Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vazi Rasmi la Korea Linaloitwa Hanbok

Vazi Rasmi la Korea Linaloitwa Hanbok

Vazi Rasmi la Korea Linaloitwa Hanbok

Na mwandishi wa Amkeni! katika Jamhuri ya Korea

WAKOREA hawavai nguo ili kujifunika tu. Kwa mfano, fikiria vazi lao la kitamaduni linaloitwa hanbok.

Mshono wa Kipekee

Vazi la hanbok lina sehemu mbili, blauzi fupi na sketi ndefu. * Nyakati nyingine urefu wa sketi huwa mara nne zaidi ya urefu wa blauzi. Kwa hiyo, hata mwanamke mfupi ataonekana kuwa mrefu anapolivaa.

Vazi la hanbok lina mikunjo isiyotambulika kwa urahisi. Mikono ya blauzi inafanana na mabawa, nayo sketi huanzia kifuani hadi chini. Kifuani kuna mshipi wenye fundo la kipekee na sehemu mbili za mshipi huo huning’inia kutoka upande wa mbele wa blauzi hadi miguuni. Mavazi mengi ya hanbok yana mapambo maridadi ya miraba na maua yanayoshonelewa shingoni na kwenye sehemu za mwisho za mikono ya blauzi, na pia kwenye sketi. Naam, mshono wa vazi hilo na rangi zake nyingi zinalifanya liwe maridadi sana!

Vazi la Majira Yote

Uzuri wa vazi hilo ni kwamba linaweza kuvaliwa katika hali mbalimbali. Kwa kuwa kwa kawaida vazi hilo hutengenezwa kwa nyuzi za asilia, linaweza kutumiwa wakati wa majira yoyote. Kwa mfano, yule anayelivaa vazi la hanbok ambalo limetengenezwa kwa nyuzi za asilia kama vile upupu au katani, hatasikia joto sana wakati wa majira ya joto, ijapokuwa linafunika karibu mwili wote. Vazi lililotengenezwa kwa nyuzi za aina nyingine huhifadhi joto, nalo linafaa sana katika majira ya baridi kali.

Vazi la hanbok ni lenye kustarehesha pia. Vazi hilo halikushonwa hivyo kwa sababu ya mtindo, bali kwa sababu karne nyingi zilizopita farasi walitumiwa sana katika eneo hilo. Gazeti Culture & I linasema: “Vazi hilo lilibuniwa ili litumiwe wakati wa baridi kali na wakati wa uwindaji na shughuli nyingine za watu wanaohama-hama.” Kwa hiyo, wapanda-farasi Wakorea hawakuvaa mavazi yaliyowabana. Naam, Wakorea wanaofurahia kuvaa hanbok leo wanapaswa kuwashukuru mababu zao kwa mavazi hayo yenye kustarehesha!

Jambo jingine lenye kuvutia kuhusu vazi hilo ni kwamba rangi zake zina maana mbalimbali kupatana na mapokeo ya kale. Zamani, mara nyingi watawala Wakorea walivalia mavazi yenye rangi za kuvutia, nao wakulima walivalia hasa mavazi meupe. Mwanamke mseja aliweza kutambuliwa kwa mavazi yenye rangi nyekundu na manjano. Baada ya kuolewa, rangi ya vazi lake la hanbok lilionyesha cheo cha mumewe. Siku hizi, mama ya bibi-arusi anatarajiwa kuvalia rangi nyekundu hafifu, na mama ya bwana-arusi kwa kawaida huvalia vazi la bluu. Mavazi hayo huwatambulisha kwa urahisi.

Vazi la Hanbok la Siku Hizi

Baada ya Vita vya Korea (1950-1953), jitihada zilifanywa ili kufanya maisha yawe ya kisasa. Kwa hiyo, katika miaka ya 1970 watu walianza kuvalia mavazi ya nchi za Magharibi badala ya vazi la hanbok. Hivyo, vazi hilo likawa linavaliwa tu kwenye arusi, sikukuu, na pindi nyingine za pekee.

Hata hivyo, hivi karibuni watu wameanza kuvalia vazi hilo tena. Kwa mfano, mwaka wa 1996, Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi ilitangazwa kuwa “siku ya kuvalia hanbok,” ili kuwachochea watu walipende vazi hilo tena. Washonaji walibuni mitindo mipya ya hanbok ili kuwavutia hasa vijana. Ni wazi kwamba watu hupata uradhi fulani wanaporudia tamaduni za zamani, kwa kuwa kwa mara nyingine tena vazi la hanbok la kisasa linapendwa sana. Wakati huu ambapo watu wengi hupenda mitindo inayovutia kimahaba, vazi la hanbok linafurahisha kwa sababu ni maridadi na lenye kiasi.—1 Timotheo 2:9.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Ijapokuwa kuna vazi la hanbok la wanaume na wanawake, tutazungumzia lile la wanawake.