Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wafanye Watoto Wako Wafurahie Kusoma

Kulingana na gazeti Reforma la Mexico, mtaalamu mmoja anayeitwa Beatriz González Ortuño anasema hivi: “Imeonekana kwamba ikiwa wazazi ni wasomaji wazuri basi watoto watawaiga.” Inafaa kuwachochea watoto kupenda kusoma hata kabla hawajaanza kutofautisha vokali, kwani wana uwezo mkubwa wa kujifunza. Kwa mfano, unaweza kuwasomea hadithi ambazo zitawachochea kufikiri. Gazeti hilo linapendekeza ufanye mambo yafuatayo ili watoto wafurahie kusoma: “Keti nao. . . . Waache wafungue kurasa za kitabu mnachosoma, wakukatize wanapotaka, na kuuliza maswali. . . . Waombe wakueleze kuhusu vitu na watu walio katika hadithi mnayosoma. Jibu maswali yao yote. . . . Husianisha mambo yaliyo katika kitabu na maisha ya watoto.”

Tembo Waathiriwa na Pilipili

Tembo walio katika mbuga za wanyama za Afrika wamesababisha matatizo mengi kati ya wahifadhi wa mazingira na wakulima. Kujenga nyua, kuwasha moto, na kelele za ngoma hazijawazuia tembo wasitoke kwenye mbuga hizo. Tembo wanaozurura wameharibu mimea mara nyingi na hata kuwauwa watu. Hatimaye kitu cha kuwazuia wasitoke kimepatikana, yaani, mpilipili. Gazeti The Witness la Afrika Kusini linaripoti kwamba mmea huo unapopandwa karibu na mpaka wa mbuga, tembo hugeuka wakiwa “wameudhika kwa sababu ya harufu ya mmea huo.” Maafisa wa mbuga za wanyama sasa hawahitaji “kuwarudisha tembo ndani ya mbuga,” nayo mimea ya wakulima haiharibiwi sana. Watu wanaweza kuchuma pesa nyingi kwa kuzalisha pilipili.

Ujumbe Mfupi wa Simu Hukatiza Usingizi

Gazeti Apotheken Umschau la Ujerumani linaripoti kwamba “ujumbe mfupi wa simu hukatiza usingizi wa vijana.” Katika uchunguzi uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Leuven, Ubelgiji, vijana 2,500 walio na umri wa miaka 13 hadi 16, waliulizwa wao huamshwa mara ngapi na ujumbe mfupi wa simu za mkononi, na wao huwa wachovu kadiri gani katika pindi mbalimbali. Asilimia 10 kati yao walisema kwamba wao huamshwa angalau mara moja kwa juma. Asilimia 3 kati yao waliamshwa kila usiku. Mmoja wa watafiti waliofanya uchunguzi huo, anasema kwamba “uchunguzi huo unaonyesha simu za mkononi zinaweza kuathiri sana usingizi wa vijana wengi.” Gazeti Apotheken Umschau linapendekeza hivi: “Wazazi wanapaswa kuhakikisha kwamba watoto wao wamezima simu za mkononi usiku.”

Jinsi Samaki Wanavyoogelea Dhidi ya Mkondo wa Maji

Uchunguzi uliochapishwa katika gazeti Science ulionyesha kwamba trauti wa mtoni na samaki wengine huogelea katika mikondo ya maji yanayopita kasi sana kuzunguka vitu visivyosonga vilivyomo majini, ili wasitumie nguvu nyingi kuogelea na hivyo kuwa na nguvu za kutosha kuogelea dhidi ya mkondo wa maji. Gazeti New Scientist linasema kwamba kwa kujipinda-pinda na kufuata mikondo hiyo ya maji, samaki hao huhifadhi nguvu nyingi sana hivi kwamba hawatumii misuli yao mikuu ya kuogelea. George Lauder, mtaalamu wa misuli katika Chuo Kikuu cha Harvard, na ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa uchunguzi huo anaeleza kwamba, “mbinu hii inahitaji kiasi kidogo sana cha nguvu ili kusonga kupitia maji yenye msukosuko.” Gazeti New Scientist linasema kwamba “samaki hao hujipinda-pinda kama mabawa ya ndege ili wasukumwe na maji hayo yanayopita kasi, au kama matanga ya meli yanavyojipinda ili kushika upepo.”

Wazee Si Mzigo

Ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Australia ya Uchunguzi wa Familia inasema kwamba “badala ya kufikiria tu gharama za kuwatunza wazee, inafaa kufikiria msaada wanaotoa na kiasi cha pesa wanazookoa wanapofanya kazi bila kupata mshahara. Kwa kufanya kazi nyingi wao hutupa msaada ambao hatuwezi kuupata kutoka kwa wafanya-kazi wa kuajiriwa.” Uchunguzi huo unaonyesha kwamba “Waaustralia walio na umri wa zaidi ya miaka 65 husaidia nchi kuokoa karibu dola bilioni 39 za Australia [dola bilioni 27 za Marekani] kwa mwaka wanapofanya kazi ya kuwatunza wengine bila malipo.” Wao hujitolea kufanya kazi kama vile kutunza watoto na watu wazima walio wagonjwa, na kazi nyingine za nyumbani. Wachunguzi hao wanasema kwamba kufanya kazi bila kulipwa “kunaweza kuunganisha jamii.” Thamani yake haiwezi kupimwa kwa pesa.

Kitabu Kilichochapishwa Zamani

Shirika la Utangazaji la Uingereza linaripoti kwamba kitabu cha zamani zaidi kuchapishwa ambacho bado kipo sasa kinapatikana katika Maktaba ya Uingereza. Kitabu cha Wabuddha kinachoitwa The Diamond Sutra kina tarehe ya mwaka 868 W.K. na kilipatikana ndani ya pango fulani huko Dunhuang, China, katika mwaka wa 1907. Ripoti hiyo inasema kwamba “hiyo ni hati ya kukunja ya rangi ya kijivu yenye maandishi ya Kichina, ambayo imezungushwa kwenye kijiti cha mbao.” Inasemekana kwamba kitabu hicho pamoja na vitu vingine vilivyopatikana nacho, vilikuwa “katika maktaba iliyokuwa ndani ya pango hilo wapata mwaka wa 1000 W.K.” Hati hiyo ya kukunja ilichapishwa mamia ya miaka kabla uchapishaji haujaanza katika Ulaya, lakini shirika hilo la utangazaji linaripoti kwamba “kufikia wakati huo tayari utengenezaji wa karatasi na uchapishaji ulikuwa umesitawi nchini China.”

Kelele Hupunguza Uwezo wa Mtu wa Kuitikia

Gazeti The Toronto Star linasema hivi: “Kunapokuwa na kelele nyingi mtu huitikia polepole zaidi.” Hayo ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Duane Button katika Chuo Kikuu cha Memorial, huko Newfoundland, Kanada. Katika uchunguzi huo watu walifanya kazi zilizowahitaji watumie nguvu na akili huku wakisikiliza kelele za viwango tofauti-tofauti. Aligundua kwamba kelele za ofisini za kiasi cha desibeli 53 hupunguza uwezo wa mtu wa kuitikia kwa asilimia 5, huku kelele kama zile za viwandani za kiasi cha desibeli 95 hupunguza uwezo wake wa kuitikia kwa asilimia 10. Ingawa kuna tofauti ndogo sana katika muda unaopita kabla ya watu kuitikia, ripoti hiyo inaonyesha kwamba “tofauti hizo ndogo zinaweza kuathiri mtu sana anapoendesha gari.” Button anasema kwamba mtu akikawia kuitikia hata kwa muda usiozidi sekunde moja, anaweza kusababisha msiba.

Makanisa Yanauzwa

Dayosisi Kuu ya Kanisa Katoliki huko Boston, Marekani, imetangaza kwamba itafunga parokia 65 kati ya parokia zake 357 ambazo ni asilimia 20 hivi ya parokia zote. Makanisa 60 na majengo mengine 120 ya kanisa hilo yatauzwa pia. Kulingana na gazeti The New York Times, mabadiliko hayo “yamesababishwa kwa kiasi fulani na kupungua kwa hudhurio na matatizo mengi ya kiuchumi ambayo yanatokana na kashfa za kingono zinazowakabili makasisi.” Gazeti hilo linamnukuu R. Scott Appleby, msimamizi wa Kituo cha Cushwa cha Uchunguzi wa Ukatoliki wa Marekani katika Chuo Kikuu cha Notre Dame, akisema kwamba “pesa nyingi za dayosisi kuu zimetumiwa katika kashfa hiyo” hivi kwamba haiwezi “kushughulikia parokia zote.”