Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Vituo vya Kuboresha Afya ya Watoto

Vituo vingi vya kuboresha afya ya watoto vimeanzishwa nchini Ujerumani na kwingineko, laripoti gazeti la Frankfurter Allgemeine Sonntagszeitung. Zaidi ya kurembeshwa, watoto wenye umri wa miaka minne hukandwa kwa mafuta yaliyopashwa joto na hupata matibabu mengine. Wataalamu fulani wanaamini kwamba mambo hayo hufanywa ili kupata pesa wala si kuboresha afya ya mtoto. Peter Wippermann msimamizi wa Ofisi ya Mabadiliko ya Kijamii ya Hamburg anasema kwamba “watoto wanaharakishwa kuwa watu wazima” kwa sababu ya faida ya kifedha. Kulingana na Dakt. Christoph Kampmann, msimamizi wa taasisi ya magonjwa ya watoto katika Chuo Kikuu cha Mainz, jambo moja la kuhangaisha ni kwamba “watoto watakuwa wenye ubinafsi na kujiona kuwa bora huku wakijifikiria wenyewe tu.” Ripoti hiyo inasema kwamba badala ya kwenda kwenye vituo vya kuboresha afya kwa sababu ya matatizo yanayotukia utotoni, “watoto wanapaswa kupanda juu ya miti na kucheza-cheza. Kufanya hivyo kutazuia matatizo ya mkao wa mwili, kudhibiti hamu ya kula, na kuboresha usingizi.”

Kilimo Kinachohitaji Maji Mengi

Gazeti Australian linasema: “Australia ndilo bara kavu zaidi, lakini tunatumia maji mengi zaidi ulimwenguni kwa wastani wa kila mtu mmoja.” Kila mtu mmoja huko Australia hutumia lita 900 kila siku ikilinganishwa na lita 600 huko Amerika Kaskazini. Ripoti hiyo inasema: “Robo tatu za maji yanayotumiwa nchini Australia hutumiwa katika kilimo.” Lita 1010 za maji huhitajiwa kuzalisha kilo moja ya ngano. Ili kutokeza lita moja ya maziwa, lita 600 za maji zinahitajiwa kunyunyizia maeneo ya malisho ya ng’ombe. Pia zaidi ya lita 18,000 za maji zinahitajiwa kutokeza kilo moja ya siagi na lita 50,000 za maji zinahitajiwa kutokeza kilo moja ya nyama ya ng’ombe. Pia maji mengi sana yanahitajiwa ili kutengeneza vitambaa. Ili kutokeza kilo moja ya pamba lita 5,300 za maji zinahitajiwa, na zaidi ya lita 171,000 za maji zinahitajiwa kutokeza kilo moja ya sufu. Inakadiriwa kwamba lita 685,000 za maji hutumiwa kutengeneza suti moja tu ya sufu.

Halijoto Inawaathiri Viumbe wa Mwituni

Gazeti The Weekend Australian linasema: “Idadi ya buibui wa Australia kutia ndani buibui hatari wa redback imeongezeka sana huku wanasayansi wakikisia kwamba ongezeko la joto duniani linasababisha ongezeko kubwa la viumbe wa mwituni.” Kulingana na Dakt. Robert Raven wa Jumba la Makumbusho la Queensland, buibui ambao huzaa mara moja kwa mwaka wanatarajiwa kuzaa mara tatu au nne mwaka huu. Anasema: “Buibui ambao wanapaswa kuwa wachanga wakati huu wa mwaka tayari wamekomaa. Tumeona buibui fulani wakiishi mara mbili ya muda wao wa kawaida.” Watafiti pia wanaonelea kwamba halijoto inaathiri ndege. Gazeti hilo linasema: “Ndege kama vile mdiria ambao kwa kawaida hutaga mara moja kwa mwaka, wanataga mara mbili kwa mwaka.” Isitoshe, ndege “wanataga mapema na kurudi mapema kutoka Ulaya kwa sababu majira ya baridi kali humalizika mapema na hilo linaonyesha kwamba huenda mabadiliko hayo yanatukia ulimwenguni pote.”

Miezi Zaidi Yavumbuliwa

Kulingana na gazeti la kisayansi ¿Cómo ves? la Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Mexico, maendeleo ya kiteknolojia yamefanya idadi ya miezi inayojulikana kuwapo katika mfumo wa jua kuongezeka maradufu katika miaka sita. Kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2003, ilijulikana kwamba miezi 136 ilizunguka sayari saba, na wataalamu wa nyota wanatarajia kugundua miezi zaidi ingawa yaonekana Zebaki na Zuhura hazina miezi. Sumbula ina miezi mingi zaidi kati ya miezi inayojulikana (61), ikifuatwa na Sarateni (31), Zohali (27), Kausi (13), na Mihiri (2). Sayari za Utaridi na Dunia zina mwezi mmoja kila moja.

Uchovu Unaweza Kuwa Dalili ya Mshtuko wa Moyo

Toleo la kimataifa la gazeti The Miami Herald linaripoti kwamba kulingana na uchunguzi mmoja “kuchoka isivyo kawaida na kushindwa kulala kunaweza kuwa dalili ya kwamba mwanamke atapata mshtuko wa moyo.” Ingawa asilimia 30 tu ya wanawake waliofanyiwa uchunguzi waliripoti kwamba walihisi maumivu kifuani, asilimia 71 walikuwa wamechoka isivyo kawaida zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kupata mshtuko wa moyo. Profesa Jean McSweeney wa Chuo Kikuu cha Arkansas cha Sayansi ya Tiba anasema kwamba “uchovu huo si wa kawaida na haueleweki” na anaongezea kwamba “wengine huwa wachovu sana hivi kwamba hawawezi kumaliza kutandika kitanda bila kupumzika. . . . Ugonjwa wa moyo ndio unaowaua wanawake sana.” Anasema, “tukiweza kuwasadikisha na kuwafanya wanawake watambue dalili mapema, tutaweza kuwatibu na kuzuia mshtuko wa moyo au kupunguza uwezekano wa kuupata mapema.”

Kuzuia Mafuriko Huko Venice

Jiji la Venice huko Italia lililojengwa kwenye visiwa vipatavyo 120 katika Bahari ya Adriatic, hukumbwa na mafuriko. Baada ya uchunguzi na mijadala mingi, serikali ya Italia imekubali kuanzishwa kwa ujenzi wa vizuizi vinavyoweza kusogezwa kwenye milango mitatu ya bahari hiyo. Vizuizi hivyo vimetengenezwa kwa masanduku ya chuma 79, kila kimoja kikiwa na kimo cha meta 30, upana wa meta 20, na unene wa meta 5. Katika hali za kawaida masanduku hayo yatajazwa maji ili yalale kwenye sakafu ya bahari na kuruhusu usafiri na mtiririko wa maji. Lakini mafuriko yanapotazamiwa, masanduku hayo yatajazwa hewa. Kwa kuwa yanaweza kuelea, yatainuka kutoka sakafuni kama madaraja yanayoweza kusogezwa hadi yafike juu ya maji. Yakiwa karibu-karibu, masanduku hayo yatafanyiza kizuizi kirefu kitakachozuia mafuriko. Inatazamiwa kwamba mfumo huo utaanza kufanya kazi mwaka wa 2011.

Habari za Uvutaji wa Sigara

• Kulingana na jarida la The Wall Street Journal, “watafiti wamegundua kwamba kupigwa marufuku kwa uvutaji wa sigara kwa miezi sita katika baa, mikahawa, na sehemu nyingine za biashara kama hizo huko Helena, Mont[ana], kulichangia kupunguza visa vya watu wanaolazwa hospitalini kwa sababu ya mshtuko wa moyo kwa asilimia 60 hivi.” Mahakama ya eneo hilo ilipoondoa marufuku hayo, idadi ya visa vya watu waliopata mshtuko wa moyo ilirudia kiwango chake cha awali. Daktari wa magonjwa ya moyo, Sidney Smith alisema: “Huo ni uthibitisho wenye nguvu unaoonyesha umuhimu wa kuepuka hatari ya kupumua moshi wa sigara inayovutwa na mtu mwingine.”

• “Serikali za majimbo ambazo hapo awali zilipinga vikali utengenezaji wa sigara, sasa ziko katika hali inayotatanisha: Ziko tayari kusaidia kampuni kubwa zaidi ya kutengeneza sigara nchini,” lasema jarida The Wall Street Journal. Kwa nini? Hakimu mmoja aliamua kwamba kampuni hiyo inapaswa kulipa dhamana ya dola bilioni 12 ili kukata rufani ya kesi. Hilo lingefilisisha kampuni hiyo na haingeweza kulipa serikali hizo za majimbo mabilioni ya dola zilizohitajiwa ili kusuluhisha kesi ya awali. Makala hiyo ilisema serikali za majimbo, “zilianza kutegemea pesa hizo ambazo huwezesha majimbo mengi kuepuka matatizo ya kifedha.” Jambo hilo “lilifanya serikali hizo ziunge mkono kampuni za kutengeneza sigara.” Majuma mawili baadaye hakimu huyo alifanya uamuzi mwingine na kuruhusu kampuni hiyo kulipa dhamana ndogo.