.

3. Kibisi Si rahisi kuwatenganisha vibisi na makinda yao. Punde tu baada ya kuanguliwa, wao huvihama viota vyao vinavyoelea na kuanza kuishi migongoni mwa wazazi wao. Makinda hayo hupanda kwenye migongo ya wazazi. Wakiwa humo wao hupata joto na ulinzi huku baba au mama akiogelea. Kila mzazi ana zamu yake ya kubeba makinda na ya kupiga mbizi ili kupata chakula. Ijapokuwa makinda hayo hujifunza haraka kupiga mbizi na kujitafutia chakula, wao huendelea kuwa na uhusiano wa karibu na wazazi kwa muda fulani.

4. Twiga Ni vigumu sana kwa twiga kuzaa zaidi ya mtoto mmoja kwa wakati mmoja. Si vigumu kuelewa kinachosababisha hali hiyo. Twiga aliyetoka tu kuzaliwa kama yule aliye katika picha anaweza kuwa na uzani wa kilo 60 hivi na urefu wa meta mbili! Baada ya saa nzima tangu kuzaliwa, twiga mchanga huanza kutembea na kunyonya maziwa ya mama yake. Ijapokuwa twiga mchanga huanza kula nyasi punde tu baada ya kuzaliwa, yeye huendelea kunyonya kwa miezi tisa. Anapokabili hatari, yeye hujificha katikati ya miguu ya mama yake kwani mama hutumia miguu yake yenye nguvu kupiga adui mateke.

5. Mdiria Ni lazima mdiria awe na ustadi na awe mteuzi anapovua samaki ili alishe makinda yake. Wataalamu wa ndege wamegundua kwamba baada tu ya makinda kuangauliwa, wazazi wote wawili huwalisha kwa samaki wadogo walio na urefu wa sentimeta moja hadi sentimeta mbili. Ndege hao hubeba samaki kwa midomo yao huku kichwa cha samaki kikiwa nje ya mdomo wao. Hilo hufanya iwe rahisi kwa makinda kula samaki kwani wanaweza kuwameza kwa urahisi kuanzia kichwani. Kadiri wanavyokua, mdiria huwalisha kwa samaki wakubwa zaidi. Isitoshe, ndege hao huwalisha makinda kwa ukawaida zaidi. Mwanzoni kila kinda hulishwa baada ya kila dakika 45 hivi. Lakini wanapokuwa na umri wa siku 18 hivi, makinda huwa na hamu kubwa ya kula, hivyo wao hulishwa samaki baada ya kila dakika 15! Kinda aliye katika picha amekihama kiota na karibuni ataanza kujivulia samaki. Kufikia sasa huenda ukafikiri kwamba wazazi watapumzika kutokana na kazi ya kuwatunza makinda. Lakini sivyo hata kidogo! Mara nyingi wao huanza tena kazi ya kuwalisha na kuwatunza makinda wengine katika majira hayohayo ya kiangazi.

Bila shaka hatujui mambo mengi kuhusu jinsi wanyama wanavyowatunza watoto wao. Hata hivyo, kadiri wataalamu wanavyogundua mambo mapya, ndivyo inavyodhihirika kwamba wanyama wana hisia yenye nguvu sana ya kumhangaikia mtoto. Ikiwa Mungu aliwaumba wanyama kwa njia hiyo, ni wazi kwamba anawatazamia wazazi wawalishe na kuwatunza watoto wao kwani wanahitaji mambo hayo.