Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Hasira Hudhoofisha Moyo

Gazeti Daily News la New York linaripoti kwamba “wanaume ambao huwa na hasira kali na huwashambulia watu, wanakabili uwezekano mkubwa wa kuwa na mpigo usio wa kawaida wa moyo.” Watafiti waligundua kwamba wanaume wanaokasirika upesi, wanaowashambulia wengine kwa maneno makali wanapoudhiwa, au wanaokasirika sana wanapochambuliwa, wanakabili uwezekano wa asilimia 30 wa kuwa na tatizo la mpigo usio wa kawaida wa moyo kuliko wanaume wasio na mazoea hayo. Elaine Eaker, ambaye anasimamia uchunguzi huo, anasema hivi: “Watu fulani wanaamini kwamba unaweza kuepuka madhara ya kiafya ya kuwa na hasira kwa kuionyesha badala ya kuidhibiti. . . . Lakini uchunguzi huo umeonyesha kwamba hilo si kweli, kwani wanaume waliochunguzwa walikabili hatari kubwa ya kuwa na mpigo usio wa kawaida wa moyo na vilevile hatari ya kufa kutokana na sababu nyingine nyingi.”

Ndoa na Talaka Nchini Uingereza

Gazeti Daily Telegraph la London linaripoti kwamba nchini Uingereza “thuluthi moja ya waseja wanasema kwamba ‘haielekei hata kidogo’ kwamba watafunga ndoa.” Jenny Catlin, mtafiti wa shirika la Mintel International Group, anasema hivi: “Kwa wazi, hilo huonyesha kwamba maoni ya watu kuhusu ndoa yamebadilika.” Kisha anaongeza: “Sasa ni jambo linalokubalika zaidi kuishi na mwenzi na kupata watoto, bila kufunga ndoa.” Kwa kuwa gharama za arusi zinaendelea kuongezeka, na sasa zimefikia dola 28,600, watu wengi sasa wanafikiria kufanya arusi katika nchi nyingine. Zaidi ya asilimia 10 ya wenzi Waingereza huamua kufanya harusi nje ya nchi yao. Kwa sababu sherehe hizo huhudhuriwa na wageni wachache sana na gharama za kutayarisha chakula huwa ndogo, huenda mtu akatumia thuluthi moja tu ya kiasi cha pesa ambazo angetumia ikiwa angefanya harusi nchini kwao. Huku idadi ya harusi ikipungua, idadi ya talaka inaongezeka. Gazeti Telegraph linasema hivi: “Leo idadi ya wanawake wazee ambao wametalikiwa imezidi mara tano ile ya miaka 30 iliyopita, na inaonekana kwamba itazidi kuongezeka.”

Watoto Wanaotendewa Vibaya Nchini Mexico

Kulingana na Idara ya Sheria ya Mexico City, “msichana 1 kati ya kila wasichana 8 na mvulana 1 kati ya kila wavulana 10 hutendewa vibaya kingono katika Mexico City,” laripoti gazeti El Universal. Idara hiyo inasambaza vijitabu vinavyowaonya wazazi kuhusu kutendewa vibaya kingono na kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa iwapo jambo hilo limetukia. Mapendekezo hayo yanatia ndani mambo yafuatayo: (1) Mwamini na umtegemeze mtoto wako anapokuambia kwamba ametendewa vibaya kingono. (2) Mweleze mtoto kwamba si yeye aliyesababisha hali hiyo. (3) Mweleze mtoto kwamba jambo ambalo ametendewa ni kinyume cha sheria na kwamba mnahitaji kuwajulisha polisi ili asitendewe hivyo tena.

Kuondoa Michoro ya Chanjo

Gazeti Vancouver Sun la Kanada linasema “uchunguzi fulani umeonyesha kwamba asilimia 80 hadi 90 ya watu walio na michoro ya chanjo hutaka iondolewe baadaye maishani.” Mtaalamu mmoja wa ngozi anasema hivi: “Kwa kuwa idadi ya michoro ya chanjo ambayo watu huchorwa inazidi kuongezeka, watu wengi zaidi wanataka waondolewe michoro hiyo.” Dan, mwenye umri wa miaka 27, ambaye alikuwa na mchoro wa chanjo wa rangi ya kijani, ni mmoja kati ya watu hao. Anasema hivi: “Mchoro huu haupatani na maisha yangu ya sasa.” Ijapokuwa kuna matibabu ya kisasa ya kuondoa michoro ya chanjo kwa kutumia miale ya leza, matibabu hayo husababisha maumivu mengi, hugharimu sana, nayo huchukua muda mrefu. Gazeti hilo linasema kwamba “kuondoa mchoro mdogo tu wa chanjo kunaweza kugharimu dola 1,400 za Kanada.” Kisha linaongeza hivi: “Huenda isiwezekane kuondoa michoro ya chanjo ya kisasa yenye rangi mbalimbali, hasa ikiwa ni mikubwa sana.”

Fueli Hatari

Gazeti Down to Earth la New Delhi, India, linasema kwamba “katika nchi zinazoendelea moshi unaosababishwa na mioto inayotumiwa kupika ndani ya nyumba huua mtu mmoja kila sekunde 20. Idadi hiyo inapita idadi ya watu wanaokufa kutokana na malaria, na ni sawa na idadi ya watu wanaokufa kutokana na ukosefu wa maji safi na mfumo wa kuondoa uchafu.” Kuwasha moto kwa kutumia makaa ya mawe, kuni, au samadi, na ukosefu wa hewa ya kutosha ndani ya nyumba huwahatarisha sana watu. Uchafuzi huo pia umehusianishwa na kansa ya mapafu, ugonjwa wa pumu, kifua kikuu, na mkamba. Wataalamu kutoka katika shirika moja la utafiti wanasema kuwa watu walio maskini sana hivi kwamba hawawezi kutumia fueli ambayo haichafui hewa, wanaweza kupunguza hatari ya kuathiriwa kwa asilimia 80 hivi iwapo watatumia bomba linalofaa la kutolea moshi. Kati ya watu milioni 1.6 wanaokufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba, milioni moja hivi ni watoto.

Wafanyakazi Waliopita Umri wa Kustaafu

Gazeti The Globe and Mail linaripoti kwamba Wakanada wengi waliofikisha umri wa kustaafu wa miaka 65, wangali wanafanya kazi. Idadi ya raia walio wazee imeongezeka kwa asilimia 11 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, lakini idadi ya wazee wanaofanya kazi imeongezeka kwa asilimia 20 hivi. Kwa nini watu wengi wanaahirisha kustaafu? Mkaguzi wa takwimu wa Kanada, Doreen Duchesne, anasema kwamba “siku hizi watu wana afya na wanaishi kwa muda mrefu.” Pia inasemekana kwamba mahitaji ya kifedha na kuchoshwa na maisha kunachangia hali hiyo. Kulingana na ripoti hiyo, asilimia 6 ya watu walio na umri unaozidi miaka 80 bado wanafanya kazi. Wengi wao hujishughulisha hasa na kilimo, huku baadhi yao wakifanya kazi za ofisini na biashara.

Moshi Umelifunika Bara la Ulaya

Gazeti El País la Hispania linaripoti kwamba sasa idadi ya watu wanaovuta sigara katika Muungano wa Ulaya imefikia asilimia 40. Ugiriki ndiyo nchi yenye wavutaji wengi zaidi wa sigara barani Ulaya, kwani asilimia 44 ya watu huko huvuta sigara. Kila mwaka Ugiriki huzalisha tani 40,000 za tumbaku, na hilo huifanya iwe nchi inayozalisha tumbaku kwa wingi zaidi huko Ulaya. Ureno ndiyo nchi iliyo na wavutaji wachache zaidi wa sigara kutia ndani watu wanaovuta sigara mara chache tu, kwani idadi yao inazidi asilimia 29. Hilo linashangaza kwani sigara nchini Ureno huuzwa kwa bei ya chini sana kuliko katika nchi nyingine za Muungano wa Ulaya. Tangu mwaka wa 1982, Ureno ilipiga marufuku matangazo ya biashara ya sigara na uvutaji wa sigara katika maeneo ya umma, na huenda hilo ni mojawapo ya sababu zinazofanya kuwe na idadi ndogo ya watu wanaovuta sigara.

Kitabu Ambacho Kimetafsiriwa Zaidi

Biblia bado ndicho kitabu ambacho kimetafsiriwa zaidi ulimwenguni. Biblia nzima au sehemu zake zimetafsiriwa katika lugha 2,355 kati ya lugha 6,500 hivi zinazotumiwa leo. Kufikia sasa Biblia imetafsiriwa katika lugha 665 za Afrika, lugha 585 za Asia, lugha 414 za Oceania, lugha 404 za Amerika ya Latini na Karibea, lugha 209 za Ulaya, na lugha 75 za Amerika ya Kaskazini. Kwa sasa shirika la Muungano wa Vyama vya Biblia linasaidia miradi ya kutafsiri Biblia katika lugha 600 hivi.