Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vyanzo vya Ubaguzi

Vyanzo vya Ubaguzi

Vyanzo vya Ubaguzi

UBAGUZI unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali. Hata hivyo, sababu mbili kuu ni (1) tamaa ya kumtafuta mtu wa kulaumu na (2) chuki inayosababishwa na dhuluma zilizofanywa zamani.

Kama ilivyoonyeshwa katika makala inayotangulia, msiba unapotokea, mara nyingi watu humtafuta mtu wa kulaumu. Watu mashuhuri wanapolalamika mara nyingi kuhusu watu wa jamii ndogo, malalamiko hayo hukubaliwa na ubaguzi hutokea. Kwa mfano, matatizo ya kiuchumi yanapotokea katika nchi za Magharibi, watu ambao wamehamia huko hulaumiwa kwa kusababisha ukosefu wa kazi, hata ingawa kwa kawaida wao hufanya kazi ambazo wenyeji hawapendi.

Lakini ubaguzi hausababishwi nyakati zote na tamaa ya kumtafuta mtu wa kulaumu. Ubaguzi unaweza kusababishwa pia na mambo yaliyotukia wakati uliopita. Ripoti ya UNESCO Against Racism inasema: “Si kutia chumvi kusema kwamba biashara ya watumwa iliweka msingi wa ubaguzi wa rangi na madharau dhidi ya utamaduni wa watu weusi.” Watu waliofanya biashara ya utumwa walitetea biashara yao yenye kuchukiza ya kuwanunua na kuwauza wanadamu kwa kudai kwamba Waafrika ni duni. Ubaguzi huo usio na msingi wowote, ambao baadaye uliwaathiri watu waliokuwa chini ya ukoloni, bado unaendelea.

Ulimwenguni pote, matukio ya wakati uliopita ya uonevu na dhuluma huendeleza ubaguzi. Uhasama kati ya Wakatoliki na Waprotestanti nchini Ireland ulianza katika karne ya 16, watawala wa Uingereza walipowanyanyasa na kuwapeleka Wakatoliki uhamishoni. Ukatili uliofanywa na watu waliodai kuwa Wakristo wakati wa vile Vita Vitakatifu huwafanya Waislamu wa Mashariki ya Kati waendelee kuwa na chuki. Uhasama baina ya Waserbia na Wakroatia katika eneo la Balkan ulichochewa na mauaji ya raia wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Kama mifano hiyo inavyoonyesha, uadui ambao umekuwepo kati ya vikundi viwili unaweza kuzidisha ubaguzi.

Kutofahamu Watu wa Jamii Nyingine

Mtoto mchanga hana ubaguzi. Badala yake, watafiti wanasema kwamba mara nyingi ni rahisi kwa mtoto kucheza na mtoto wa jamii tofauti na yake. Hata hivyo, mtoto anapofikia umri wa miaka 10 au 11, huenda asipendezwe na watu wa kabila, rangi, au dini tofauti. Anapoendelea kukua, yeye husitawisha maoni tofauti-tofauti kuhusu watu wa jamii nyingine na anaweza kuendelea kuwa na maoni hayo katika maisha yake yote.

Mtoto hupataje maoni hayo? Mtoto hupata maoni hayo mabaya hasa kupitia maneno na matendo ya wazazi wake, kisha kutoka kwa marafiki au walimu. Baadaye, anaweza kuathiriwa na majirani, magazeti, redio, au televisheni. Ingawa hajui mengi au hata hajui chochote kuhusu jamii asiyoipenda, anapokuwa mtu mzima yeye huwa amekata kauli kwamba watu wa jamii hiyo ni duni na hawaaminiki. Hata anaweza kuwachukia.

Kwa sababu ya kusafiri na kufanya biashara sana, watu wa tamaduni na makabila mbalimbali katika nchi nyingi wanazidi kuchangamana. Hata hivyo, kwa kawaida mtu ambaye amesitawisha hisia kali za ubaguzi hushikilia maoni yake mabaya yasiyo na msingi. Pia anaweza kushikilia maoni yake mabaya kuhusu maelfu au hata mamilioni ya watu, akidai kwamba wote wana sifa mbaya. Akipatwa na jambo baya, hata ikiwa limesababishwa na mtu mmoja tu wa jamii hiyo, atazidi kuwa mwenye ubaguzi. Kwa upande mwingine, jambo lolote zuri linalofanywa na mtu wa jamii hiyo hupuuzwa na kuonwa kuwa jambo lisilotazamiwa.

Kuacha Ubaguzi

Ingawa watu wengi hushutumu ubaguzi kwa maneno, wao huendelea kuwa wenye ubaguzi. Kwa hakika, watu wengi wenye hisia kali za ubaguzi husisitiza kwamba hawana ubaguzi. Wengine husema kwamba si jambo zito, hasa ikiwa watu hawaonyeshi hisia zao za ubaguzi. Hata hivyo, ubaguzi ni jambo zito kwa sababu huwaumiza na kuwagawanya watu. Kutofahamu watu wa jamii nyingine hutokeza ubaguzi, nao ubaguzi hutokeza chuki. Mwandishi Charles Caleb Colton (1780?-1832) alieleza hivi: “Sisi huchukia watu fulani kwa sababu hatuwajui; na hatutawajua kwa sababu tunawachukia.” Lakini, ikiwa mtu anaweza kujifunza kuwa mwenye ubaguzi, anaweza pia kujifunza kuacha ubaguzi. Jinsi gani?

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Je, Dini Zinawafanya Watu Wavumiliane au Wabaguane?

Katika kitabu chake The Nature of Prejudice, Gordon W. Allport anasema kwamba “kwa kawaida, inaonekana washiriki wa Makanisa huwa wenye ubaguzi kuliko watu ambao hawashirikiani na Makanisa.” Hiyo haishangazi kwa kuwa mara nyingi dini imesababisha ubaguzi badala ya kuukomesha. Kwa mfano, makasisi walichochea chuki dhidi ya Wayahudi kwa karne nyingi. Kulingana na kitabu A History of Christianity, wakati fulani Hitler alisema hivi: “Kuhusu Wayahudi, mimi nitaendelea tu na maoni yaleyale ambayo kanisa Katoliki limekuwa nayo kwa miaka 1500.”

Wakati wa visa vya ukatili katika eneo la Balkan, mafundisho ya dini ya Othodoksi na ya Katoliki hayakuwafanya watu wawavumilie na kuwaheshimu majirani wao wa dini tofauti.

Vivyo hivyo, washiriki wa kanisa huko Rwanda waliwachinja waumini wenzao. Gazeti National Catholic Reporter lilisema kwamba mapigano yaliyotukia huko yalikuwa “mauaji halisi na ya kweli ya kabila moja ambayo kwa kusikitisha, hata Wakatoliki wanahusika.”

Kanisa Katoliki limekubali kwamba limehusika katika visa vya ukatili. Katika mwaka wa 2000, Papa John Paul wa Pili aliomba msamaha kwa “matendo ya wakati uliopita ya kukiuka kanuni” wakati wa Misa ya hadhara huko Rome. Katika pindi hiyo, “chuki ya kidini na dhuluma dhidi ya Wayahudi, wanawake, wenyeji, wahamiaji, maskini, na watoto ambao bado hawajazaliwa” ilitajwa waziwazi.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Juu: Kambi ya wakimbizi, Bosnia na Herzegovina, Oktoba 20, 1995

Wakimbizi wawili Waserbia huko Bosnia wakitarajia mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe

[Hisani]

Photo by Scott Peterson/Liaison

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kufundishwa kuwachukia wengine

Mtoto anaweza kupata maoni mabaya kutoka kwa wazazi wake, televisheni, na vyanzo vingine