Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kula Takataka

Mwanabiolojia Wilfried Meyer anasema: “Inashangaza jinsi ambavyo takataka zimekuwa chakula muhimu cha ndege na wanyama. Katika maeneo fulani aina fulani za wanyama hula takataka tu.” Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la Der Spiegel, uchunguzi uliofanywa ulimwenguni pote unaonyesha kwamba karibu aina 70 za ndege na aina 50 za wanyama hula takataka. Mfumo wa kutegemeana umesitawi kwenye marundo ya takataka. Wadudu husitawi katika joto linalotokezwa na takataka zinazooza. Ndege na wanyama wadogo hula wadudu hao kisha wanawindwa na ndege na wanyama wengine. Inashangaza kwamba baadhi ya ndege waoga hawatoroki kunapokuwa na kelele za mashine za kushindilia takataka au wanadamu na wanyama wanapokuwa kwenye maeneo ya takataka.

Tembo Wanaoteka Nyara

Inaonekana kwamba si wanadamu tu wanaowanyang’anya watu vitu katika barabara kuu. Kulingana na gazeti Bangkok Post, tembo pia wameanza kuwanyang’anya watu vitu. Tembo wenye njaa kutoka kwenye misitu iliyo mashariki mwa Bangkok wamekuwa wakifunga barabara zinazotumiwa na malori ya kubeba miwa na kupora miwa. Kwa kawaida, tembo 130 hivi huishi katika mbuga ya wanyama wa pori ya Ang Lue Nai, lakini kwa sababu ya ukame hawapati majani ya kutosha na hivyo wanalazimika kutangatanga ili kutafuta chakula. Msimamizi wa mbuga hiyo, Yoo Senatham, aliripoti kwamba tembo fulani wameanza kuvamia mashamba, huku wengine wakiokota miwa inayoangushwa na ­madereva wa malori wenye huruma.

Dawa za Wanyama

Kwa muda mrefu, Shirika la Afya Ulimwenguni limeonya dhidi ya kuwapa wanyama wa kufugwa ambao si wagonjwa dawa nyingi zisizo za lazima. Kulingana na gazeti ABC la Hispania, dawa hizo zimetumiwa kwa ukawaida katika chakula cha mifugo “ili kuwanonesha upesi wanyama hao.” Hivi majuzi, uchunguzi uliofanywa nchini Denmark ulionyesha kwamba kufuga wanyama bila kuwapa dawa kuna faida. Wakulima walipoacha kuweka dawa katika chakula cha wanyama, uzalishaji wa kuku haukuathiriwa, na gharama za kufuga nguruwe ziliongezeka kwa asilimia 1 tu. Shirika la Afya Ulimwenguni limesifu hatua hiyo ya Denmark na linahimiza nchi nyingine kufanya hivyo pia. Gazeti hilo linasema kwamba kufanya hivyo “kutaboresha afya ya watu pia.”

Udanganyifu Katika Mchezo wa Chesi

Gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung linaripoti kwamba “nyakati nyingine wachezaji wengi wa chesi hawazingatii sheria za mchezo huo.” Mfano mmoja ni wa mchezaji mmoja chipukizi aliyemshinda bingwa wa chesi. Hata hivyo, baadaye iligunduliwa kwamba alikuwa ameficha maikrofoni, vidude vya kuwekwa masikioni ili kusikia, na kamera kwenye nywele zake ndefu ili kuwasiliana na mchezaji mwingine aliyekuwa akitumia kompyuta katika chumba kingine. Wachezaji wengine huenda chooni, na baada ya kufunga mlango, wao hutoa kompyuta ndogo na kuitumia kupanga jinsi watakavyocheza. Wale wanaocheza kwenye Intaneti wanaweza kudanganya pia. Wengine hutumia programu ya chesi kwenye kompyuta wanapocheza kwenye Intaneti. Katika visa vingine, wachezaji fulani walitumia majina mawili na kucheza dhidi yao wenyewe, na kila mara jina moja lilishindwa huku lile lingine likipata maksi zaidi. Gazeti hilo linasema kwamba “wengi hawachezi ili kupata pesa. Katika visa vingi, hawachochewi na pupa bali huchochewa na tamaa ya umashuhuri.”

Je, Kweli Wazee Wanaweza Kujifunza?

Gazeti Daily Nation la Nairobi liliripoti hivi: “Kati ya watoto wenye umri wa miaka sita wanaosomea katika [shule moja ya msingi katika Mkoa wa Rift Valley nchini Kenya], kuna mwanafunzi mmoja aliye mkubwa kuliko wengine.” Huyo ni mzee mwenye umri wa miaka 84 ambaye alianza darasa la kwanza “ili ajifunze kusoma Biblia.” Ingawa ana wajukuu ambao wako katika madarasa ya juu, bado anaenda shuleni. Mzee huyo aliliambia hivi gazeti Nation: “Watu wamekuwa wakiniambia mambo fulani katika Biblia ambayo sina uhakika kwamba ni ya kweli, na ninataka kujisomea hicho Kitabu Kitakatifu ili kuhakikisha mambo hayo.” Akiwa amevalia sare za shule na kubeba kalamu na vitabu, yeye hujitahidi kufuata sheria ngumu za shule. Hata hivyo, anaruhusiwa kufanya mambo fulani kwa njia tofauti na wengine. Wanafunzi wengine wanapofanya mazoezi na kucheza, yeye “huruhusiwa kunyoosha misuli yake taratibu.”

Matetemeko Hatari Katika Mwaka wa 2003

“Kulingana na Shirika la Marekani la Uchunguzi wa Jiolojia, mwaka wa 2003 ndio mwaka ambao watu wengi zaidi walikufa kutokana na matetemeko ya ardhi tangu mwaka wa 1990, kwani idadi ya vifo ilizidi mara 25 ile ya mwaka wa 2002,” yasema ripoti moja ya shirika hilo. “Katika mwaka wa 2002, watu 1711 walikufa kutokana na matetemeko ya ardhi ulimwenguni,” hali watu 43,819 walikufa mwaka jana. Kati ya vifo hivyo, 41,000 vilitukia huko Iran wakati tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 6.6 lilipotokea katika jiji la Bam katika Desemba 26. Tetemeko kali zaidi lililozidi kipimo cha 8.0, lilitokea huko Hokkaido, Japani, katika Septemba 25. Lilikuwa na kipimo cha 8.3. Kulingana na ripoti hiyo, “Shirika la Marekani la Uchunguzi wa Jiolojia hugundua matetemeko ya ardhi 50 hivi kila siku. . . . Kwa wastani, matetemeko makubwa 18 (yenye kipimo cha 7.0 hadi 7.9) na moja kubwa zaidi (lenye kipimo cha 8.0 au zaidi) hutokea kila mwaka ulimwenguni. Mamilioni ya matetemeko ya ardhi hutokea ulimwenguni kila mwaka, lakini mengi hayagunduliwi kwa sababu yanatukia katika maeneo yaliyo mbali au huwa madogo sana.”

Kwa Nini Watoto Wengi Ni Wahalifu?

Wataalamu wanaamini kwamba kuzorota kwa maisha ya familia ndicho kisababishi kikubwa cha ongezeko la haraka la uhalifu miongoni mwa watoto. Kulingana na ripoti moja katika gazeti Weekend Witness la Afrika Kusini, wengi wa watoto hao hutoka katika familia zilizovunjika au katika familia ambazo wazazi wote wawili wanafanya kazi nao huwa na shughuli nyingi na wamechoka hivi kwamba hawezi kuwashughulikia. Kulingana na mtaalamu wa jinai, Dakt. Irma Labuschagne, vijana wengi hawaelewi “familia” ni nini, nao “wanatamani kupendwa na kukubaliwa.” Hivyo, wanatafuta mambo hayo kwingineko, nao hushawishiwa kwa urahisi kujiunga na magenge ya wahalifu ambayo huwafanya wahisi kwamba wanapendwa. Dakt. Cecelia Jansen, ambaye ni mwanasaikolojia, anasema kwamba wazazi “hushughulikia sana kutafuta cheo, mafanikio na mali hivi kwamba hawajui kinachowapata washiriki wa familia zao.” Kulingana na gazeti hilo, Labuschagne na Jansen wanapendekeza “familia ziishi kama zamani.” Gazeti hilo linakata kauli hii: “Hakuna kitu kinachoweza kuchukua mahali pa maisha ya familia yaliyo mazuri, yenye furaha, na yaliyo ya kawaida.”