Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sungura na Vyura Wavamia Bara

Sungura na Vyura Wavamia Bara

Sungura na Vyura Wavamia Bara

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

UWANJA wa pigano ni eneo lililoharibiwa na lisilo na rutuba. Sasa eneo hilo lililokuwa na mimea mingi sana limejaa mashimo yenye kina kirefu na mizoga ya wapiganaji. Askari hao hawana mavazi ya vita yanayowawezesha kujificha kwenye mimea, hawana wala viatu wala kofia, bali wamevalia makoti yenye manyoya na wana meno makali. Hao ni sungura wa mwitu waliovamia Australia.

Sungura Kila Mahali

Sungura kutoka Ulaya walifika kwenye ncha ya kusini-mashariki ya Australia mnamo 1859. Walikuwa wameletwa nchini ili kuwafurahisha wawindaji wa eneo hilo, lakini baada ya muda walianza kuwindwa ili kudhibiti idadi yao.

Ijapokuwa sungura wa Ulaya walichukua miaka 900 kuvamia na kujaza eneo lote la nchi ya Uingereza, iliwachukua miaka 50 tu kujaza sehemu ya nchi ya Australia inayozidi nusu ya eneo lote la Ulaya. Kwa kuwa sungura wa kike aliyekomaa angeweza kuzaa watoto 40 kwa mwaka, sungura hao waliongezeka haraka na kujaa katika eneo la kilometa 100 hivi kila mwaka. Ripoti moja ya Idara ya Sayansi ya Maeneo ya Mashambani inasema: “Hilo lilikuwa ongezeko la haraka zaidi ulimwenguni la wanyama wanaovamia maeneo.” Sungura hao walisababisha hasara kubwa.

Sungura wanapovamia eneo fulani, wao hula chakula cha wanyama wa eneo hilo na kuingia katika mashimo ya wanyama hao. Inasemekana kwamba wamesababisha kutoweka kwa jamii nyingi za wanyama. Pia inadaiwa kwamba wameangamiza misitu. Mtafiti mmoja anasema kwamba “sungura hula miche ya miti, na hivyo miti iliyokomaa inaponyauka hakuna miti mingine inayokua badala yake.” Wanapovamia kisiwa kidogo, wanaweza kusababisha uharibifu mkubwa. Ripoti ya Idara ya Sayansi ya Mali za Asili inasema hivi: “Kufikia mwaka wa 1936, sungura waliokuwa wameletwa kwenye Kisiwa cha Laysan katika mwaka wa 1903, walikuwa wameangamiza jamii tatu za ndege na jamii 22 kati ya jamii 26 za mimea. . . . Katika mwaka wa 1923, kisiwa hicho kilikuwa na mchanga usio na rutuba na miti michache midogo.”

Kutumia Silaha za Maangamizi Makubwa

Nchini Australia, sungura walipigwa risasi, wakanaswa katika mitego, na kutiliwa sumu. Ua maarufu wenye urefu wa kilometa 1,830 ulijengwa kuvuka jimbo lote la Western Australia ili kuwazuia sungura hao. * Hata hivyo, jitihada hizo zote hazikuweza kuzuia jeshi hilo la wavamizi.

Kisha katika mwaka wa 1950, sungura hao walianza kushambuliwa kwa silaha ya kibiolojia, yaani, virusi vya myxomatosis. Virusi hivyo vilipunguza sana idadi ya sungura, ambao wakati huo walikadiriwa kuwa milioni 600. Virusi hivyo huenezwa na mbu na viroboto navyo huwaua sungura tu. Sungura milioni 500 walikufa kutokana na virusi hivyo katika kipindi cha miaka miwili tu. Hata hivyo, muda si muda sungura wakawa sugu na hawakuathiriwa tena na virusi hivyo. Sungura waliosalia walizaana sana. Hivyo, kufikia miaka ya 1990, idadi ya sungura iliongezeka kufikia milioni 300 hivi. Suluhisho lingine lilihitajiwa.

Faida na Hasara

Katika mwaka wa 1995, silaha ya pili ya kibiolojia, yaani ugonjwa unaosababisha sungura avuje damu, ilitumiwa dhidi ya sungura nchini Australia. Ugonjwa huo ulizuka kwa mara ya kwanza nchini China katika mwaka wa 1984. Kufikia mwaka wa 1998, ugonjwa huo ulikuwa umeenea hadi Ulaya na muda mfupi baadaye sungura milioni 30 wa kufugwa wakafa kutokana nao huko Italia. Ugonjwa huo uliathiri sana biashara ya sungura huko Ulaya lakini ukawafaidi wakulima wa Australia kwani sungura milioni kumi waliangamizwa katika kipindi cha miezi miwili ya kwanza baada ya ugonjwa huo kuenezwa. Inaonekana kwamba virusi vya ugonjwa huo huwaathiri sungura tu, ambao hufa saa 30 hadi 40 baada ya kuambukizwa bila kuonyesha dalili zozote za kuugua. Kufikia mwaka wa 2003, ugonjwa huo ulikuwa umepunguza idadi ya sungura katika maeneo mengi makavu ya Australia kwa asilimia 85 au zaidi.

Kwa kuwa hakukuwa na sungura wa kula mimea, mimea ya okidi katika mbuga moja ya kitaifa huko South Australia iliongezeka mara nane kwa kipindi kisichozidi miaka mitano. Katika sehemu nyingine za jimbo hilo, “mimea mingi imesitawi mapema . . . katika maeneo ambako ugonjwa huo ulizuka mara kadhaa,” linasema gazeti Ecos. Wanyama wawindaji walioletwa katika maeneo hayo, kama vile mbweha na paka wa mwituni, wamepungua pia kwa sababu ya ukosefu wa sungura. Wataalamu na wakulima wamefurahishwa na silaha hiyo mpya kwani sungura wamekuwa wakisababisha hasara ya karibu dola milioni 600 kwa mwaka nchini Australia. Hata hivyo, bado haijulikani jinsi ugonjwa huo utakavyowaathiri sungura sugu wa Australia katika siku zijazo.

Mwokozi Awa Msaliti

Ingawa huenda ikaonekana kwamba wanasayansi wamefaulu kuwakomesha sungura wa mwituni, yaelekea wameshindwa kuwakomesha chura fulani ambao wamevamia hivi majuzi. Sawa na sungura, chura hao waliletwa nchini Australia. Kwa nini?

Mapema katika karne ya 20, jamii mbili za mbawakawa wanaovamia miwa waliathiri sana biashara ya miwa huko Australia, ambayo kwa sasa inailetea nchi hiyo dola bilioni mbili kwa mwaka. Katika mwaka wa 1935, wakulima wa miwa walimwona chura anayeitwa Bufo marinus, ambaye anatoshana na ngumi, kuwa mwokozi kwa sababu yeye hula sana mbawakawa. Ijapokuwa wanasayansi fulani walitilia shaka jambo hilo, vyura hao walisafirishwa kutoka Amerika Kusini, wakapitishwa Hawaii, na hatimaye kupelekwa kwenye mashamba ya miwa ya Queensland.

Vyura hao walipopelekwa huko, walipuuza mradi wao wa kuwavamia mbawakawa, na kuwa wasaliti. Vyura hao huwa na sumu katika kila hatua ya maisha yao, tangu yai hadi wanapokomaa. Wanapoendelea kukua, tezi za pekee hukua chini ya ngozi yao, na wanapokasirishwa wao hutokeza sumu hatari sana iliyo kama maziwa kupitia tezi hizo. Inasemekana kwamba vyura hao huua mijusi, nyoka, mbwa-mwitu, na hata mamba ambao huwameza. Wao huzaana sana na kufikia sasa wamesambaa zaidi ya kilometa 900 kutoka mahali walipowekwa mara ya kwanza. Idadi ya vyura hao wa Australia inazidi kwa mara kumi hivi idadi ya wale wa Venezuela, nchi ambako walitoka. Sawa na ilivyokuwa katika pigo linalosimuliwa katika Biblia, vyura hao huvamia mashamba na nyumba, nao huingia katika vyoo. Vyura hao wanaenea kilometa 30 kwa mwaka, nao wamefika katika Mbuga ya Kitaifa ya Kakadu katika Eneo la Kaskazini ambayo imeorodheshwa katika mirathi ya ulimwengu. Inasemekana eneo hilo linawafaa sana vyura. Serikali ya Australia imetumia mamilioni ya dola kufanya utafiti ili kukabiliana na vyura hao, lakini bado mbinu bora ya kuwazuia haijavumbuliwa. Pambano linaendelea, na kufikia sasa vyura wanawashinda wanadamu.

Ni Nini Kinachosababisha Mapambano?

Katika mazingira ya asili, idadi ya viumbe hudhibitiwa kiasili. Lakini wakiondolewa katika mazingira yao ya asili, hata viumbe ambao si hatari wanaweza kuongezeka haraka na kusababisha madhara.

Watu wa kwanza kuhamia Australia kutoka Ulaya hawakutambua kwamba wanyama na mimea iliyoingizwa nchini humo ingesababisha madhara makubwa. Ni kweli kwamba jamii nyingi za wanyama na mimea iliyoingizwa imeleta manufaa. Kwa sasa Waaustralia wanategemea hasa jamii za wanyama na mimea iliyoingizwa nchini kama vile, kondoo, ng’ombe, ngano, mpunga, na mimea mingine. Hata hivyo, visa hivyo vya sungura wa mwituni na vyura huonyesha kwamba wanadamu wanapaswa kufikiria kwa uzito kabla ya kuvuruga mpangilio tata wa asili uliopo duniani.

[Maelezo ya Chini]

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mwokozi aligeuka kuwa msaliti—vyura wanaendelea kuenea

[Hisani]

U.S. Geological Survey/photo by Hardin Waddle

[Picha katika ukurasa wa 26]

Wavamizi wenye kiu kwenye kidimbwi cha maji katika Kisiwa cha Wardang, katika Ghuba ya Spencer, huko South Australia

[Hisani]

By courtesy of the CSIRO

[Picha katika ukurasa wa 25 zimeandaliwa na]

Rabbits: Department of Agriculture, Western Australia; toad: David Hancock/© SkyScans