Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nilikuwa Kiongozi wa Dini ya Wakickapoo

Nilikuwa Kiongozi wa Dini ya Wakickapoo

Nilikuwa Kiongozi wa Dini ya Wakickapoo

SIMULIZI LA BOB LEE WHITE, SR.

Nilizaliwa mwaka wa 1935 katika kibanda kidogo cha Wahindi wa Amerika kilichoezekwa kwa maganda ya miti na matete, huko McLoud, Oklahoma, Marekani. Katika lugha ya Wakickapoo * ninaitwa Pa-ME-Ton-Wa, jina linalomaanisha “Maji Yanayopita.” Nilifundishwa dini ya Wahindi wa Amerika nilipokuwa mvulana mdogo. Kwa nini?

BABA ya mamangu, kama vile baba yake, alikuwa kiongozi wa dini wa kabila moja la Wakickapoo, ambalo ni la ukoo wa Maji wa Wahindi wa Amerika huko Oklahoma. Alipokufa bila kuwa na mwana, viongozi 12, au wazee, waliamua kwamba mwana wa kwanza wa binti mkubwa wa kiongozi huyo aliyekufa achukue mahali pake. Mimi ndiye niliyekuwa mwana huyo.

Nilivyopata Kuwa Kiongozi wa Dini

Kwa kawaida kiongozi mpya angeanza kazi hiyo akiwa na umri wa miaka 30 baada ya kipindi cha kufunga, ambapo angeona maono au kuelimishwa kwa njia nyingine jinsi ya kufanya shughuli hizo za kidini. Tangu utotoni nilifundishwa dini ya Wakickapoo. Nilirithi mavazi ya kidini na ME-shon, yaani, kifurushi kitakatifu. Kifurushi hicho ambacho nyakati nyingine kiliitwa kifurushi cha dawa, kilikuwa mkusanyo wa vitu vya kidini vilivyofungwa katika ngozi ya mnyama. Kifurushi hicho chenye urefu wa sentimeta 60 hivi kina umbo la yai. Nilikaa kwa muda mrefu mahali patakatifu pa hema la ibada, ambapo niliwasikiliza viongozi wa kabila la Kickapoo waliponifunulia siri za dini yetu. Kwa hiyo, nikawa kiongozi mpya wa dini ya Wakickapoo nikiwa mdogo.

Nilielewa mambo hayo yote vizuri ijapokuwa nilikuwa mchanga. Kwa kuwa siri hizo hazikuandikwa, hakuna mtu mwingine isipokuwa mimi ambaye alijua mapokeo hayo ya kidini ya vizazi vingi vilivyopita. Kama ningalifanya vile wazee wa ukoo walivyotaka, ningalibaki huko, nikisimamia shughuli zote za dini mpaka leo.

Hata hivyo, nilienda shule huko Kansas. Jambo hilo liliwatia wazee wasiwasi, kwa kuwa waliogopa kwamba ningepotelea katika “ulimwengu wa Wazungu.” Baada ya kumaliza shule nilienda Los Angeles, California, ambako nilikutana tena na Diane, msichana niliyempenda tangu utotoni. Jina lake la kienyeji ni Tu-NO-Tak-Wa ambalo linamaanisha Dubu Anayegeuka, naye ni wa ukoo wa Dubu. Mama zetu na babu zetu walikuwa marafiki tangu zamani. Tulioana Septemba 1956. Wazazi wa Diane walikuwa watu wa dini pia. Babu yake alianzisha dini ya Peyote katika kabila la Kickapoo.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 22.

Dini ya Peyote

Dini ya Peyote imeenea katika makabila mengi ya Wahindi leo. Quanah Parker (1845-1911 hivi), kiongozi wa dini na chifu wa ukoo wa Kwahadi wa kabila la Comanche, “alihusika sana katika kuendeleza dini ya peyote katika Eneo la Wahindi.” (The Encyclopedia of Native American Religions) Alitangaza kwa bidii ubora wa dawa za kulevya za mmea wa dungusi aina ya peyote unaosemekana una uwezo wa kuponya. Alipata wafuasi katika makabila mengi ya Wahindi wa Amerika Kaskazini. Kwa hiyo, miongoni mwa Wakickapoo, kama vile makabila mengine mengi, dini mbili zilikubaliwa, yaani, dini yao ya kikabila na vilevile dini ya Peyote.

Naenda Hollywood

Nilipokuwa Los Angeles, nilijihusisha sana na mashirika ya jamii ya Wahindi na hata nikawa msimamizi wa mashirika kadhaa. Baadhi ya mashirika hayo ni Shirika la Ngoma na Manyoya, Shirika la Kitaifa la Wanariadha Wahindi, na shirika la Wahindi la mchezo fulani wa mpira. Pia nilikuwa mwanachama wa baraza la wakurugenzi wa Kituo cha Wahindi huko Los Angeles.

Nilifahamiana na watu kadhaa mashuhuri huko Hollywood. Baadhi yao ni Iron Eyes Cody, mtangazaji maarufu wa habari za mazingira kwenye televisheni, na Jay Silverheels, aliyeigiza Mhindi aitwaye Tonto katika mfululizo wa kipindi cha televisheni kinachoitwa Mpanda-Farasi Mpweke (Lone Ranger). Sinema maarufu zaidi niliyohusika ni ile ya Magari Songeni Magharibi! (Westward Ho, the Wagons!) mhusika mkuu akiwa Fess Parker, na sinema inayoitwa Wenzi (Pardners), wahusika wakuu wakiwa Dean Martin na Jerry Lewis.

Mimi na Diane tulifanya kazi kwa muda kwenye sehemu ya burudani inayoitwa Disneyland. Nilifanya michezo ya kuigiza ya dakika kumi kila saa, mchana kutwa. Diane anasema hivi huku akitabasamu: “Nilihitaji tu kuvaa na kutembea-tembea kati ya watu mchana kutwa huku ‘nikijifanya’ kuwa Mhindi.”

Mtazamo Tofauti wa Kiroho

Mmoja wa Mashahidi wa Yehova alimtembelea Diane mwaka wa 1962, na kumpa kijitabu fulani. Shahidi huyo alimrudia tena na tena, lakini Diane aliendelea kutoa visababu vya kutomsikiliza. Shahidi huyo alipomuuliza kama alitaka aache kumtembelea, Diane alisema kimoyo-moyo, ‘Ndiyo! Ndiyo!’ Lakini kwa sababu hakutaka kumuumiza, akasema: “Hapana!” Kwa hiyo, Shahidi huyo akaendelea kumtembelea. Sikuzote aliniambia mambo aliyojifunza. Nyakati nyingine aliposahau kunieleza nilimuuliza hivi: “Je, yule mwanamke Shahidi wa Yehova alikuja? Alisema nini?”

Pindi moja mwanamke huyo alimweleza Diane kuhusu hotuba fulani ya pekee katika mkutano wa Mashahidi wa Yehova kwenye Jumba la Mkutano la Los Angeles. Alijitolea kuwatunza watoto wetu wanne tulipokuwa kwenye mkutano huo. Diane hata hakunitajia jambo hilo kwa kuwa alifikiri singeenda. Lakini akaniambia baada ya Shahidi huyo kusisitiza aniambie. Alishangaa niliposema: “Je, unamaanisha kwamba Mzungu huyo atakaa hapa awatunze na kuwalisha watoto wetu?”

Hivyo, mwaka wa 1969 tukahudhuria mkutano wetu wa kwanza. Sikuelewa kila jambo lililotajwa jukwaani. Hata hivyo, nilivutiwa na utaratibu kwenye mkutano huo. Nilishangaa kuwaona watu 20,000 wakipata chakula cha mchana kwa muda mfupi sana kupitia mpango wao wa kujitolea. Pia niliona kwamba hawakuwa na ubaguzi, watu weusi na weupe waliitana ndugu na dada.

Mnamo Agosti 1969, Mashahidi hao walianza kunifunza Biblia wakitumia kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele. * Sikuwa na nia inayofaa nilipokubali kujifunza Biblia. Nilikuwa nimejiunga na mashirika kadhaa ya Wahindi na nilitarajia kuwa mwanasiasa. Nilifikiri inafaa nijifunze Biblia kwa sababu ilionekana kwamba wanasiasa waliijua na hata waliinukuu. Lakini sasa ninatambua kwamba watu hao hawakujua mengi kuhusu Neno la Mungu.

Badiliko Kubwa Maishani Mwangu

Nilipoanza kujifunza Biblia, nilifanya maendeleo haraka. Nilijiuzulu kutoka mashirika yote niliyokuwa nimejiunga nayo, na nilijua kwamba nilipaswa kuacha dini yangu ya zamani ya kikabila. Ninakumbuka nilipoandika barua ya kujiuzulu dini hiyo. Niliandika tarehe kwenye sehemu ya juu ya ukurasa kisha nikaandika “Kwa.” Baada ya kufikiria kwa muda mrefu niliyepaswa kumwandikia, nilitambua kwamba barua hiyo ilipaswa kuandikiwa kiongozi wa dini ya kikabila, yaani, mimi! Nilitatua tatizo hilo mara moja kwa kuandika “Mama Mpendwa.” Kisha, nikamweleza mamangu kwamba sitaendelea kushirikiana na dini hiyo na kwamba sitakuwa kiongozi wake tena.

Mnamo Januari 3, 1970, mimi na mke wangu tulibatizwa na kuwa Mashahidi wa Yehova. Mwaka wa 1973, nikawa mzee wa kutaniko. Sasa badala ya kuwa kiongozi wa dini ya Wakickapoo nilikuwa nikiongoza kutaniko letu katika ibada ya kweli ya Yehova Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu. Mnamo Julai 1974, tulirudi McLoud, Oklahoma, ili tuwasaidie wenyeji wa asili wa Amerika kujua tumaini la kweli la wanadamu wote, kupatana na Neno la Mungu, Biblia.

Kama makabila mengine, Wakickapoo walitumia tumbaku katika ibada yao. Lakini hawakuivuta. Waliinyunyiza motoni kama uvumba, wakiamini kwamba sala zao zingeenda mbinguni katika moshi wake. Viongozi wazee miongoni mwa Wakickapoo waliamini kwamba ni jambo ovu kuvuta tumbaku na kwamba ni dhihaka kutumia kiko kwa sababu kinatokana na Wazungu.

Nimeulizwa iwapo nina picha zinazoonyesha mavazi yangu ya dini ya zamani. Kwa kweli picha hazikuruhusiwa kwa sababu ya kuogopa kwamba wachawi wangezitumia. Kwa miaka hiyo yote, niliponyolewa nywele zangu zilizikwa na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuzigusa. Hivyo, hazingeweza kutumiwa katika uchawi, ambao Wahindi wanauchukua kwa uzito sana.

Nilipoacha dini ya Wakickapoo, wazee wa ukoo walianza kuongoza dini hiyo. Wakati wazee 12 walionichagua walipokufa, wazee wapya wa ukoo walichukua madaraka, na muda si muda wakafanya mabadiliko mengi katika dini hiyo. Sasa ni mzee mmoja tu wa ukoo anayebaki, naye ni mzee sana. Sikusudii kuwaeleza wengine yale niliyofunzwa nilipokuwa mvulana mdogo.

Sasa ninajitahidi sana kuwafundisha watu wa mataifa na makabila yote Neno la Mungu. Kwa kuwa mimi ni mhubiri wa wakati wote, nimekuwa na pendeleo la kufundisha kwenye maeneo ya Wahindi kotekote Marekani. Baadhi ya makabila ambayo nimeyatembelea ni, Waosage huko Oklahoma, Wamohave, Wahopi, na Wanavajo huko Arizona. Ninafurahia kuwaeleza Wahindi wenzangu kwamba “Nchi ya Uwindaji Yenye Furaha,” usemi ambao tumetumia kwa muda mrefu kuhusu maisha ya baada ya kifo, unakazia fikira “nchi.” Kwa hiyo, ninawaeleza kwamba maneno hayo yanaonyesha kwamba tarajio lao ni kuishi hapa duniani wala si mbinguni kama wanavyoamini. Ninatarajia kwa hamu ufufuo wa Wahindi wengi wa kale ili niweze kuwafundisha kuhusu ulimwengu mpya wa Mungu.—Yohana 5:28, 29; 2 Petro 3:13.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Jina Kickapoo linatokana na neno kiikaapoa, “watu wenye kuhama-hama.”—Encyclopedia of North American Indians.

^ fu. 19 Kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]

Dini ya Peyote Ni Nini?

Sasa, dini ya Peyote inaitwa Kanisa la Wahindi wa Amerika. Peyote ni mmea mdogo aina ya dungusi (ona kulia) unaopatikana hasa katika bonde la Rio Grande huko Mexico na pia Texas. Dini ya Peyote ina zaidi ya wafuasi 200,000 wa makabila ya Amerika Kaskazini. “Leo, dini hiyo ambayo ilianzishwa zamani huko Mexico, inahusisha mambo ya Ukristo, lakini bado ni dini ya Wahindi pekee.” (A Native American Encyclopedia—History, Culture, and Peoples) Sherehe ya Mwezi-Nusu na ya Mwezi Mkubwa ndizo muhimu zaidi katika dini ya Peyote. Sherehe hizo zinahusisha “utamaduni wa Kihindi na Ukristo.” Sherehe hizo ambazo kwa kawaida huanza Jumamosi, husherehekewa usiku kucha. Wakati wa sherehe hizo kikundi cha wanaume huketi kwa mviringo ndani ya hema lenye umbo la pia. Wao hupata maono huku wakila chipukizi nyingi chungu za dungusi ya peyote, na kuimba nyimbo takatifu kwa kufuatana na mdundo wa ngoma na kibuyu chenye kulia kama kayamba.

[Hisani]

Courtesy TAMU Cactus Photo Gallery

[Picha katika ukurasa wa 21]

Nikiwa nimevalia kama mpiganaji wa Wakickapoo

[Picha katika ukurasa wa 23]

Nikiwa na mke wangu Diane leo