Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni nini suluhisho la Kunenepa Kupita Kiasi?

Ni nini suluhisho la Kunenepa Kupita Kiasi?

Ni nini suluhisho la Kunenepa Kupita Kiasi?

AMKENI! lilimhoji mtaalamu wa lishe anayeitwa Diane, na muuguzi anayeitwa Ellen. Wote wawili huwahudumia wagonjwa wanene na walionenepa kupita kiasi. Wote walisema kwamba mtu anapoacha kula vyakula vyenye wanga na kula protini nyingi (nyama) anaweza kupunguza uzito. Hata hivyo, wanasema kwamba hatimaye hilo linaweza kusababisha madhara. * Jambo hilo linathibitishwa na chati ya tiba inayoitwa Kudumisha Uzito Unaofaa. Inasema hivi: “Kuzoea kula kiasi kidogo cha wanga ni hatari, hasa bila mwongozo wa daktari.” Inaendelea kusema: “Lengo la mazoea hayo ni kupunguza uzito haraka kwa kusababisha ongezeko kubwa sana la ketoni (ambazo hutokezwa wakati mafuta yanaposagwa mwilini).” Ikiwa unafikiria kupunguza kiasi cha wanga unachokula, ingefaa kwanza umwombe daktari mashauri.

Ikiwa unataka kupunguza uzito, usivunjike moyo. Dakt. Walter C. Willett anasema kwamba “inawezekana kupunguza uzito, na hilo halimaanishi kujinyima au kula chakula kilekile nyakati zote. Kwa kujitahidi sana na kutumia maarifa, watu wengi wanaweza kufanikiwa kupunguza na kudumisha uzito wao huku wakila vyakula wanavyovifurahia kwa usawaziko na kufanya mazoezi karibu kila siku. Jitihada hizo zinahitajiwa ili uishi muda mrefu ukiwa na afya nzuri.” *—Italiki ni zetu.

Mazoezi Ni Muhimu Kadiri Gani?

Dakt. Willett anasema hivi: “Zaidi ya kutovuta sigara, kufanya mazoezi ndiyo njia bora zaidi ya kuwa na afya au kudumisha afya bora, na hivyo kuepuka magonjwa hatari.” Mtu anapaswa kufanya mazoezi mara ngapi? Kuna faida gani kufanya mazoezi?

Wataalamu fulani wanasema kwamba kufanya mazoezi kila siku, hata kama ni kwa dakika 30 tu, kunaweza kukunufaisha sana. Lakini imesemwa kwamba hata kufanya mazoezi mara tatu tu kwa juma kunaweza kumsaidia mtu aepuke matatizo makubwa wakati ujao. Tunapofanya mazoezi tunapunguza kalori. Mtu anayetaka kupunguza uzito anapaswa kujiuliza swali hili muhimu, Je, kila siku mimi hula chakula chenye kalori nyingi na kutumia kalori chache? Ukila chakula chenye kalori nyingi na kutumia kalori chache, bila shaka utaongeza uzito. Kwa hiyo, tembea au uendeshe baiskeli badala ya kusafiri kwa gari. Panda ngazi badala ya kutumia lifti. Fanya mazoezi! Tumia kalori!

Dakt. Willett anaeleza hivi: “Watu wengi huona kwamba kutembea ni njia bora ya kufanya mazoezi kwa sababu mtu hahitaji vifaa vya pekee, anaweza kutembea wakati wowote na mahali popote, na si rahisi kuumia.” Anapendekeza watu watembee haraka-haraka badala ya kutembea kwa starehe. Pia anapendekeza watu wafanye mazoezi kwa dakika 30 kila siku ikiwezekana.

Je, Suluhisho Ni Kufanyiwa Upasuaji?

Ili kupunguza uzito na kuepuka kuongeza uzito, watu wengine walionenepa kupita kiasi wamefuata mashauri ya wataalamu fulani ambao hupendekeza mbinu mbalimbali za upasuaji. Ni nani wanaoweza kupasuliwa? Waandishi wa kitabu Mayo Clinic on Healthy Weight wanapendekeza hivi: “Huenda daktari akataka ufanyiwe upasuaji ikiwa BMI yako inazidi 40, hilo likionyesha kwamba umenenepa kupita kiasi.” (Ona chati kwenye ukurasa wa 5.) Kichapo Mayo Clinic Health Letter kinapendekeza hivi: “Upasuaji kwa ajili ya watu walionenepa kupita kiasi unapendekezwa tu kwa watu wenye umri wa kati ya miaka 18 na 65 ambao BMI yao imezidi 40 na unene wao unahatarisha sana afya yao.”—Italiki ni zetu.

Ni nini baadhi ya njia za upasuaji? Njia hizo zinahusisha kufupisha sehemu ya tumbo inayoitwa chango, kufunga sehemu fulani ya tumbo na kuacha nafasi ndogo ya kupitisha chakula, na kufunga sehemu ya juu ya tumbo, na kuacha kifuko kidogo kinachoweza kutoshea kiasi kidogo tu cha chakula. Katika njia hiyo iliyotajwa mwisho, chango hukatwa na kuunganishwa na kifuko hicho. Hivyo, chakula hakiingii katika sehemu kubwa ya tumbo kutia ndani duodeni (duodenum).

Vipi watu ambao wamepunguza uzito sana? Je, wamepata faida zozote?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Madhara hayo yanatia ndani ongezeko kubwa la chuma katika damu, matatizo ya figo, na kufunga choo.

^ fu. 3 Inafaa Wakristo waliojiweka wakfu, ambao wanataka kutumia maisha yao kwa njia inayokubalika katika utumishi mtakatifu wa Mungu, wapunguze uzito ili wawe na afya njema. Badala ya kufa mapema, wanaweza kumtumikia Mungu kwa miaka mingi.—Waroma 12:1.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Madokezo ya Mazoea Mazuri ya Kula

Peremende Tamutamu, peremende

zilizotengenezwa viwandani (mara chache;

usile zaidi ya kalori 75 kwa siku)

Mafuta Mafuta ya zeituni, njugu, mafuta ya

canola, parachichi (mara 3-5 kwa siku; yaani

kila mara pakua kijiko kimoja kidogo cha mafuta

au vijiko viwili vikubwa vya njugu)

Protini na Vyakula vya Maziwa Maharagwe, samaki,

nyama isiyo na mafuta mengi, mayai, vyakula

vilivyotengenezwa kwa maziwa visivyo na mafuta mengi,

jibini (mara 3-7 kwa siku; kila mara pakua gramu 85

hivi tu za nyama iliyopikwa au samaki)

Vyakula Vyenye Wanga Hasa nafaka, spageti, mkate, wali

(mara 4-8 kwa siku; kila mara kula kipande cha mkate)

Matunda na Mboga Kula mboga mbalimbali (kula mara nyingi; angalau 3)

Amkeni! halipendekezi mazoea yoyote hususa ya kula na njia za kudhibiti uzito. Linawaeleza tu wasomaji wake baadhi ya njia zinazoweza kutumiwa. Watu wanapaswa kupata mashauri ya daktari kabla ya kuanza mazoezi yoyote au kufuata mazoea fulani ya kula.

[Hisani]

Kwa mujibu wa Mayo Clinic

[SAnduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Wengine wametumia madokezo haya ili kupunguza uzito:

1 Jua kiasi cha kalori zilizomo katika chakula unachokula na vinywaji unavyokunywa. Kumbuka: Vinywaji huwa na kalori nyingi, hasa vile vilivyoongezwa sukari. Vilevile, pombe huwa na kalori nyingi sana. Pia, jihadhari na soda zinazotangazwa sana na wafanyabiashara. Chunguza kiwango cha kalori kilichoonyeshwa kwenye kibandiko. Ukifanya hivyo, huenda ukashangaa kuona kiasi cha kalori kilicho katika kinywaji hicho.

2 Epuka kushawishiwa. Bila shaka, utakula chipsi, chokoleti, au biskuti ikiwa zinapatikana kwa wingi nyumbani! Usiweke vitu hivyo nyumbani, badala yake hifadhi tu vyakula vilivyo na kalori chache, kama vile matofaa, karoti, na vyakula vya nafaka.

3 Kula kitu kidogo kabla ya mlo. Kufanya hivyo kutapunguza hamu yako ya kula na huenda kukakufanya ule chakula kidogo.

4 Usile kila kitu kinachoandaliwa. Chagua unachokula. Usile chochote ambacho unajua kina kalori nyingi sana.

5 Usiharakishe. Haraka ni ya nini? Furahia mlo wako kwa kuchunguza unachokula—angalia rangi yake, onja ladha yake, na ufurahie jinsi kinavyochangamana vizuri. Tambua dalili za mwili zinazokuonyesha kwamba umeshiba.

6 Acha kula kabla ya kuhisi kwamba umeshiba.

7 Katika nchi fulani, mikahawa huwapakulia watu chakula kingi kupita kiasi. Unaweza kula nusu ya chakula hicho au unaweza kumgawia mtu mwingine.

8 Si lazima ule vyakula vitamu vinavyoandaliwa baada ya mlo mkuu. Baada ya mlo, ni afadhali kula tunda au kitu kingine chenye kalori chache.

9 Wauzaji wa vyakula hutaka ule sana. Kusudi lao ni kupata faida. Watajaribu kulenga udhaifu wako. Usipumbazwe na matangazo yao ya biashara ya ujanja na picha maridadi. Unaweza kukataa katakata kushawishiwa nao!

[Hisani]

Madokezo haya yametolewa katika kitabu Eat, Drink, and Be Healthy, cha Dakt. Walter C. Willett

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Fanya mazoezi!