Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Magazeti Yanayowavutia Watu

Magazeti Yanayowavutia Watu

Magazeti Yanayowavutia Watu

MAGAZETI maridadi na yanayong’aa yametandazwa chini yakingoja yanunuliwe. Ingawa hukukusudia kuyatazama, unavutiwa na picha zake maridadi. Ni kana kwamba magazeti hayo maridadi yanasema, “Ninunue tafadhali!” Ijapokuwa huenda ni kweli kwamba huwezi kuamua yaliyomo katika kitabu kwa kutazama jalada tu, picha za majalada ya magazeti hayo huwavutia wanunuzi. Katika nchi nyingi magazeti hayo hupatikana kwa wingi na kuna mashindano makali ya kupata wateja.

Magazeti yanaweza kugawanywa katika vikundi viwili vikuu: magazeti yanayohusu biashara na ufundi na magazeti yanayolenga kikundi fulani hususa. Magazeti hayo yanayolenga kikundi fulani hususa huzungumzia mambo mbalimbali. Magazeti hayo maridadi hutofautiana na magazeti ya habari katika ukubwa na mambo yanayozungumziwa, kwani yale maridadi huwa madogo na huchapishwa kwenye karatasi bora zaidi ambayo huyafanya yapendeze na kumvutia mnunuzi. Kwa kawaida magazeti maridadi hayazungumzii sana matukio na habari za kila siku kama vile magazeti ya habari. Waandishi wengi huchangia habari mbalimbali zinazoandikwa katika magazeti hayo maridadi, nayo huwa na habari na maoni mbalimbali. Pia huwa na mitindo mbalimbali ya uandishi, kama vile kuripoti mambo au kuzungumzia mambo ya kibinafsi yanayogusa hisia.

Unapotazama magazeti yanayouzwa, uamuzi wako wa kuyanunua au kutoyanunua utategemea mambo kadhaa. Uamuzi wako utategemea sana jinsia yako na vilevile mapendezi yako na hasa bei ya gazeti hilo. Naam, magazeti hayo huwa bei ghali sana labda mara tatu au nne ya magazeti ya kawaida. Lakini gazeti la leo la habari litatupwa na la kesho litanunuliwa, hali gazeti maridadi halipitwi na wakati upesi. Unaponunua gazeti maridadi unaweza kulisoma taratibu na kulihifadhi kwa majuma au miezi na labda hata kuwapa wengine. Wakati mwingine maktaba hupenda magazeti ya zamani na watu fulani hupenda kuyahifadhi.

Je, Yanalingana na Bei?

Bila shaka, wewe mwenyewe ndiye unayeweza kuamua ikiwa magazeti hayo maridadi yanalingana na bei yake. Magazeti hayo huuzwa bei ghali hasa kwa sababu kuyachapisha hugharimu pesa nyingi sana. Ni lazima wachapishaji wafanye utafiti mwingi kuhusu uuzaji kabla ya kuanza kuchapisha gazeti jipya na kuliuza katika soko ambalo tayari lina magazeti mengi. Siku hizi mashirika makubwa huchapisha magazeti 30 au zaidi wakitumia matbaa zao wenyewe. Hata hivyo, mashirika hayo hutumia pesa nyingi sana kwani kila gazeti hutayarishwa na watu tofauti.

Ukitazama ndani ya jalada la gazeti linalolenga kikundi hususa, utashangaa kuona jinsi lilivyo na wahariri na wasimamizi wengi. Kila mmoja wao hushughulikia sehemu tofauti ya gazeti na kuna watu wanaofanya kazi chini yake. Kwa kawaida, magazeti mashuhuri huwa na waandishi na wapiga-picha, lakini wengi wao wamejiajiri au hufanyia kazi makampuni mbalimbali, hivyo wao hupata kandarasi zinazowawezesha kufanya kazi kwa ukawaida au kwa muda mfupi.

Makala zote za waandishi hukaguliwa na wasomaji wa prufu. Nyingi kati ya habari zinazopokewa huandikwa upya au kurekebishwa kwa kiasi fulani na wahariri. Magazeti hayo huwa na picha nyingi, hivyo wachoraji stadi wa picha wanahitajiwa. Wengine huanza kupanga kurasa ili kuamua kitakachokuwa kwenye kila ukurasa. Maandishi na picha zinapaswa kupangwa kwa njia ambayo itamvutia msomaji na kumchochea atazame kila sehemu. Mashirika mengi ya uchapishaji huwa na kitabu kinachoonyesha maneno na mitindo inayopaswa kutumiwa katika magazeti yao. Mhariri mkuu ndiye mwamuzi wa mwisho. Anahitaji kufanya maamuzi haraka ili gazeti lisicheleweshwe. Nakala moja hutayarishwa ili ichunguzwe na wasimamizi kabla ya gazeti kuchapishwa.

Gharama zinatia ndani uchapishaji, ugawanyaji, na vilevile mishahara ya wafanyakazi. Kwa sababu si nakala zote zitakazouzwa, wauzaji wa rejareja hukubali magazeti mengi kwani wanaweza kuyarudisha wasipoyauza. Ni kweli kwamba bei ya gazeti haiwezi kulipia gharama za uchapishaji. Kwa hakika gazeti linalolenga kikundi hususa haliwezi kuendelea kuchapishwa ikiwa halina matangazo mengi ya biashara. Hivi karibuni gazeti moja la kimataifa lenye kurasa 200 lilikuwa na zaidi ya kurasa 80 za matangazo ya biashara. Watangazaji wa bidhaa hutambua kwamba bidhaa zao zitatangazwa vizuri zinapoonyeshwa kwenye kurasa zinazong’aa na zenye rangi kamili.

Huko Australia, inakadiriwa kwamba kwa wastani kila mtu hutumia dakika 1.2 kusoma gazeti kila siku. Na inakadiriwa kwamba kila mtu nchini humo hutumia dakika 1.1 kila siku kutazama filamu au dakika 0.7 kusikiliza muziki. Si ajabu kwamba magazeti ni njia bora ya kuwasilisha matangazo ya biashara.

Kinachowavutia Watu

Ingawa hatuwezi kuyachanganua magazeti yote yaliyochapishwa, acha tuyachunguze kifupi magazeti yanayoandikwa kwa ajili ya wanawake. Hivi majuzi, habari zilizomo katika magazeti hayo zimechunguzwa kwa sababu ingawa watu fulani hawayaoni kuwa mabaya, wengine wanaona kwamba yanawashushia wanawake heshima. Hapana shaka kwamba yanasisimua na kuvutia na hivyo watu wengi huyanunua. Hata hivyo, magazeti ya wanawake yamebadilika katika miaka ya karibuni. Baadhi ya magazeti yaliyokuwa yakizungumzia mambo ya nyumbani sasa yanachapisha makala nyingi kuhusu watu mashuhuri. Pia, makala kuhusu afya zinapendwa sana siku hizi. Wanawake walipenda kusoma hadithi fupi, na hadithi za mfululizo ndizo hasa zilizoongeza mauzo. Lakini sasa ni magazeti machache tu yaliyo na hadithi hizo.

Ni nini kinachofanya magazeti hayo yanunuliwe sana leo? Kile kilichoko kwenye jalada ndicho huwavutia watu. Mwanamke akionyeshwa kwenye jalada, lazima awe mashuhuri au mrembo. Mrembo anayeonyeshwa kwenye jalada anapaswa kuwa kijana mwembamba na kompyuta inaweza kutumiwa kuboresha picha yake. Vipi maneno yaliyo kwenye jalada? Bila shaka, lazima yalingane na umri na hali za maisha ya wasomaji. Majalada ya magazeti fulani huonyesha mitindo, mengine huonyesha zawadi za kushindaniwa. Mara nyingi jalada huonyesha yaliyomo.

Je, Magazeti Maridadi Yanaweza Kutuathiri?

Wachapishaji wa magazeti hudai kwamba wanajua kile ambacho wanawake wanataka. Na ni kweli kwamba wao hufanya utafiti ili wajue kile ambacho wanawake wengi wanataka. Lakini tunapaswa kujiuliza, Je, kweli wanatosheleza uhitaji fulani uliopo, au wanabuni uhitaji huo ili wao wenyewe wautosheleze? Hebu tuchunguze jinsi magazeti mengi ya wanawake huathiri maoni ya watu. Kwanza, magazeti hayo huelezea mtindo wa maisha na maoni ya watu mashuhuri. Huenda hayo ndiyo mambo ambayo watu hupenda kusoma, lakini je, kuna hatari zozote zilizofichika? Katika kitabu chake About Face, Jonathan Cole, mtaalamu wa mfumo wa neva katika Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza, anaonya kwamba kuona sura ya mtu bila kukutana wala kuzungumza naye kunaweza kumfanya mtu adhanie kwamba anamfahamu. Habari nyingi huandikwa kuhusu watu mashuhuri na huenda hilo ndilo linalowafanya watu wahuzunike sana kuhusu kifo cha mtu ambaye hawakumjua lakini ambaye walikuwa wamemwona mara nyingi kwenye magazeti. Bila shaka, habari za televisheni na magazeti zinaweza pia kuwafanya watu wadhanie kwamba wana uhusiano wa karibu na watu wasiowajua.

Jambo lingine linalochunguzwa ni jinsi magazeti yanavyoweza kuathiri maoni ya wanawake kuhusu umbo linalofaa. Ijapokuwa viwango hutofautiana katika nchi mbalimbali, magazeti ya wanawake katika nchi zilizoendelea hupendekeza kwamba kuwa mwembamba ndiyo mambo yote. Walimu fulani, wazazi, na hata wanamitindo wenyewe wameshutumu picha zinazoonyeshwa kwenye magazeti ya wanawake wakisema kwamba zinachangia ongezeko la magonjwa yanayosababishwa na kuhofia kunenepa na zoea la wanawake—hasa wasichana—kuepuka kula.

Ili kuchunguza ukweli wa madai hayo, toleo la Australia la gazeti moja la kimataifa liliwahoji wasomaji wake na kuomba kikundi cha wataalamu kutoa maelezo kuhusu matokeo ya uchunguzi huo. Zaidi ya wanawake 2,000 walishiriki, na asilimia 82 kati yao walikuwa kati ya umri wa miaka 16 na 29. Chati ya uzito uliopendekezwa ilitumiwa na iliorodhesha uzito kulingana na kimo, umri, na kadhalika. Asilimia 60 hivi ya wanawake walifikiri kwamba wao ni wazito kupita kiasi, ingawa ni asilimia 22.6 tu waliozidi uzito uliopendekezwa. Ingawa asilimia 59 ya wale waliokuwa chini ya uzito uliopendekezwa walifikiri kwamba walikuwa na uzito unaopendekezwa, asilimia 58 ya wale wenye uzito uliopendekezwa walifikiri kwamba ni wazito kupita kiasi. Ni asilimia 12 tu walioridhika na uzito wao. Baadhi yao waliichambua chati iliyotolewa na Idara ya Afya ya Australia wakisema kwamba, uzito ulioorodheshwa kwa kila kimo ulikuwa wa juu sana. Isitoshe, asilimia 67 walikubali kwamba nyakati zote walitamani kuwa na umbo la wanawake wengine, na mwanamke 1 kati ya 8 alikubali kwamba ana tatizo la kuhofia kunenepa au zamani alikuwa nalo.

Fiona Pelly, mtaalamu wa lishe aliyekuwa miongoni mwa wataalamu hao, alisema: “Ni wazi kwamba wanawake wanahangaishwa sana na uzito.” Na Dakt. Janice Russell, msimamizi wa hospitali ya magonjwa yanayosababishwa na kuhofia kunenepa huko Sydney alisema: “Jambo lenye kuumiza hata zaidi ni kwamba hisia kama vile hatia na wivu zilionekana wazi [katika uchunguzi huo]. Haifai kuwa na hisia kama hizo nyakati zote.”

Hata hivyo, jambo la maana zaidi lililogunduliwa ni kwamba ingawa baadhi ya waliohojiwa walikubali kwamba waliwaiga waigizaji mashuhuri wa sinema, asilimia 72 walisema kwamba walivutiwa hasa na warembo wanaoonyeshwa kwenye magazeti. Msichana mmoja aliyesaidiwa na hospitali moja inayowaelimisha watu kuhusu lishe alisema kwamba anajivunia kuwa na uzito wa kilogramu 55 lakini akakubali hivi: “Bado, vyombo vya habari, magazeti, na watu mashuhuri hunifanya nitamani kuwa mwembamba zaidi.” Uchunguzi mwingine uliofanywa kwingineko umekuwa na matokeo kama hayo.

Magazeti Mawili Yaliyo Tofauti

Mojawapo ya magazeti mazuri na yenye kuarifu ni hili unalosoma sasa hivi, yaani, Amkeni! Hukulinunua, lakini huenda ulipewa na mtu njiani au labda mtu fulani alikuletea nyumbani. Gazeti hili huchapishwa na kugawanywa ulimwenguni pote na watu waliojitolea, nalo hutolewa bila malipo. Waandishi wa Amkeni! wa kujitolea kutoka sehemu zote za dunia hutuma makala mbalimbali. Wachoraji na watafsiri wake wamejitolea pia. Gazeti la Amkeni! lilitokea kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 1946. Lilichukua mahali pa gazeti la Consolation na The Golden Age, lililoanza kuchapishwa mwaka wa 1919. Magazeti hayo yamechapishwa sikuzote bila matangazo yoyote ya biashara. Kwa sasa Amkeni! linachapishwa katika lugha 87, nalo hutolewa mara mbili kila mwezi katika lugha nyingi kati ya hizo, na zaidi ya nakala milioni 22 husambazwa ulimwenguni pote.

Gazeti la Mnara wa Mlinzi linalochapishwa pamoja na Amkeni! lina rekodi ya kupendeza hata zaidi, kwani sasa linachapishwa katika lugha 148. Nakala zaidi ya milioni 25 za kila toleo la Mnara wa Mlinzi huchapishwa, nalo limesambazwa tangu mwaka wa 1879. Magazeti hayo mawili yamesaidia sana kuwafahamisha watu kuhusu masuala muhimu maishani, nayo huwapendeza wanaume, wanawake, na vijana ulimwenguni pote.

Sote tunapaswa kukumbuka kwamba hatukuzaliwa na ujuzi. Hekima na ujuzi huongezeka tunapoendelea kukua, na mara nyingi maoni na maisha yetu husitawi kutokana na yale tunayosoma. Hiyo ndiyo sababu ni muhimu sana kuchagua habari za kusoma zinazofaa na zenye kujenga.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Magazeti yanaweza kuathiri maoni ya watu kuhusu umbo

[Picha katika ukurasa wa 26]

Nakala zaidi ya milioni 25 za gazeti la Mnara wa Mlinzi huchapishwa katika lugha 148 na nakala zaidi ya milioni 22 za gazeti la Amkeni! huchapishwa katika lugha 87