Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Wamo Hatarini?

Kwa Nini Wamo Hatarini?

Kwa Nini Wamo Hatarini?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA

SIMBA-MILIA mwenye fahari wa Bengal, mbwa-mwitu, korongo wa sarus, kasa, na tembo wa Asia ni baadhi ya jamii za wanyama zilizomo hatarini nchini India. Pia fikiria mnyama mkubwa zaidi wa nchi kavu anayeitwa tembo.

Pembe za tembo zinapendwa sana. Japani ni mojawapo ya nchi zinazotumia pembe hizo zaidi, na vilevile zinapendwa sana nchini China ambako zinatumiwa kutengeneza vijiti vya kulia chakula. Jambo hilo limewaathirije tembo wa Asia?

Wakati mmoja gazeti The Times of India lilieleza hivi: “Tembo wa Asia ni tofauti na tembo wa Afrika kwani ni wachache walio na pembe, nao ni wa kiume tu. Hivyo, tembo wa kiume waliokomaa ndio hasa huuawa. Kulingana na habari rasmi, tembo mia moja hivi [wa kiume] huuawa kila mwaka nchini India, na hilo huathiri uwiano kati ya tembo wa kiume na wa kike.” Mauaji hayo yamehatarisha sana jamii hiyo ya tembo.

Kuwaua Ili Kupata Pembe Tu

Pia, fikiria kifaru, ambaye ni mnyama wa nchi kavu aliye wa pili kwa ukubwa. Vifaru wenye pembe moja wamesalia tu nchini India na Nepal. Hata hivyo, Mbuga ya Wanyama ya Pobitara iliyoko kaskazini-mashariki mwa jimbo la Assam nchini India ina ukubwa wa kilometa 38 tu za mraba, na hilo ni eneo dogo la kuwahifadhi vifaru. Hivyo, wanyama hao huvamia mashamba yaliyo karibu, ambako huenda wakafyatuliwa risasi au kuuawa kwa sumu.

Wanadamu wamevumbua mbinu za ujanja za kumuua kifaru. Kuna nyaya mbili za umeme zinazopita juu ya Mbuga ya Pobitara. Wawindaji-haramu huning’iniza waya kwenye nyaya hizo kwa kutumia mwanzi mrefu, kisha waya huo hubembea karibu na ardhi. Mtaalamu wa wanyama-pori, Vivek Menon, anaeleza kilichotukia wakati kifaru mmoja alipogusa waya huo: “Nguvu za umeme zilipompiga, alipumua kwa nguvu mara mbili na kuanguka haraka . . . Mnyama huyo akalala kwa upande na kufa papo hapo.”

Inasikitisha kwamba mnyama huyo mkubwa huuawa kwa sababu ya pembe yake ndogo iliyo na uzito wa kilo moja! Kifaru amehatarishwa sana kwa sababu ya thamani kubwa ya pembe yake, ambayo ni mkusanyiko wa nywele nyingi zilizo kama kucha za binadamu.

Kuwaua Ili Kutengeneza Shali za Shahtoosh

Paa wa Tibet, au chiru, ana sufu inayoitwa shahtoosh. Sufu hiyo ni laini sana hivi kwamba shali inayotengenezwa kutokana nayo inaweza kupitishwa kwenye pete ya kidole. Shali hiyo inaweza kugharimu dola 16,000, na hivyo ni mojawapo ya shali zinazouzwa kwa bei ghali sana ulimwenguni. Hilo limemwathirije paa huyo?

Gazeti The Indian Express linasema kwamba “chiru watano huuawa ili kutengeneza shali moja ya shahtoosh.” Inasemekana kwamba paa 20,000 hivi wa Tibet huuawa kila mwaka. Paa hao huuawa ijapokuwa wanapaswa kulindwa na sheria fulani za kulinda wanyama waliomo hatarini. Isitoshe, katika 1979 uuzaji wa sufu ya shahtoosh ulipigwa marufuku. Hata hivyo, tangu wakati huo idadi ya chiru imezidi kupungua.

Kuuawa Ili Kupata Ngozi na Mifupa

Pia simba-milia na wanyama wengine wa pori wa jamii hiyo wamo hatarini nchini India. Katika maeneo mengine, inadhaniwa kwamba aina fulani za simba-milia kama vile Caspian, Java, na Bali tayari wametoweka. Mwanzoni mwa karne ya 20, simba-milia 40,000 hivi walikuwepo katika misitu ya India. Idadi yao imepungua kadiri miaka ilivyopita. Hiyo ni kwa sababu makao yao yamekuwa yakiharibiwa na wamewindwa kwa ajili ya ngozi na mifupa fulani inayotumiwa katika tiba ya Kichina.

Kitabu The Secret Life of Tigers kinaeleza jinsi ambavyo simba-milia wameathiriwa na ukosefu wa makao yanayofaa kinaposema hivi: “Idadi ya simba-milia inaweza kuongezeka iwapo tu misitu wanamoishi itapanuka. Ikiwa misitu hiyo si mikubwa vya kutosha, simba-milia watapunguza idadi yao kwa kupigana na kuuana ili kupata chakula na makao.”

Vipi kuhusu wanyama wengine wa jamii hiyo nchini India? Kwenye bustani moja ya wanyama huko Junagadh, Gujarat, mtalii mmoja aliona kizimba kitupu. Ishara iliyokuwa nje ya kizimba hicho ilikuwa na picha ya duma wa Asia na ujumbe ulioandikwa katika Kigujarati, ambao ulisema: “Duma hawa walitoweka nchini India katika miaka ya 1950.”

Wanyama Hawa Wana Tumaini Gani?

Inaonekana kwamba wanyama waliomo hatarini nchini India hawana tumaini zuri. Uthibitisho mwingi unaonyesha kwamba wanadamu wameharibu dunia kwa ubinafsi, na hivyo wamewaangamiza wanyama-pori wengi wa ajabu. Basi itakuwaje? Maneno ya Mungu yenye kutumainika, yanayopatikana katika Biblia Takatifu, yanaonyesha kwamba karibuni unabii huu utatimizwa: “Mataifa wakawa na ghadhabu, nayo ghadhabu yako [Mungu] mwenyewe ikaja, na wakati uliowekwa . . . kuwaharibu wale wanaoiharibu dunia.”Ufunuo 11:18.

Itakuwaje wakati watu wote wanaoiharibu dunia na kuwaangamiza wanyama watakapoondolewa? Itakuwa pindi nzuri ajabu! Wanadamu hawatahatarisha tena jamii yoyote ya wanyama. Hilo litatimizwa wakati ambapo Ufalme wa Mungu, ambao Yesu Kristo aliwafundisha wanadamu kuomba, utatawala.—Isaya 11:6-9; Mathayo 6:10.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Baadhi ya wanyama waliomo hatarini nchini India

Korongo wa “sarus”

Simba-milia wa Bengal

Tembo wa Asia

Kifaru mwenye pembe moja

Paa wa Tibet

[Hisani]

Crane: Cortesía del Zoo de la Casa de Campo, Madrid; antelope: © Xi Zhi Nong/naturepl.com